2017-05-28 12:55:00

Papa Francisko: Wakristo dumisheni moyo wa sala na utume


Yesu Kristo Mfufuka kabla ya kupaa kwenda zake mbinguni aliwaambia wafuasi wake kwamba, amepewa mamlaka yote mbinguni na duniani ambayo kimsingi ni nguvu ya Mungu na akawaahidia kuwapatia nguvu ya Roho Mtakatifu yenye utendaji na uweza mkuu unaoweza kuunganisha mbingu na dunia; fumbo linaloadhimishwa kwa Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni. Ni Sherehe inayoonesha kutukuka kwa mwili wa binadamu mbele ya Mwenyezi Mungu, kiini cha imani na matumaini kwamba, daima Mwenyezi Mungu ataendelea kuambatana na binadamu na kwamba, mbinguni, kila mtu anaandaliwa makazi ya milele.

Kumbe, waamini wanapaswa kuishi hapa duniani wakiwa wanayaambata zaidi yale ya mbinguni, kama alivyofanya Yesu kwa kuunganisha mbingu na dunia! Lakini, waamini wanakumbushwa kwamba, licha ya Kristo Yesu kupaa mbinguni, lakini bado anaendelea kuwa pamoja na waja wake hadi utimilifu wa dahali. Huko mbinguni anaonesha ubinadamu wake na wa watu wake na hivyo anaendelea kuwaombea kila siku ya maisha, lakini kwa namna ya pekee kabisa anawaombea msamaha wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, kwa kumwonesha Baba wa milele makovu ya Madonda yake matakatifu, mwaliko wa kujiaminisha mbele yake kwani Yesu ni wakili wa binadamu mbele ya Mungu.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuhitimisha hija yake ya kichungaji Jimbo kuu la Genova, Kaskazini mwa Italia, Jumamosi jioni tarehe 27 Mei 2017. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba,  dhamana na mamlaka ya kuwaombea watu, Yesu amelikabidhi Kanisa lake, changamoto na mwaliko kwa waamini kusali kwa ajili ya nia mbali mbali pamoja na kuhakikisha kwamba, walau wanatenga muda wa sala. Waamini wasipojenga na kudumisha utamaduni wa kusali, watakaukiwa na kunyauka kama kigae, kumbe, wanapaswa kutua nanga ya matumaini ya sala zao mbele ya Mwenyezi Mungu, ili kumwezesha Mungu kupenya uweza wake katika maisha ya binadamu!

Sala ya Kikristo inafumbata mambo mazito katika maisha, kwa kujenga na kudumisha amani na utulivu wa ndani, lakini zaidi kwa kuchukua yote na kumkabidhi Mwenyezi Mungu, ili kuwaombea walimwengu na kwamba, hiki ni kiini cha upendo wa Mungu unaomwalika binadamu kuomba, kutafuta na kubisha hodi bila kuchoka mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Sala inaiwezesha dunia kusonga mbele na Kanisa kutekeleza dhamana na utume wake ambao unaweza pia kufanikiwa kusimamisha vita na amani kurejea tena. Yesu amewatangulia wafuasi wake mbele ya Mwenyezi Mungu, kumbe wasikate tamaa kuendelea kusali ili kuunganisha mbingu na dunia.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukaza kwa kusema, Yesu anawathamini na kuwapenda wafuasi wake, kiasi hata cha kuwashirikisha utume wa kwenda kutangaza, kushuhudia na kuwafundisha wote kuwa ni wafuasi wake, licha ya udhaifu na mapungufu ya waja wake, ikiwa kama wakristo wanadhani watakuwa kwanza watakatifu ndio waanze kazi ya kuinjilisha, kamwe kazi hii haitaanzwa kwani damu wataendelea kuanguka katika mapungufu yao: Udhaifu mkubwa ni pale waamini wanapojifungia katika ubinafsi wao!

Changamoto ni kutoka kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wokovu, kwani Kristo mwenyewe ni nanga ya usalama wa watu wake. Sakramenti ya Ubatizo imewakirimia waamini nguvu ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kwani wao ni mahujaji, wamissionari na wanariadha wa mbio za matumaini; wanyenyekevu na wenye moyo thabiti; makini na wabunifu; wenyeheshima na ufahamu; wachapa kazi, wazi na wenye kuonesha mshikamano wanapotembea kwenye barabara za dunia , ili kuwasaidia watu kumfahamu Kristo Yesu katika maisha yao. Hii ni dhamana pevu inayopaswa kuvaliwa njuga haraka iwezekanavyo!

Na Padre Richard A, Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.