2017-05-20 12:32:00

Sinodi ya Maaskofu: Vijana chakarikeni vyema ninyi ni wadau wakuu!


Mama Kanisa anapenda kuwaangalia vijana kwa jicho la upendeleo kama alivyofanya Kristo Yesu kwa Mtume Yohane, yule mwanafunzi aliyempenda zaidi, kiasi kwamba, akawa ni shuhuda makini wa mateso, kifo na ufufuko wake! Mama Kanisa anawataka vijana wa kizazi kipya wawe ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili; vyombo na mwanga wa imani, matumaini na mapendo; wawe kweli ni mashuhuda na wajenzi wa furaha ya upendo katika familia. Kanisa linataka kujenga na kudumisha utamaduni wa kuwatambua vijana kuwa jeuri ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake; kuwasindikiza na kuandamana nao, ili waweze kufanya maamuzi magumu katika maisha yao kwa ujasiri na ari kuu zaidi pamoja na kutambua kwamba, Kanisa ni mama mwema anayewapenda na kuwatakia mema vijana wa kizazi kipya!

Mama Kanisa kwa kutambua na kuthamini mchango wa vijana wa kizazi kipya katika maisha na utume wake, ameamua kuitisha maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayotimua vumbi mwezi Oktoba, 2018 hapa mjini Vatican kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Mama Kanisa anataka kuona furaha na upendo vikibubujika kutoka katika maisha ya vijana wa kizazi kipya, mambo msingi yanayofumbatwa katika Nyaraka za Kitume zilizotolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na Papa Francisko.

Hii ni changamoto endelevu ambayo imefanyiwa rejea na Kardinali Lorenzo Baldisseri wakati wa ziara yake ya kichungaji huko Taiwan alipokutana na kuzungumza na Baraza la Kanda ya Maaskofu Katoliki wa China. Vijana wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika mchakato wa maandalizi, maadhimisho na hatimaye, utekelezaji wa wosia wa kitume utakaotolewa na Mama Kanisa baada ya maadhimisho ya Sinodi. Vijana wajengewe imani, matumaini na uhakika wa maisha yao; wasaidiwe kukabiliana na changamoto sanjari na kujengewa uwezo wa kuboresha maisha yao kwa njia ya sera na mikakati makini inayotekelezwa na Mama Kanisa, elimu bora itakayowawezesha kujikita katika ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu yanayozingatia utu, heshima, ustawi na mafao ya wengi!

Umaskini na ukosefu wa fursa za ajira ni kati ya changamoto kubwa kwa vijana wa kizazi kipya. Mambo yote haya yanapaswa kuvaliwa njuga na Mama Kanisa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali, ili kweli vijana wa kizazi kipya waweze kuwa ni wahusika wakuu katika maisha na utume wa Kanisa! Duniani kuna magonjwa, mateso na mahangaiko makubwa ya binadamu kutokana na sababu mbali mbali, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana wa kizazi kipya kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huruma, furaha, amani na upendo.

Vijana wahamasishwe kushirikisha kikamilifu karama na vipaji vyao vya ugunduzi na ubunifu; ujasiri, ari na moyo wao mkuu katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yaliyoko mbele yao! Barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa vijana kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana iwe ni dira na mwongozo kwa Maaskofu wakati huu wa maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana. Maaskofu wasaidie kuwahamasisha vijana katika medani mbali mbali za maisha, ili kushiriki kujibu maswali dodoso yatakayosaidia kuandaa Hati ya Kutendea Kazi yaani “Instrumentum laboris”.

Vijana wenyewe wanaweza pia kushiriki katika maandalizi haya kwa kujibu maswali yanayowekwa kwenye mtandao wa Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu. Hati ya kutendea kazi inatarajiwa kuonesha uaminifu mkubwa wa changamoto, matatizo na fursa zilizopo katika uwanja wa vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kuwa kweli ni sehemu ya mchakato wa maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Mwenyezi Mungu anawataka vijana kuwa kweli ni chemchemi ya furaha, amani, upendo na mshikamano katika jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.