2017-05-26 15:03:00

Papa Francisko: Jitoeni kwa Mungu ili kuwa yote kwa ajili ya jirani!


Watawa Wadogo Wamissionari wa Upendo wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanatangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa jirani, lakini zaidi kwa maskini, waliotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii kama ambavyo kauli mbiu ya maadhimisho ya mkutano mkuu wa 12 wa Shirika inavyowataka “Kujitoa kwa Mungu ili kuwa yote kwa kwa ajili ya jirani”. Hii ni changamoto ya kuwa kweli mitume wamissionari, mashuhuda na vyombo vya Injili ya upendo hasa kwa wale walioko pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 26 Mei 2017 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa 12 wa Shirika la Watawa Wadogo wa Missionari wa Upendo. Ametumia fursa hii kuwashukuru kwa niaba ya Mama Kanisa kwa utume wanaoutekeleza miongoni mwa: wanawake na watoto; wagonjwa wa afya ya mwili na akili; utume miongoni mwa vijana shuleni na wazee; katekesi makini pamoja huduma mbali mbali kwa familia ya Mungu. Hii ni dhamana ya uinjilishaji inayojikita katika utambulisho wa kimissionari unaomwilishwa katika huduma kwa maskini, ili kuwatangazia na kuwashuhudia furaha ya Injili, wema, huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu uliofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu.

Hii ni huduma makini inayofumbatwa kwa namna ya pekee kwa kukutana na watu, kwa njia ya majadiliano sanjari na kuambatana nao kama mbinu ya kimissionari inayotekelezwa na watawa hawa! Huduma kwa maskini, inawahamasisha kutoka katika hali ya kujitafuta wenyewe, ili kutembea, kupandikiza na kujikita katika wongofu wa shughuli za kichungaji ili nyenzo zote ziweze kutumika katika mchakato wa uinjilishaji na huduma kwa karama ya Shirika, jambo ambalo linahitaji uhusiano wa karibu sana na Mwenyezi Mungu, ili kujenga umoja wa kimissionari!

Utume wa Kanisa unazaliwa kwa kukutana na Kristo kiini chake; aliyetumwa na Baba wa milele, anayewaita na kuwatuma ili kwenda kufanya kazi katika tamaduni mbali mbali. Kama wamissionari wanapaswa kuwa na ari na kipaji cha ubunifu kwa kusoma alama za nyakati katika sera na mikakati yao ya shughuli za kichungaji mintarafu mwanga wa Roho Mtakatifu na jicho la Kristo Mchungaji mwema; bila kuhukumu bali kutafuta uwepo endelevu wa Mwenyezi Mungu katika historia ya mwanadamu; kwa kutafakari na kuzama katika imani; kwa kuheshimu, kuhurumia, kuganga, kuponya na kurafiji, tayari kutafuta njia na mbinu mpya ya kuwafikishia watu wengi zaidi Habari Njema ya Wokovu ambayo ni Kristo Yesu!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mmissionari anapaswa kuwa ni mtu huru, asiyemezwa na malimwengu, tayari kutoka na kuishia katika hija ya maisha ya huduma, ili kushirikishana na wengine zawadi ya Injili. Anapaswa kuwa ni mtu mwepesi anayejitaabisha kutafuta utukufu na ukuu wa Mungu katika maisha yake; mtu ambaye daima yuko katika hija ya toba na wongofu wa ndani, anayejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya wongofu wa shughuli za kichungaji. Ni mtu ambaye ameyageuza maisha yake kuwa ni maskani ya Roho Mtakatifu anayemkumbusha, anayemwongoza katika utimilifu wa ukweli, anayemfundisha na kumwezesha kuwa kweli ni shuhuda wa Injili ya Kristo. Yote haya yanahitaji unyenyekevu unaokua na kukomaa kila siku, tayari kutambua na kuthamini uwepo wa Kristo Yesu kati pamoja na maelfu ya watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, changamoto hata kwa watawa hawa kujiaminisha kwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza katika maisha na utume wao!

Mmissionari wa kweli lazima ayasimike maisha yake katika Kristo Yesu na Neno lake; Liturujia, tasaufi ya maisha ya kiroho  inayomwambata mtu mzima, ili kumkamilisha bila kuwatenga wengine; kwa kusimika maisha yake hapa duniani, lakini akiwa na mwelekeo wa kwenda mbinguni; daima akikuza ndani mwake taamuli, unabii, utume na ushuhuda makini! Mmsionari anapaswa kuwa ni nabii wa huruma ya Mungu, safari endelevu inayofumbatwa katika unyenyekevu na unabii kadiri ya sura ya Mwenyezi Mungu. Huduma yao ya kimissionari iwasaidie kutekeleza unabii wa huruma kwa kumweka Mwenyezi Mungu kuwa ni kiini cha maisha yao sanjari na kuuangalia Msalaba uliosimikwa duniani! Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka wawe tayari kusikiliza na kujibu kilio cha maskini kutoka sehemu mbali mbali za dunia; watangaze huruma na upendo wa Mungu, chemchemi ya furaha, utulivu na amani ya ndani. Baba Mtakatifu anawataka watawa hawa kushirikiana na watawa wengine wanaounda familia ya Don Orione kwa kushirikishana karama ili kutembea na kushirikiana, daima wakiwa wenye haraka katika huduma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.