2017-05-12 17:48:00

Baba Mtakatifu Francisko hujaji wa matumaini na amani amewasili Ureno


Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuanza hija yake ya kitume nchini Ureno kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima, Alhamis, tarehe 11 Mei 2017 alikwenda moja kwa moja kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu mjini Vatican na kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, afya ya Warumi. Ijumaa mchana, amepata nafasi pia ya kusalimiana na wanawake sita wenye shida na mahangiko katika maisha yao, huku wakiwa wameandamana na watoto wao wachanga! Alipofika uwanja wa Ndege wa Fumicino, ameagana na viongozi wa Kanisa na Serikali ya Italia.

Akiwa angani, Baba Mtakatifu ametuma salam na matashi mema kwa Marais wa Italia, Ufaransa na Hispania. Amemwambia Rais Sergio Mattarella kwamba anakwenda nchini Ureno kuadhimisha Jubilei ya miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima. Anakwenda kukutana na umati mkubwa wa wagonjwa kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaokimbmilia ulinzi, tunza na mwanga wa matumaini kutoka kwa Bikira Maria wa Fatima anapenda kuwakumbuka na kuwaombea wagonjwa wote wa kiroho na kimwili walioko nchini Italia. Akiwa kwenye anga la Ufaransa, Baba Mtakatifu amemwandikia ujumbe wa matashi mema Rais Francois Hollande pamoja na kuwapatia wananchi wote wa Ufaransa, baraka zake za kitume! Alipotinga kwenye anga za Hispania, amemtumia pia salam na matashi mema Mfalme Felipe VI kwa kuwaombea wananchi wake amani na nguvu.

Baba Mtakatifu alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Monte Real amepokelewa na viongozi wa Serikali na Kanisa. Nyimbo za Mataifa haya mawili, zimepigwa kwa ustadi mkubwa na baadaye, viongozi wakatambulishana. Baba Mtakatifu amepata fursa ya kukutana na kuzungumza kwa faragha na Rais Marcelo Nuno Duarte Rebelo de Sousa. Amekwenda na kusali kidogo kwenye Kikanisa cha Uwanja wa Ndege wa Kijeshi kama wanavyofanya mahujaji wote wanaokwenda kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima. Baadaye Baba Mtakatifu Francisko na mgeni wake wakabadilishana zawadi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.