2017-05-22 14:50:00

Dhamana na nafasi ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa kanisa!


Roho Mtakatifu ndiye anayewafundisha waamini kumwita Kristo Yesu kuwa ni Bwana, mwaliko ni kumsikiliza kwa makini, ili hatimaye, kumtangaza na kumtolea Yesu ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Waamini wanapaswa kumfungulia Roho Mtakatifu malango ya akili na nyoyo zao ili kusikiliza wosia ambao Yesu mwenyewe aliwaachia mitume wake alipowaambia kwamba, kamwe hata waacha yatima, atawapelekea Roho wa kweli, Msaidizi ambaye ni Roho Mtakatifu Mfariji na mtetezi wao mbele ya Mwenyezi Mungu. Huu ni wosia ambao Yesu mwenyewe aliwapatia wafuasi wake wakati wa Karamu ya mwisho.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 22 Mei 2017 wakati Mama Kanisa anaadhimisha pia kumbu kumbu ya Mtakatifu Rita wa Cascia. Baba Mtakatifu amekita mahubiri yake juu ya nafasi na dhamana ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa, kwani ndiye anayelijalia Kanisa usalama wa kuokolewa na Kristo Yesu. Roho Mtakatifu anawawezesha waamini kumkiri, kumtangaza na kumshuhudia Kristo mbele ya watu wa Mataifa, kiasi hata cha kuwafunulia na kuwasindikiza katika kuufikia ukweli wote.

Roho Mtakatifu ni mwanandani wa mwamini, anayemsindikiza katika hija ya maisha yake hapa duniani; ni mwanandani pia wa Kanisa, zawadi kubwa ambayo Yesu analiachia Kanisa lake. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waalimi kumfungulia Roho Mtakatifu malango ya maisha na nyoyo zao kama alivyofanya Lidia, mwenye kuuza nguo za rangi ya zambarau, mcha Mungu; ambaye moyo wake ulifunguliwa na Bwana ili ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo Mtume. Mama huyu alifungua moyo wake na Roho Mtakatifu akaingia kwake, lakini haiwezekani kwa moyo uliofungwa na wala hapa hakuna ufunguo wa bandia! Hii ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambayo waamini wanapaswa kumwomba ili Roho Mtakatifu awasaidie kumtambua, kumkiri na kumshuhudia Kristo Yesu kuwa kweli ni Bwana! Waamini wasali daima ili kumwomba Roho Mtakatifu katika maisha yao, tayari kumsikiliza kwa makini na kutekeleza matakwa yake, ili kumtangaza na kumshuhudia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.