2017-05-15 09:56:00

Askofu mkuu Jude Thaddeus Okolo ateuliwa kuwa Balozi wa Ireland


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Jude Thaddeus Okolo kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Ireland. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Okolo alikuwa ni Balozi wa Vatican kwenye Jamhuri ya Watu wa Dominican na Mwakilishi wa Kitume huko Puerto Rico. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Okolo alizaliwa tarehe 18 Desemba 1956 huko Kano, Nigeria. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 2 Julai 1983 akepwa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya huduma kwa familia ya Mungu Jimboni Nnewi. Baadaye alitumwa na Jimbo lake kujiendeleza kwa masomo ya juu na kubahatika kujipatia Shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kanisa. 

Alianza utume wa kidiplomasia mjini Vatican kunako mwaka 1990 na tangu wakati huo ametumwa sehemu mbali mbali za dunia kwanza kabisa kama afisa wa Ubalozi na hatimaye, Balozi kamili huko nchini: Haiti Visiwa vya Antillean, Uswiss, Jamhuri ya Watu wa Czech na Australia. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2008 akamteuwa Askofu mkuu kuwa Balozi wa Vatican Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati na Chad. Kunako mwaka 2013 akateuliwa na Papa Francisko kuwa Balozi wa Vatican kwenye Jamhuri ya Watu wa Dominican na Mwakilishi wa Kitume huko Puerto Rico.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.