2017-05-24 16:02:00

Melania Trump ashuhudia Injili ya huduma na huruma kwa watoto wagonjwa


Melania Trump, Mke wa Rais Donald Trump wa Marekani baada ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican, Jumatano, tarehe 24 Mei 2017 wametembelea Kikanisa cha Sistina pamoja na Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican pamoja na maeneo ya kihistoria yaliyoko mjini Vatican. Baadaye, First Lady Melania amekwenda kutembelea Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican. Amekutana na kusalimiana na watoto pamoja na familia zao!

Alipowasili hospitalini hapo amepokelewa na Dr. Mariella Enoc, Rais wa Hospitali ya Bambino Gesù pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Hospitali hii! Hawa ni Dr. Massimilliano Rapono, Mkurugenzi wa huduma ya afya; Dr. Bruno Dallapiccola, Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Dr. Ruggero Parrotto, Mratibu mkuu wa Hospitali. Melania Trump ameweka shada la maua kwenye Sanamu ya Bikira Maria iliyoko hospitalini hapo na baadaye kutembelea sehemu mbali mbali za Hospitali ya Bambino Gesù hasa idara ya upasuaji, idara ya magonjwa ya moyo na idara ya wagonjwa mahututi waliofanyiwa operesheni ya moyo ambako wamelazwa watoto wachanga sana!

Melania Trump ametumia muda mwingi kusalimiana na kucheza na watoto wagonjwa na hatimaye, kupewa zawadi ya kitabu kinachosimulia historia na hali halisi ya maisha ya watoto wagonjwa wanaotibiwa hospitalini hapo kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kabla ya kuondoka hospitalini hapo, Melania Trump ameweka sahihi kwenye kitabu cha wageni mashuhuri kwa kusema amefarijika sana kuwatembelea na kuwataka waendelee kuimarika huku wakiwa na mwelekeo chanya wa maisha! Melania Trump anasema, anawapenda sana! Melania Trump pia amepata nafasi yak usali na kutafakari kwa kitambo kidogo kwenye Hospitali ya Bambino Gesù na hatimaye, kuondoka na kuendelea na safari yake mjini Roma.

Dr. Mariella Enoc, Rais wa Hospitali ya Bambino Gesù amesema, wamefurahishwa sana kupata ombi kutoka kwa Melania Trump la kutaka kutembelea Hospitali ya Bambino Gesù na kwamba, wanamshukuru Mungu kwa kuweza kumtembeza mgeni wao mashuhuri katika hospitali ambayo inajipambanua kwa huduma msingi za tiba kwa watoto wadogo na tafiti za kisayansi zinazotambulika kimataifa. Hii ni huduma ya Injili ya upendo inayotolewa na Vatican kwa ajili ya watoto kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaohitaji tiba makini zaidi.

Viongozi wa Hospitali ya Bambino Gesù wanamshukuru Mungu kwa kuwawezesha kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa watoto wagonjwa, tema inayopewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko! Hii ni huduma kwa watoto wenye magonjwa adimu kutoka sehemu mbali mbali za dunia! Hospitali hii ilianzishwa kunako mwaka 1869 na kuwa ni hospitali ya kwanza kabisa kutoa huduma kwa watoto wagonjwa nchini Italia. Kunako mwaka 1924 hospitali hii ikatolewa zawadi kwa Vatican. Mwaka 2006 ikapata hadhi na kutambuliwa kimataifa kama Hospitali maalum kwa ajili ya kutibu magonjwa ya watoto. Mwaka 2014 ikafungua maabara mpya kwa ajili ya kuboresha tafiti za magonjwa ya watoto kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hospitali hii inahudumiwa na wafanyakazi 2, 500 na inashirikiana na wataalam na mabingwa wa magonjwa ya watoto kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hospitali hii inashirikiana na nchi mbali mbali kwa ajili ya huduma kwa watoto wagonjwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.