2017-05-17 13:49:00

Madhabahu ni mahali pa uinjilishaji wa kina, toba na wongofu wa ndani


Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya kuanzia sasa limepewa dhamana na madaraka ya kusimamia Madhabahu ya Kimataifa kadiri ya sheria za Kanisa; Kuhakikisha kwamba, maeneo haya muhimu katika maisha na utume wa Kanisa yanakuwa ni mahali muafaka pa uinjilishaji mpya: unaojikita katika ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo. Baraza lina wajibu wa kusaidia madhabahu ya Kanisa kuwa ni mahali pa mikutano ya kitaifa na kimataifa, ili kukuza na kudumisha ibada na hija kwenye maeneo matakatifu.

Baraza lina dhamana ya kuwafunda wahudumu kwenye madhabahu haya ili yaweze kutoa huduma msingi za kichungaji, kikanisa na maisha ya kiroho pamoja na kuendeleza sanaa na utamaduni wa maeneo haya kama mifumo maalum ya uinjilishaji. Kimsingi hii ndiyo changamoto kubwa iliyotolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake binafsi ijulikanayo kama “Sanctuarium ecclesia” yaani “Madhabahu ndani ya Kanisa”.

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, hija ya 19 ya Baba Mtakatifu Francisko kimataifa huko kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima, kuanzia tarehe 12 hadi 13 Mei 2017, ambayo imeongozwa na kauli mbiu “Papa Francisko mjini Fatima 2017 pamoja na Bikira Maria kama mahujaji wa matumaini na amani”, imekuwa ni hija ya matumaini na amani kwa familia ya Mungu duniani. Imeendelea kupandikiza mbegu ya uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani tendaji changamoto na mwaliko wa kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi!

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, alikuwa ni kati ya “vigogo” wa Kanisa waliokuwa kwenye msafara wa Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima yaani: Francis Marto, Yacinta Marto na Mtumishi wa Mungu Lucia dos Santos. Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima ni mahali mahususi kabisa pa uinjilishaji mpya; kwani hapa waamini na watu wenye mapenzi mema; kwa imani na matumaini wanakimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili aweze kuwafunika kwa joho la upendo na huruma yake ya kimama kama alivyokaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake nchini Ureno hivi karibuni!

Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima ni kituo cha sala na Ibada kwa Moyo Safi wa Bikira Maria usiokuwa na doa; mahali muafaka pa kutafakari muhtasari wa kazi ya ukombozi; huruma na upendo wa Mungu kama vilivyofunuliwa na Kristo Yesu! Licha ya umati mkubwa wa watu uliokuwa umefurika katika mkesha wa Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima, lakini, mtu aliweza kusali na kuhisi kimya kikuu wakati wa Kuabudu Ekaristi Takatifu, matendo makuu ya Mungu! Hapa watu wanakwenda kusali, kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo na Mungu kwa waja wake.

Baba Mtakatifu katika hija yake, amekazia mwelekeo wa kimissionari katika hija zinazofanywa na waamini kama sehemu ya toba na wongofu wa ndani! Baba Mtakatifu anawahimiza waamini kwanza kabisa kutoka katika ubinafsi wao, tayari kusikiliza na kujibu kilio cha maskini  na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Pili ni kwa Kanisa kutoka kifua mbele kwenda pembezoni mwa maisha ya mwanadamu, ili kushuhudia na kuambata mambo msingi katika maisha ya mwanadamu.

Hii ni sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kutoka kwa familia ya Mungu! Watu wanataka kuona matendo kama kielelezo cha imani tendaji! Sala, toba na wongofu wa ndani pamoja na tafakari ya kina ya Neno la Mungu ni nyenzo muhimu sana katika uinjilishaji mpya, ili kuwaweze waamini kugundua na kuonja uwepo endelevu wa Mungu katika historia, maisha na matukio mbali mbali wanayokumbana nayo katika safari ya maisha ya hapa duniani. Kwa njia hii, waamini watakuwa na ujasiri wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu na jirani zao, tayari kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wanaohitaji msaada zaidi!

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella anakaza kusema, Madhabahu ya Fatima ni mahali pa sala na ibada kwa watu wa kawaida; watu wasiokuwa na makuu: Hapa ni mahali pa katekesi ya kina kuhusu: Imani, Sakramenti za Kanisa, Amri za Mungu na Maisha ya Sala! Haya ni mambo makuu yanayoweza pia kuendelezwa kwenye madhabahu yaliyotanwanyika sehemu mbali mbali za dunia. Madhabahu ya Bikira Maria, licha ya ukanimungu na utepetevu wa imani katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, lakini bado kuna bahari ya waamini wanaoshuhudia imani yao kwa Bikira Maria. Madhabahu yanawasaidia waamini kupata utambulisho wao, kama watoto wa Bikira Maria; ni mahali ambapo waamini wanapata nafasi tena ya kujitambua na kujikita katika safari ya imani na maendeleo endelevu ya binadamu; kwani imani inakuwa ni kielelezo na utambulisho wa mwamini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.