2017-05-13 14:48:00

Papa Francisko awaambia wagonjwa: Yesu ametangulia mbele ya Msalaba


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama kilele cha Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima, Jumamosi, tarehe 13 Mei 2017 ameongoza pia Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na hatimaye, kutoa salam kwa wagonjwa kwa kuwakumbusha kwamba, Kristo Yesu, daima anawatangulia mbele ya Msalaba na amebeba katika mwili wake mateso na mahangaiko ya binadamu.

Yesu anafahamu fika maana ya mateso, anafariji na kuwapatia waja wake nguvu kama alivyofanya kwa Mtakatifu Francisko Marto na Mtakatifu Yacinta Marto, watakatifu wa mahali na nyakati zote. Anamkumbuka Mtume Petro aliyekuwa amefungwa gerezani kule Yerusalemu, Kanisa likaungana naye kwa njia ya sala na hatimaye, Mwenyezi Mungu akamfariji Mtakatifu Petro. Hili ndilo fumbo la maisha ya Kanisa, linalomwomba Mwenyezi Mungu awafariji wanaoteseka kama wagonjwa walioko mbele yake; anawafariji hata katika hali ya kificho, katika undani wa moyo kwa kuwajalia nguvu!

Baba Mtakatifu anawakumbusha mahujaji na waamini kwamba, mbele yao katika Fumbo la Ekaristi Takatifu yumo Yesu aliyejificha katika maumbo ya Mkate, lakini yuko katika madonda ya ndugu zao wagonjwa na wale wanaoteseka. Altareni wanamwabudu Yesu Kristo na katika ndugu zao wanakumbana na Madonda Matakatifu ya Yesu. Mkristo anamwabudu na kumtafuta Yesu na kwamba, anatambua Madonda Matakatifu ya Yesu. Ikiwa kama wanataka kujitoa na kujisadaka kwa ajili ya Mungu hawana budi kujitahidi kumfahamu na kumuiga katika maisha kama walivyofanya Watoto wa Fatima, wakashiriki furaha na mateso kama sadaka safi mbele ya Mungu.

Baba Mtakatifu anawaalika wagonjwa kuishi mateso yao kama zawadi  na kumshikirisha Bikira Maria kama walivyofanya Watoto wa Fatima kwa kuyatolea mbele ya Mwenyezi Mungu kwa moyo wote! Wagonjwa wasikubali kamwe kuwa ni watu wa kupokea msaada kama kielelezo cha mshikamano, bali wawe ni washiriki wakamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya ukimya wao unaozungumza; sala na majitoleo ya kila siku, daima wakiunganisha mateso yao na yale ya Kristo Yesu kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu. Wakubali kupokea mateso katika hali ya furaha kama rasilimali ya maisha ya kiroho, amana kwa maisha ya Jumuiya ya Kikristo na kwamba, kamwe wasione aibu kuwa ni amana ya Kanisa. Yesu wa Ekaristi Takatifu amepita karibu ya wagonjwa, ili kuonesha uwepo wake wa karibu pamoja na upendo wake. Baba Mtakatifu anawaalika wagonjwa kuyaaminisha magonjwa, mahangaiko na mchoko wao kwa Kristo Yesu. Watambue kwamba, Kanisa linawasindikiza kwa sala zinazotolewa sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, Mwenyezi Mungu ni Baba na kamwe hawezi kuwasahau hata kidogo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.