2017-05-20 11:51:00

Maendeleo endelevu ni kitovu cha mabadiliko ya kweli katika maisha!


Agenda ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa kwa Mwaka 2030 ni tukio ambalo hivi karibuni, limeandaliwa na Askofu mkuu Ivan Jurkovic, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, Uswiss, kwa kushirikiana na Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyoko mjini Geneva pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo na Biashara, UNCTAD. Ni tukio ambalo limewashirikisha “vigogo” wa Mashirika mbali mbali ya Umoja wa  Mataifa yenye dhamana ya maendeleo ya binadamu!

Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu, ameshiriki kikamilifu katika tukio hili kwa kukazia kwamba, amefarijika kuona kuwa ustawi na maendeleo ya binadamu ni kati ya vipaumbele vinavyovaliwa njuga na Umoja wa Mataifa katika utekelezaji wa Agenda ya Manedeleo Endelevu Ifikapo Mwaka 2030. Anasikitika kusema, kwamba, kuna umati mkubwa sana wa watu wanaoishi katika umaskini wa hali na kipato ambao kimsingi ni matokeo ya utandawazi usiojali wengine ambao umezalisha makundi ya watu katika jamii! Yaani kuna watu ambao wanafurahia maisha kupita kiasi na kuna “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”, ambao utu na heshima yao kama binadamu vinawekwa rehani kutokana na sera na uchumi usiojali mahitaji msingi ya binadamu!

Ubinafsi, uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka ni mambo ambayo yamepelekea kuundwa kwa uchumi na biashara huria ambazo kimsingi hazifuati kanuni maadili na utu wema, kinachopewa kipaumbele cha kwanza ni rasilimali fedha na faida kubwa; tija na ukuaji mkubwa wa uchumi unaozingatia maendeleo ya vitu na wala si utu na heshima ya binadamu! Kardinali Turkson anaishukuru na kuipongeza Jumuiya ya Kimataifa ambayo imeamua kuwekeza zaidi katika mshikamano dhidi ya ubinafsi na tabia ya kutaka kuwatenga watu katika mchakato wa maendeleo endelevu! Huu ni mshikamano na maskini wa kizazi cha sasa na kile kijacho!

Vatican inayaangalia maendeleo endelevu ya binadamu kwa kuzingatia utu na heshima ya binadamu; ustawi na mafao ya wengi. Ni maendeleo yanayofumbata uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu; elimu na afya msingi inayokumbatia kwa namna ya pekee Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Haya ni maendeleo yanayopania kuleta maboresho katika maisha ya watu kwa kukazia tija na uzalishaji unaofanikishwa na rasilimali watu; umilikaji sawa wa ardhi; chakula na kwamba, maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu na asili ya uha iwa viumbe vyote duniani! Ni maendeleo yanayofumbata tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kwa kutambua kwamba familia ni wakala wa kwanza wa maendeleo endelevu ya binadamu, kielelezo cha umoja na mshikamano, kati ya watu wa mataifa na taasisi za kimataifa!

Viongozi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa wamekazia umuhimu wa Umoja wa Mataifa kuzisaidia nchi wanachama kuhakikisha kwamba, Malengo ya Maendeleo Endelevu kufikia Mwaka 2030 yanatekelezwa kikamilifu kwa kuibua na kutekeleza sera na mikakati makini ya maendeleo endelevu inayotekelezeka kikamilifu. Dr. Mukhisa Kituyi, Katibu mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo na Biashara, UNCTAD anasema, kuna haja pia ya kuishirikisha sekta binafsi ili kuchangia katika ustawi na maendeleo ya wengi. Viongozi wengine wanasema, dini na mashirika ya kidini sehemu mbali mbali za dunia yamekuwa na mchango mkubwa katika kukuza na kudumisha mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu, hasa vijini kwa kuwekeza katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii. Kumbe, kuna haja pia ya kupambana na magonjwa hatari kama vile UKIMWI, Malaria na Kifua Kikuu yanayokwamisha mchakato wa maendeleo endelevu kwa kupukutisha nguvu kazi inayohitajika katika kuzalisha na kutoa huduma.

Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji inapaswa kuangaliwa kama fursa ya maendeleo endelevu na wala si kikwazo kama ambavyo kinashughulikiwa kwa sasa na baadhi ya nchi duniani. Ukosefu wa fursa za ajira, elimu makini na huduma bora za afya hasa kwa vijana wa kizazi kipya ni vikwazo vikubwa vya maendeleo kwa vijana wengi duniani! Ndiyo maana, viongozi wengi wa Mashirika ya Kimataifa wanaunga mkono hoja ya Vatican kuhakikisha kwamba, sera na mikakati ya maendeleo endelevu inatoa kipaumbele cha kwanza kwa mahitaji msingi, ustawi na mafao ya wengi! Hapa kuna haja ya kujenga uchumi shirikishi!

Bwana Pasquale Lupoli afisa mwandamizi kutoka Shrika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa,”IOM” anasema, kuna watu milioni 250 ambao wanaishi duniani kama wakimbizi na wahamiaji na kuna zaidi ya watu milioni 40 ambao hawana makazi hata katika nchi zao wenyewe. Wakati huo huo mchango wa wakimbizi na wahamiaji katika Pato Ghafi la Taifa ”GNP” ni kiasi cha bilioni 585 kwa mwaka. Kwa mara ya kwanza wakimbizi na wahamiaji wameingizwa katika agenda za kimataifa kwa kutambua kwamba, hata wao wanachangia kwa kiasi kikubwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Changamoto kwa wakati huu ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaandaa sheria, taratibu na kanuni za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji; na kwamba, changamoto hii inapaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa na wala si kubakia kuwa ni mzigo kwa baadhi ya nchi duniani, ili kweli wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji liweze kuwa ni fursa makini na kichocheo cha maendeleo endelevu ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.