2017-05-23 14:34:00

Papa Francisko: Nendeni mkatangaze na kushuhudia furaha ya Injili!


Kuna Wakristo wengi ambao wamepoteza maisha yao kwa kunyanyaswa na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Ni watu ambao kamwe hawakukubali kumezwa na malimwengu, wakawa tayari kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Injili ya Kristo. Kati yao ni Mwenyeheri Oscar A. Romero aliyeuwawa kikatili wakati akiadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na sasa imekwisha kutimia miaka miwili tangu alipotangazwa na Mama Kanisa kuwa ni Mwenyeheri. Ni kiongozi wa Kanisa aliyesimama imara kupambana na nyanyaso na dhuluma dhidi ya maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 23 Mei 2017. Hapa anasema, kuna haja ya kuvuka kutoka katika kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa woga na mashaka na kuanza kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu kwa waja wake kama ilivyotokea kwa Mtume Paulo na Sila waliokemea pepo mchafu kwa jina la Yesu na kumtoka yule kijakazi saa ile ile watu wakatambua kwamba, Paulo na Sila walikuwa ni watumishi wa Mungu aliye hai.

Kwa Mtume Paulo akatambua mara moja kwamba, hii haikuwa ni njia sahihi ya kuwaongoa watu wa Filipi, kwani walikuwa ni vuguvugu bila hamasa hata kidogo na matokeo yake wakaanza kuwashitaki, kuwashambulia na hatimaye kutupwa gerezani, tena kwenye chumba cha ndani kabisa na kufungwa miguu kwa mkatale. Huu ni ushuhuda ambao umetolewa na wakleri, watawa na waamini walei sehemu mbali mbali za dunia. Kati yao ni Mwenyeheri Oscar Romero aliyesimama kidete kutangaza na kushuhudia ukweli, kiasi hata cha kuhatarisha maisha yake na Kanisa katika ujumla wake.

Wananchi wa Filipi walikasirika kutokana na Mitume wa Yesu kumponya yule kijakazi kwani waliwaharibia nguvu kazi ya bure! Baba Mtakatifu anakaza kusema, shetani daima anapenda kuingia kwa watu kwa kutumia fedha. Hali kama hii ni hatari kabisa hata kwa Kanisa! Pale ambapo Kanisa limetulia tuli kama “maji mtunguni” hapo kuna hatari ya kumezwa na malimwengu. Waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili kama walivyokuwa Mtume Paulo na Sila, kwani licha ya kucharazwa viboko na kufungwa gerezani, bado waliendelea kusali na kumsifu Mungu.

Walikuwa na furaha ya ajabu kiasi hata cha kuokoa maisha ya mlinzi wa gereza aliposhuhudia matendo makuu ya Mungu kwa watumishi wake, akadhani kwamba, walikuwa wametoroka kutoka gerezani. Baba Mtakatifu anasema, hii ni sehemu ya simulizi la Sura ya Kumi na Sita ya Kitabu cha Matendo ya Mitume. Yule mlinzi wa gereza, akashirikishwa furaha ya Injili, akatubu na kubatizwa. Huu ndio mchakato unaopaswa kufanywa na waamini kila siku ya maisha yao, kwa kuondokana na malimwengu na kuanza kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake; tayari kutangaza na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Ni wongofu wa kutoka katika dini inayotafuta kujinufaisha yenyewe na kuanza kutembea katika ushuhuda unaomtangaza Yesu kuwa ni Bwana na Mwokozi! 

Huu ndio muujiza unaotekelezwa na Roho Mtakatifu kwa mashahidi na waungama imani wa Kristo kwa nyakati zote. Baba Mtakatifu mwishoni mwa mahubiri yake anasema, Kanisa linasimama na kuendelezwa kwa ushuhuda wa waungama imani na wafiadini. Hili ni Kanisa linalomtangaza Kristo Yesu kuwa ni Bwana na liko tayari kupambana na pepo wachafu. Changamoto kwa waamini ni kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya kuendelea kulipyaisha Kanisa katika ujana unaofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani, tayari kuwa ni shuhuda na chombo cha furaha ya Injili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.