2017-05-25 16:42:00

Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni: Utukufu wa ubinadamu!


Siku arobaini baada ya Ufufuko wa Kristo Kanisa huadhimisha Sherehe ya kupaa Bwana mbinguni. Sherehe hii huadhimishwa siku ya Alhamisi baada ya Dominika ya 6 ya Pasaka na kutokana na changamoto za kichungaji huweza kusogezwa mbele na kuadhimishwa katika Dominika ya 7 ya Pasaka na hivyo kutoa fursa kwa waamini wengi kuisheherekea siku hii. Katika sala ya mwanzo tumesema: “huko alikotutangulia yeye kichwa chetu, ndiko tunakoamini kufika sisi tulio mwili wake”. Tunaadhimisha tukio la furaha sana katika historia ya ubinadamu wetu kwani mbingu na dunia vinaungana tena. Yeye aliutwaa ubinadamu wetu anakuwa mwakilishi wetu huko juu mbinguni. Ubinadamu wetu uliokombolewa, ulio katika hali ya utukufu wa ufufuko sasa unakaa pamoja na Mungu huko juu mbinguni.

Somo la kwanza linatupatia mambo mawili: kwanza linatupatia hakika ya kwamba huyu aliyepaa mbinguni ni Kristo Mfufuka. Anapaa mbinguni baada ya ufufuko wake na baada ya kuwahakikishia wafuasi wake kuwa ni Yeye kweli amefufuka: “aliwadhihirishia nafsi yake, kwa dalili nyingi, baada ya kuteswa kwake, ya kwamba yu hai, akiwatokea muda wa siku arobaini, na kuyanena mambo yaliyohusu ufalme wa Mungu”. Dokezo hili ni muhimu katika imani yetu kwani tunaitafakari hadhi yake huyu anayepaa mbinguni. Yupo katika mwili wa utukufu na anapaa kwenda kuungana na Baba aliye mtukufu. Ni dokezo kwetu kuwa ni katika hali hiyo ya utukufu ambayo tunarithishwa kwa njia ya Kristo katika Roho Mtakatifu ndipo nasi tunaungana na Mungu.

Ufufuko wa Kristo unapyaisha tena ubinadamu wetu ambao ulichakazwa na dhambi. Mwili wake wa utukufu hauchangamani tena na dhambi bali unakwenda kuungana na Mungu mtukufu. Hadhi hii inapasika kuhisiwa na binadamu wote na kusema kwa shangwe kubwa kama Papa Leo mkuu: “Ewe Mwanadamu, kitambue cheo chako”. Cheo chetu ambacho tulikuwa nacho tangu wakati wa uumbaji ni kuwa pamoja na Mungu. Dhambi ndiyo ilimfukuzisha mwanadamu kutoka bustani ya Edeni mahali ambapo Bwana Mungu alimwandalia mwanadamu na daima alimtembelea.  Baada ya dhambi ya kwanza Mungu “alimtoa mwanadamu katika bustani ya Edeni, alime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa. Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima” (Mw 3:23 – 24). Kwa ufufuko na kwa kupaa kwake mbinguni Kristo anamrudisha tena mwanadamu katika kutaniko hili la Mungu.

Pili anawapatia mitume wake utume akisema: “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi”. Sehemu hii inatuunganisha na somo la Injili ya leo ambapo tunatumwa kwenda kuitangaza habari njema. Kristo mfufuka kabla ya kupaa mbinguni anawatuma mitume wake, ambao ni jamii ya kwanza ya wanadamu kushirikishwa hali yake ya kimungu, kuisambaza habari njema yaani wokovu wa mwanadamu kwa watu wote. Hili ni dokezo muhimu kwamba Yeye hakuja kwa ajili ya kuwapeleka wachache (kikundi kidogo alichokuwa nacho wakati wa maisha yake hapa duniani) mbinguni bali kwa ajili ya wanadamu wote: “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi”.

Utume huu unapatiwa nyenzo ya msaada, Roho Mtakatifu ambaye Kanisa zima kwa sasa lipo katika novena maalum ya kuomba ujio wake. Roho huyo ni uhakikisho wa uwepo wa Mungu pamoja nasi na uthibitisho wa ahadi ya Kristo akisema: “mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari”. Nafasi hii ya Roho Mtakatifu inatuonya kwamba Kanisa katika kutume wake lisiuweke kando uwepo wa Roho wa Mtakatifu. Utume wote wa Kanisa ni muendelezo wa utume wa Kristo. Yeye anathibitisha kuwa pamoja nasi daima kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu ndiye anauhisha upya ndani mwetu uwepo na Mungu na kutufanya upya katika Kristo. Fumbo la Umwilisho linajionesha kwa namna kuu kabisa kwa sherehe ya leo, muunganiko wetu na Kristo ambao unatupatia sisi utume wa kuwa mashhuhuda wa Kristo kwa watu wote na unawezeshwa na Roho Mtakatifu.

Kristo anapopaa mbinguni anakwenda kututayarishia makao. Yeye mwenyewe aliahidi akisema kwamba “naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwanu; ili nilipo mimi, nanyi muwepo” (Yoh 14: 2 – 3). Kabla ya kupaa kwake alituthibitishia kuwa anakokwenda ni kwa Baba yake na Baba yetu, kwa Mungu wake na Mungu wetu (Rej Yoh 20:17). Hii ni ahadi ya matumaini na sababu ya kupata nguvu kwenda kuitangaza Injili ya Kristo. Ni ahadi inayotupatia nguvu kwani tunaona moja kwa moja tunaitangaza habari inayotuhusu sisi wenyewe kwani tunayemtangaza ameungana nasi, ni Kristo ndugu yetu na mwishoni tutamkuta anatusubiri mbinguni kwa Baba yake na Baba yetu. Hivyo utume wetu wakristo ni kwenda kushuhudia na kuifunua hadhi hiyo kwa watu wote.

Ushuhuda wa upya wa maisha hujidhihirisha kwa namna nyingi lakini Kristo aliweka upendo kuwa njia mahsusi ya utambulisho wetu: “Watu watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi” (Yoh 13:35). Utangazaji wetu wa habari njema utapata nguvu zaidi katika matendo yetu mema yanaoufunua upendo wa Mungu kwa wengine. Katika nyakati zetu hizi tumekuwa na mabingwa walioonesha kwamba kweli sasa ubinadamu umeungana na umungu. Kati yao ni Mama Theresa wa Calcutta ambaye mkutano wake wa ndani na Kristo umemfanya kuwa kioo cha utume wa upendo kwa watu wote hasa maskini na wanaoteseka na alama ya ukristo wetu kwa watu wote. Ulimwengu umeitambua tunu iliyopo ndani mwake; ulimwengu umeonja kwamba kweli umungu na ubinadamu umekutana kwani wote waliuonja upendo wa Mungu kupitia nafsi ya Mama huyu Mtakatifu.

Tunapoalikwa kuwa mashuhuda wa upya huo tunapokea changamoto kubwa. Tunashuhudia leo hii watoto wengi wanateseka na kukosa haki zao za msingi, akina mama wengi wananyimwa haki zao, wanyonge wengi wanazidi kudidimizwa kwa vitendo vya rushwa. Katika neno moja ni kwamba, tunashuhudia ubinadamu uliojeruhiwa. Katika hali hii hamu ya upendo wa Mungu inatawala mioyo yao. Mwanadamu katika mazingira haya ana kiu ya kumwona Mungu. Furaha ya sherehe ya leo itapata maana pale tutakapowashirikisha wenzetu katika hali hiyo ya mahangaiko tone la upendo wa Mungu. Sisi tunafurahi na tunapata nguvu sababu tumehakikishiwa kuwa ubinadamu umeungana na mbingu lakini furaha hii si yetu binafsi, ni zawadi ambayo inatuita kutoka nje na kuwashirikisha wengine.

Kristo anapopaa mbinguni na kuunganisha ubinadamu wetu na mbingu anataka pia kwa namna nyingine kuweka mamlaka ya kimungu hapa duniani. Katika Injili anatuambia kwamba: “nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani”. Hii ni kutonesha kwamba yatendekayo duniani yanaunganika na yale ya mbinguni na mamlaka yanayotawala ni yale Kristo. Mamlaka haya ya Kristo yanajikita katika ukweli ambao fumbo la Kristo linaujumuisha. Hivyo ushuhuda wa maisha ambao Kristo anatutuma kuutangaza unapaswa kujikita katika hilo. Ni wajibu wetu sote kama wana Kanisa kuuambia ulimwengu huu ukweli huo, kuyastawisha mamlaka hayo ya Kristo katika jamii ya wanadamu.

Mausia ya Mtakatifu Paulo katika somo la pili yawe dira kwetu. Tuiombe roho ya hekima na kuujua ukuu tuliofanyiziwa. Tujitoe bila kujibakisha katika utume wetu ili kumshuhudia Yeye aliyepaa mbinguni kututayarishia makao. Hilo litakuwa ni tendo la shukrani kwetu kwani huduma yetu hiyo itawafikia wote na hivyo malengo ya utumishi wake, yaani wokovu kwa watu wote yatatimia. Mwishoni, kama tulivyoomba katika sala ya mwanzo tutafika huko alikotutangulia Yeye aliye kichwa chetu.

Kutoka studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.