2017-05-28 14:47:00

Papa: ajira, utu na heshima ya binadamu ni muhimu katika uchumi


Baba Mtakatifu Francisko  Jumamosi asubuhi tarehe 27 Mei 2017 ameondoka kuelekea Jimbo kuu la Genova, Kaskazini mwa Italia na alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Cristoforo Colombo wa Genova amelakiwa na viongozi wa Kanisa na Serikali na baadaye aliondoka kwa gari kuelekea kwenye kiwanda cha ILVA Cornigliano na huko majibu maswali manne ya msingi. Kardinali Angelo Bagnasco amemwelezea Baba Mtakatifu Francisko kwamba, wafanyakazi kwa sasa wanakabiliwa na hali ngumu sana ya maisha kutokana na mtikisiko wa uchumi kitaifa na kimataifa na kwamba, waathirika wakuu ni vijana ambao hawawezi kufanya maamuzi magumu katika maisha yao na matokeo yake wanakosa dira na mwelekeo sahihi wa maisha.

Kanisa kwa njia ya sera na mikakati yake ya shughuli za kichungaji limeendelea kuunga mkono juhudi za kuimarisha viwanda vidogo vidogo na vya kati, ili kusaidia familia kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara. Wafanyakazi wamemwomba Baba Mtakatifu neno la faraja na matumaini katika kipindi hiki kigumu cha historia na maisha yao, ili waweze kusonga mbele licha ya changamoto zilizoko mbele yao!

Kumekuwepo na mageuzi makubwa ya viwanda kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, lakini kiwango cha ukosefu wa fursa za ajira kinaendelea kuongezeka kila kukicha, hali inayosababisha mpasuko katika mafungamano ya kijamii. Leo dhana ya kazi haina umuhimu sana kwa watu wengi ambao wanaendelea kuteseka kwa kukosa fursa za ajira. Wanasema, kazi ni fursa ya ushuhuda wa upendo na mshikamano; umoja na udugu wa Kiinjili. Wanamwomba Baba Mtakatifu ili aweze kuwapatia ushauri wa kusonga mbele kwa imani na matumaini! Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika kuwasikiliza na kuwahudumia watu wasiokuwa na fursa za ajira, lakini wakati mwingine, wanaishiwa nguvu ya kusonga mbele kwa kuelemewa sana na athari za ukosefu wa fursa za ajira!

Baba Mtakatifu Francisko akijibu maswali na changamoto hizi zote amesema kwamba, kwa mara ya kwanza katika historia ya maisha yake ameweza kufika Genova, mahali ambapo wazazi wake walipanda Meli kuelekea Argentina kama wahamiaji ili kutafuta fursa ya maisha bora zaidi. Baba Mtakatifu anasikitika kusema, leo hii dhamana na thamani ya kazi imepungua sana kwani si tena kipaumbele cha kwanza kwani kazi ni utimilifu wa utu na maisha ya binadamu. Kanisa linathamini sana kazi na wafanyakazi kwa kutambua kwamba, hata Yesu mwenyewe alifanya kazi chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu. Mahali penye fursa za ajira, hapo kuna ustawi na upendo kwa Mungu na Kanisa.

Ulimwengu wa wafanyakazi ni kipaumbele cha binadamu na Kanisa kwani Amri ya kwanza ambayo Mwenyezi Mungu amemwachia binadamu ni kufanya kazi na kuitawala dunia. Baba Mtakatifu anasema, fadhila za mfanyabiashara bora zinafumbatwa katika: kipaji cha uaminifu na ubunifu; upendo na nidhamu ya kazi; kwa kuthamini na kujali mchango na jasho la wafanyakazi wake. Mfanyabiashara ni muhimu sana katika sera na mikakati ya uchumi! Hakuna uchumi mzuri ikiwa kama hakuna wafanyabishara wema na wachapakazi, wanaoweza kujisadaka bila ya kujibakiza kushiriki katika mchakato wa kubuni fursa za ajira ili kuzalisha bidhaa na kutoa huduma. Jambo la msingi ni kwa wafanyabiashara na wafanyakazi kutambua na kuthamini karama ya kila upande kwani karama hizi zinategemeana na kukamilishana!

Wafanyakazi wanahamasishwa na Baba Mtakatifu kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao kwa juhudi na maarifa; kwa weledi, nidhamu na uwajibikaji mkubwa. Yote haya yakishakutekelezwa kwa dhati, basi mfanyakazi anapaswa kupewa mshahara unaokidhi mahitaji msingi ya binadamu, ili kukuza na kudumisha utu na heshima yake kama mfanyakazi. Mfanyabiashara anashiriki matumaini, mateso na mahangaiko ya wafanyakazi wake; tayari kujadiliana katika ukweli na uwazi, ustawi na maendeleo ya wengi ili kufikia suluhu ya kudumu ya changamoto za ukosefu wa fursa za ajira. Inasikitisha kuona viwanda vinafilisika na hatimaye kufungwa kwani waathirika wakubwa ni wafanyabiashara, lakini zaidi wafanyakazi na familia zao.

Lakini kwa bahati mbaya anasema Baba Mtakatifu kuna wafanyabiashara wanaotafuta faida kubwa kwa kutumia jasho la wafanyakazi wao, hawa ndio katika Injili ya Yesu anawaita wezi na wanyang’anyi wanaotafuta faida kubwa badala ya kuwa ni wachungaji wema wanaopenda viwanda na wafanyakazi wao. Viwanda vinapoheshimu utu wa wafanyakazi, ustawi na maendeleo ya wengi, vinakuwa ni msaada hata kwa maskini. Uchumi usiojikita katika utu na heshima ya binadamu;  mahitaji na haki msingi za binadamu, kuna hatari ya kuwageuza wafanyakazi kuwa ni vichokoo vya kujitafutia mali na utajiri wa haraka haraka. Wanasiasa wakati mwingine wamekuwa ni chanzo cha mitikisiko ya kiuchumi kitaifa na kimataifa kutokana na sera na mikakati ovyo ya kiuchumi pamoja na ukiritimba. Matokeo yake ni kuibuka kwa saratani ya rushwa na ufisadi; kutoweka kwa uaminifu, uwajibikaji na uzalendo: Lakini pamoja na magumu na changamoto za maisha, wafanyabiashara wakweli, waaminifu na waadilifu watastawi kama mtende wa Lebanon.

Wakati fulani Bwana Luigi Einaudi, Rais wa Italia aliwahi kusema kwamba, kuna maelfu ya wafanyakazi wanaozalisha mali na kutoa huduma pamoja na kuweka akiba, lakini katika jamii kuna watu ambao wanawadhulumu na kuwanyanyasa, kiasi cha kuwakatisha tamaa. Kumbe wafabiashara wasiwe na uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka badala yake wawe ni watu wa haki, ari na mwamko wa kutaka kuona maendeleo ya viwanda vyao yakipanuka na kuongezeka kutokana na kuendelea kuwekeza zaidi na zaidi. Wafanyabiashara na wafanyakazi wametakiwa kuwa makini kwa na watu wanaoweza kuwatumbukia katika majanga makubwa ya maisha kutokana na tamaa ya utajiri wa haraka haraka na faida kubwa. Sheria, kanuni na taratibu za kazi zinatakiwa kuangaliwa kwa umakini mkubwa, kwani zinapopindishwa matokeo yake ni watu kukosa fursa za ajira! Wafanyakazi wajenge utamaduni wa sala sanjari na kuhudhuria Ibada ya Misa Takatifu, Jumapili bila kusahau kupata siku ya mapumziko. Mwishoni, Baba Mtakatifu amehitimisha majadiliano na ulimwengu wa wafanyakazi kwa kumwomba Roho Mtakatifu mfariji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.