2017-05-22 16:03:00

Jumuiya ya Kimataifa iwekeze matumaini kwa vijana na familia!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 22 Mei 2017 amekutana na kuzungumza na Bwana Michael D. Higgins, Rais wa Ireland pamoja na ujumbe wake, ambaye, baadaye walikutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa. Viongozi hawa wawili katika mazungumzo yao ya faragha wamegusia umuhimu wa kuendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano kati ya Vatican na Ireland.

Baadaye, Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake Rais Higgins wamegusia masuala mbali mbali yenye mafao na manufaa kwa ustawi na maendeleo ya wengi. Kati ya mambo haya ni umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu; utu na heshima yake katika kila hatua ya maisha. Wamegusia changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani na umuhimu wa kuonesha upendo na ukarimu kwa wahamiaji hawa wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote sanjari na kujikita katika maendeleo endelevu.

Baba Mtakatifu Francisko na Rais Michael D. Higgins wa Ireland kwa namna ya pekee kabisa wamejikita katika mchakato wa ujenzi wa tunu msingi za maisha kwa vijana wa kizazi kipya pamoja na familia; umuhimu wa kukumbatia kanuni maadili ili kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, hasa kuhusiana na maswala ya kiuchumi. Mwishoni, waliweza kubadilishana mawazo kuhusu mustakabali wa Bara la Ulaya kwa siku za usoni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.