2017-05-12 14:41:00

Papa Francisko: Msiogope ukweli wala kunaswa na mawazo binafsi!


Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuondoka kuelekea Fatima nchini Ureno, Ijumaa, tarehe 12 Mei 2017, amekutana na kuzungumza na wajumbe waliokuwa wanashiriki katika mkutano wa mambo ya nyota ulioandaliwa na Kituo cha Unajimu cha Vatican, huko Castel Gandolfo. Wajumbe hawa wamekuwa wakichambua masuala ya kisayansi yanayoligusa Kanisa kwa namna ya pekee! Ni masuala yanayohusu mwanzo wa dunia na mabadiliko yake; undani wa anga na nyakati.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, haya ni mambo yenye maana ya pekee katika sayansi, falsafa, taalimungu na maisha ya kiroho. Hapa ni mahali ambapo taaluma mbali mbali zinaweza kukutana na kujadiliana, lakini pia ni uwanja ambao uko wazi kwa taaluma hizi kutofautiana na hatimaye, kusigana kabisa! Baba Mtakatifu amechukua fursa hii kumpongeza Monsingo Georges Lematre, Padre Mkatoliki na Mtaalamu wa mambo ya ulimwengu, aliyekuwa na kipaji cha ubunifu katika masuala ya imani na sayansi; akasimama kidete kulinda na kutetea tofauti ya mifumo kati ya sayansi na taalimungu; taaluma mbili zenye dhamana zinazotofatiana kabisa kama ambavyo alikwishawahi kusema Mtakatifu Thoma wa Akwino kwamba, mwelekeo finyu katika masuala haya ni hatari kwa sayansi pamoja na imani.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mzaburi anawakumbusha walimwengu kwamba, mtu ni kitu gani hata umkumbuke, na binadamu hata umwangalie? Albert Einstein alipenda kusema kwamba, pengine mtu anaweza kusema kuwa “Fumbo la Dunia haliwezi kufahamika”. Lakini, ikumbukwe kwamba, uwapo na uwezo wa akili ya binadamu si matokeo ya kinzani au bahati nasibu, bali ni hekima ya Mungu iliyokuwako tangu mwanzo wa njia yake kabla ya matendo yake ya kale. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwapongeza kwa kazi nzuri sanjari na kuwatia shime kuendelea na tafiti kuhusu ukweli, bila kuuogopa ukweli wenyewe au kunaswa nao kutokana na mawazo yao binafsi. Baba Mtakatifu anawaalika kupokea kwa shukrani na unyenyekevu, ugunduzi mpya, hasa wakati huu, binadamu anapoendelea kutembea katika maarifa, inawezekana kuwa na mang’amuzi ya kweli ya uwepo wa Mungu anayeweza kuzima kiu ya mioyo yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.