2017-05-18 16:06:00

Roho Mtakatifu awawezeshe kuwa mashuhuda wa Kristo Mfufuka!


Ndugu msikiliza wa Radio Vatican, Nabii Isaya anatualika katika wimbo wa mwanzo wa Dominika hii akituambia: “Hubirini kwa sauti ya kuimba, tangazeni haya yatamkeni mpaka mwisho wa dunia, semeni, Bwana amelikomboa taifa lake, aleluya”. Ukristo si nadharia bali ni uhalisia katika maisha. Mkristo daima anaalikwa kudhihirisha hadhi yake, kwamba amekombolewa kutoka utumwa wa dhambi na kufanyika kuwa mwana huru katika Kristo. Mkristo anapaswa kumshuhudia Kristo anayemwilika ndani mwake. Hayo ndiyo matendo au mahubiri ambayo mwanadamu katika maisha ya ufufuko anapaswa kuyadhihirisha.

Ushuhuda wetu hujifunua katika upendo wetu kwa Kristo na jirani zetu. Kristo anatuambia “mkinipenda, mtazishika amri zangu”. Hapa tunakiona kigezo cha ushuhuda huo wa Kristo ambacho ni kudumu katika amri zake. Pengine tunaweza kujiuliza ni zipi zilizo amri zake. Tunaweza kusingizia kwamba hatuwezi kuionesha sehemu fulani katika Maandiko inayozifafanua amri za Kristo. Lakini amri zake ni jumla ya Injili yake yote ambayo imetoa mwanga na kielelezo kwa mwanadamu ili kuufikia wokovu. Dominika iliyopita aliziweka amri zake zote katika fumbo la nafsi yake kwa kujitambulisha kwetu kama njia, ukweli na uzima (Rej Yoh 14:6).

Jumla ya maisha ya mwanadamu katika ukweli inajumuishwa katika utume wake ambao unatolewa kwa muhtasari katika kurasa za Injili Takatifu. Hivyo upendo wetu kwa Kristo unajifunua katika utii wetu kwa Injili Takatifu. Ni katika Injili Takatifu ambamo Kristo ametuwekea medani zote za maisha ya mwanadamu. Tunapata maelekezo sahihi ya namna yanavyopaswa kuwa mahusiano yetu na Mungu na pia mahusiano yetu na wanadamu wote. Injili Takatifu ni nyenzo ya msaada na kiunganishi chetu kwa Mungu. Uaminifu wetu katika Neno la Mungu humleta karibu nasi na hudadavua vema nafasi yake katika fumbo la mwanadamu. Mwanadamu anayejitenga mbali na Mungu kwa dhambi huwezeshwa kurudi karibu naye na kuungana naye.

Kumpenda Kristo hakutujii hivi hivi kwa uwezo wa kiakili tu bali ni tukio linalohitaji uwezo kutoka juu. Ndiyo maana Kristo anatuahidia msaidizi “Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui”. Hili ni dokezo muhimu la ushuhuda wa maisha ya kikristo na jawabu kwa upinzani wa amri za Kristo katika jamii mamboleo. Nafasi hii ya Roho Mtakatifu ni muhimu katika maisha yetu kwani inaendelea kuufanya uwepo wa Kristo kuwa ndani mwetu. Kristo anasema “Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu. Bado kitambo kidogo na ulimwengu haunioni tena; bali ninyi mnaniona. Na kwa sababu mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai”. Hivyo uwepo wake Roho wa Mungu ndani yetu unaifanya Injili ya Kristo kuwa hai ndani mwetu na hivyo kuwezeshwa kuutangaza wokovu wa Mungu kwa maisha yetu.

“Muwe tayari sikuzote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu”. Himizo hili ya kitume la Mtume Petro linatukumbusha namna stahiki ya ushuhuda wa maisha yetu ya kikristo. Hapa tunaaelekezwa kwamba utayari wetu wa kuidhirisha imani yetu ufanyike katika hali ya upole na kwa hofu. Tuitangaze Injili ya Kristo kwa upole, kwa mfano wa Kristo mwenyewe. Tuitangaze Injili ya Kristo si kwa kutafuta kuwadharau au kuwatukana wengine. Ushuhuda wetu unapaswa kuvikwa huruma na unyenyekevu wa kimungu. Tujaribu kuepa kwa namna yoyote mashindano na kutumia nguvu nyingi. Pengine tunashuhudia katika ulimwengu wa leo baadhi ya wanaotumia nguvu na hata kuwadhalilisha wengine katika kuitangaza imani iliyomo ndani mwao. Hii si njia ya kuitangaza imani yetu ya kikristo.

Mtume Petro anaendelea kukazia akisema: “Nanyi muwe na dhamiri njema, ili katika neno lile mnalosingiziwa, watahayarishwe wale wautukanao mwenendo wenu mwema katika Kristo”. Zipo nafasi mbalimbali katika maisha ambazo tunaweza kupitia mateso iwe ni kimwili, kiroho au kisaikolojia lakini namna njema ya kumdhihirisha Roho wa Mungu aliye ndani mwako si kwa mtindo wa «Dawa ya moto ni moto» au «ama zake ama zangu» au «Jino kwa jino». Maisha yetu si ya kujibu kwa kisasi au kwa kupambana bali mapambano yetu yapambwe na dhamiri safi katika Kristo. Kujibu kwa upole, upendo na msamaha kama Kristo mwenyewe anavyotufundisha akisema “mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili” (Mt 5:39).

Hofu tunayohimizwa si woga au kurudi nyuma bali ni hofu ya Mungu. Hofu ya Mungu hujumulishwa katika tendo la kustaajabia na kuutambua ukuu wake kwetu. Tunapopokea hali hiyo kwa kushirikishwa wana warithi wa Mungu katika Kristo na kwa njia ya Roho Mtakatifu hofu hiyo inapaswa kububujika katika matendo yetu ya upendo kwa wenzetu. Upendo huo hutusukuma kuheshimu na kumpatia kila mmoja hadhi yake anayostahili. Hofu hii inatusukuma kuitambua nafsi ya Mungu katika nafsi ya mwenzangu. Ushuhuda wa maisha ya kikristo unapaswa kukuza udugu kati yetu. Umoja katika jumuiya za kikristo ni udhihirisho wa kazi ya Roho Mtakatifu.

Somo la kwanza la Dominika hii limetuwekea mbele Jumuiya ya kwanza ya kikristo kama kielelezo cha maisha ya kikristo yanayoidhihirisha nguvu ya Roho Mtakatifu. Shemasi Filipo anadhihirisha uwepo huo wa kimungu ndani mwake kwa maana “pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule”. Kazi za Kristo zinadhihirika katika huduma ya upendo kwa wote. Mitume Petro na Yohane wanapowatembelea na kuwaimarisha waliobatizwa kwa sababu ya mahubiri na matendo ya Filipo walinuia wote wayadhihirishe matendo makuu ya Mungu na furaha yao iwe ni ya kudumu. Roho Mtakatifu hutenda kazi pamoja nasi. Ni wajibu wetu kuwa mashuhuda wa uwepo huu wa kimungu ndani mwetu. Tumtangaze Kristo kwa matendo yetu mema ya kila siku ambayo yanauimarisha uhusiano wetu na Mungu na wanadamu wote. Imani yetu ishuhudiwe katika matendo yetu tunayoyatenda katika upole na hofu kuu.

Kutoka studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.