2017-05-17 14:17:00

Bado kuna vitendo vinavyotishia amani, utu na heshima ya binadamu!


Maadhimisho ya kilele cha Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima, tarehe 13 Mei 2017 kwa uwapo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko yamekazia umuhimu wa familia ya Mungu kujenga na kudumisha Injili ya matumaini na amani duniani! Il kweli dunia iweze kupata amani ya kudumu kuna haja ya kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa kujikita katika udugu na mshikamano. Amani ya kweli inabubujika kutoka katika Moyo Safi wa Bikira Maria usiokuwa na doa na kwamba, hii ni changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini na amani kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko!

Huu ni ujumbe uliotolewa na Askofu mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa alipokuwa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima, katika Ibada iliyoadhimishwa kwenye Makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani. Bado kuna haja ya kuendelea kuombea amani duniani kutokana na ukweli kwamba, bado kuna damu ya watu wasiokuwa na hatia inaendelea kumwagika kutokana na vita huko Siria, Sudan ya Kusini, Somalia, Yemen, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati na DRC. Bado kuna watu wanateseka kutokana na vita inayoendelea huko Ucrain; kuna wasi wasi wa kufumuka kwa mashambulizi ya kijeshi huko Korea ya Kaskazini inayoendelea kuvunja mikataba ya Jumuiya ya Kimataifa, kiasi hata cha kuanza kuwajengea watu hofu.

Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, bado wanahamasishwa na Bikira Maria kusali kwa ajili ya kusitisha na hatimaye, kukomeshwa kabisa kwa vitendo vya: ukabila, udini, dhuluma, unyanyasaji wa kidini pamoja na mashambulizi ya kigaidi yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu; haki msingi za kuabudu na uhuru wa kidini. Sala ipanie kukomesha biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; utumwa mamboleo na mamifumo yake yote; biashara haramu ya dawa za kulevya pamoja na biashara ya silaha duniani inayoendelea kupandikiza mbegu ya utamaduni wa kifo, chuki na uhasama kati ya watu.

Askofu mkuu Bernardito Auza anakaza kusema, Bikira Maria ni Balozi na chombo cha amani. Baba Mtakatifu Francisko anaonya kwamba, kuna Vita Kuu ya Tatu inayoendelea duniani; ni vita inayopigwana sehemu mbali mbali za dunia. Wakristo wengi wana ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Tukio la Bikira Maria kuwatokea baadhi ya watu ndani ya jamii ni jambo binafsi na wala halina uzito wa pekee katika imani ya Kanisa Katoliki. Hata pake Kanisa linapokiri kuhusu matukio kama haya kama ilivyotokea kwa Mtakatifu Francis Marto, Yacinta Marto na Mtumishi wa Mungu Lucia dos Santos, hakuna mwamini anayelazimishwa kuamini. Kanisa linaamini kufundisha yale yaliyofunuliwa katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa.

Ushuhuda wa Watoto wa Fatima kuhusu kutokewa na Bikira Maria, umepokelewa na Kanisa kwa imani na busara kubwa ya kichungaji na kwamba, ni tukio ambalo limesaidia mchakato wa toba na wongofu wa ndani; Ibada kwa Bikira Maria na kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, chemchemi ya neema, baraka na huruma ya Mungu kwa waja wake. Ni matukio ambayp yamewasaidia waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kumfahamu zaidi Kristo Yesu kwa njia ya shule ya Bikira Maria. Ni matukio ambayo yamelisaidia Kanisa kusoma alama za nyakati na kutoa majibu muafaka kwa changamoto zilizokuwa zinamkabili binadamu!

Askofu mkuu Bernardito Auza anaendelea kufafanua kwamba, toba na wongofu wa ndani; unaoheshimu na kuthamini utu wa binadamu, haki zake msingi, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha amani duniani. Haya ni mambo yanayofumbwa kwa namna ya pekee kabisa katika amani, udugu na mshikamano unaoongozwa na kanuni auni! Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kutubu na kumwongokea Mungu kwa kuachana na tabia ya ujenzi wa sera na mikakati ya uchumi inayomdhalilisha binadamu na haki zake msingi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa rasilimali fedha na faida kubwa! Matokeo yake ni binadamu kuendelea kuogelea katika majanga sanjari na kuwabeza maskini, wakimbizi na wahamiaji wanaohitaji kuonjeshwa Injili ya huruma na mshikamano. Wongofu wa ndani ni msingi thabiti wa amani duniani!

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anaendelea kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kukimbilia hifadhi na tunza kutoka kwa Bikira Maria, Mwenye Moyo Safi usiokuwa na doa, chemchemi ya huruma na mapendo; amani na utulivu unaoshinda nguvu ya silaha; ni moyo wenye uwezo wa kuleta mabadiliko katika historia ya maisha ya mwanadamu! Ikumbukwe kwamba, amani ya kweli inabubujika kutoka katika moyo wa mwanadamu! Kumbe, watu wenye nia njema wanaweza kuwa kweli ni wajenzi wa Injili ya matumaini na amani duniani! Sala itaendelea kuwa ni nyenzo muhimu sana katika kukuza na kudumisha Injili ya amani duniani na kwamba, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini na amani duniani, kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.