2017-05-22 16:36:00

Vielelezo vya utajiri wa Kanisa: Maskini, Injili na Ekaristi Takatifu


Huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii katika Parokia ya Mtakatifu Pier Damiani, Jimbo kuu la Roma iliyotembelewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 21 Mei 2017 ni matunda ya kongamano la Jimbo kuu la Roma lililokuwa linaongozwa na kauli mbiu “Ekaristi Takatifu na ushuhuda wa upendo”. Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki, Caritas, Parokiani hapo linajitahidi kutoa huduma ya chakula kwa maskini; huduma ambayo inawashirikisha wanaparokia wote, kila mtu kadiri ya nafasi na uwezo wake. Kuna familia 50 zinazohudumiwa chakula parokiani hapo.

Hii inatokana na ukweli kwamba, katika miaka ya hivi karibuni watu wengi wameathirika sana kutokana na mtikisiko wa uchumi kitaifa na kimataifa. Kuna watu wengi hawana tena fursa za ajira, kumbe wanasaidiwa parokiani hapo. Baba Mtakatifu anasema, maskini ni kito cha thamani sana katika maisha na utume wa Kanisa! Ni amana na utajiri wa Kanisa kama amabvyo ulishuhudiwa na Shemasi Laurent, mwanzo kabisa mwa madhulumu ya Kanisa. Umaskini wa hali na kipato ni matokeo ya mambo mengi yanayowasibu watu. Kanisa lina dhamana na wajibu wa kuwasaidia na kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kusaidiwa na Yesu wa Ekaristi Takatifu.

Fumbo la Ekaristi Takatifu linaadhimishwa vyema, ikiwa kama Kanisa litawawaheshimu na kuwathamini maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, hawa ni kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo kati ya waja wake; ni sehemu ya Fumbo la Msalaba. Utajiri wa Kanisa unafumbatwa pia katika Injili! Jambo la msingi ni kuwa maskini kiasi kwamba, shetani mara nyingi anapenda kutumia nafasi na mianya ya kiuchumi kwa ajili ya kuwavuruga watu. Anaingilia mfukoni na matokeo yake ni hatari kubwa sana kwa watu!

Ukiritimba na rushwa ni hatari sana kwa ustawi na maendeleo ya watu! Kanisa halina budi kusimama kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya ufukara kwa njia ya huduma makini kwa maskini, ili kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima yao. Yesu alizaliwa katika hali ya umaskini mkubwa na katika maisha na utume wake, aliwataka wafuasi wake kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini katika maisha na utume wa Kanisa. Kupenda maskini hakumaanishi kuwachukia matajiri na watu wenye uwezo, bali kuwaombea ili kweli waweze kutumia vyema rasilimali fedha kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, kwani utajiri wao ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anawashukuru watu waliobahatika kuwa na utajiri na wakautumia kwa ajili ya huduma kwa maskini kwani kuna wengine ambao utajiri wao umewatumbukiza mahali pabaya sana katika maisha, kiasi cha kumezwa na ubinafsi na uchoyo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.