2017-05-26 14:29:00

Tambua vema ugonjwa wa Fistula usiwe na fikra potofu za ulozi!


Kampeni ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu, UNFPA nchini Kenya dhidi ya ugonjwa wa Fistula ni pamoja na kuzuia, kuimarisha huduma za afya na kuwaunganisha waathirika katika jamii baada ya kunyanyapaliwa. Dkt Dan Okoro, Afisa wa Afya ya Uzazi wa Mpango, UNFPA nchini Kenya amesema mbinu moja katika kuzuia, ni kuhakisha mgonjwa anayetibiwa anapewa masharti na kuyafuata. Hata  nchini Tanzania, shirika hilo la UNFPA limekaribisha hatua ya Wizara ya Afya ya kujipanga kutafiti hali ya Fistula nchini humo.

Akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa  meneja programu ya afya ya uzazi, mama na mtoto  wa UNFPA Bi. Felista Bwana amesema hatua hiyo itatoa fursa ya kuandaa mpango mkakati unaolenga kutibu na kutokomeza fistula.Na kuhusu fikra potofu kuwa mwenye Fistula amelogwa, Bi. Bwana amesema, Fistula si ulozi wala laana, bali watu waenda hospitali wakatibiwe. Bi. Bwana ametaja hospitali kadhaa zinazotibu Fistula nchini Tanzania kuwa ni pamoja na CCRBT jijini Dar es salaam, Bugando mkoani Mwanza na Seliani huko Arusha.

Tambua ugonjwa huu wa Fistula:
Fistula ni shimo ambalo hutokea kati kati ya kibofu cha mkojo na uke au kati kati ya njia ya haja kubwa na uke wa mwanamke ambaye amejifungua kwa shida. Shimo hutokea pale ambapo kichwa cha mtoto ni kikubwa kuliko njia ya uzazi. Fistula inasababishwa na  kusukuma mtoto wakati wa kujifungua kwa mda mrefu bila usaidizi au matibabu yeyote, na anachanika  katika njia ya uzazi na kusababisha shimo, hivyo husababisha uvujaji wa kinyesi na mkojo bila kujizuiia.  Aidha kujifungua  mapema kabla ya umri kumekuwa chanzo kikubwa cha kutokea fistula, hilo linatokana na kutopevuka kwa njia za uzazi pamoja na nyonga. Wataalamu wa afya wanabaini fistula mara nyingi hutokea kwa wanawake wanaojifungulia majumbani baada ya kukosa matibabu. Ni  vema na wajibu kwamba mara kwa mara kwa wajawazito kujifungua katika kituo cha matibabu ili waweze kufuatiliwa na kupata huduma za matibabu kwa wakati mwafaka. 

Dalili: Kama unahisi kutokwa na mkojo bila kujizuia, harufu mbaya, maumivu makali sahemu za uzazi unashauliwa kuwahi hospitali au kituo cha afya kilipo karibu ili upate ushauri na matibabu zaidi.Matibabu ya fistula ni bure katika hospitali zote nchini.

Sr angela Rwezaula 
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.