2017-05-17 13:11:00

Papa Francisko: Endeleeni kuombea amani na maridhiano kati ya watu!


Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume “Misericordiae vultus” yaani “Uso wa huruma” anasema maisha ni hija na binadamu ni hujaji anayetamani kwenda mbinguni. Hija kimsingi inafumbata toba na wongofu wa ndani; inakazia umuhimu wa kushikamana na kuiambata huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu; ni changamoto ya kutoa na kupokea msamaha! Kuanzia tarehe 19 hadi 21 Mei 2017 kunafanyika hija ya wahudumu wa maisha ya kiroho kwa wanajeshi Wakatoliki Kimataifa huko Lourdes, Ufaransa inayoongozwa na kauli mbiu “Utujalie amani”. Zaidi ya wanajeshi 12, 000 kutoka katika mataifa 40 wanashiriki katika hija ya 59 ya maisha ya kiroho, ili kuomba msaada na tunza kutoka kwa Bikira Maria wa Lourdes.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, anawashukuru na kuwapongeza wale wote wanaoendelea kujisadaka na kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutafuta, kujenga na kudumisha amani duniani! Katika kipindi hiki cha mashaka na wasi wasi mkubwa kuhusu vita na kinzani za kijamii, kuna haja ya kukumbuka kwamba, amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha mwanadamu!

Kumbe, mwanadamu kamwe asichoke kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kumkirimia amani duniani. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, daima anajibu sala hii kutoka kwa watoto wake kwa kuamsha ndani ya watu wenye mapenzi mema mashuhuda na wajenzi wa amani; udugu na mshikamano wa dhati! Baba Mtakatifu anawaalika wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama kumwangalia Kristo Yesu, ili hatimaye, waweze kushinda kishawishi cha chuki na kutaka kulipizana kisasi ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda amini wa ukweli! Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutumia nafasi hii kuonesha uwepo wake wa karibu kwa wale wote wanaoendelea kuteseka kutokana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii sehemu mbali mbali za dunia! Wote hawa anawaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Lourdes.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.