2017-05-11 14:30:00

Shikamaneni na maskini kupambana na rushwa na ufisadi wa mali ya umma


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, CELAM linalowaunganisha Maaskofu kutoka katika nchi 22 wanakutana mjini San Salvador katika mkutano wao wa mwaka unaoongozwa na kauli mbiu “Kanisa maskini kwa ajili ya maskini”. Mkutano huu pia ni sehemu ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 300 tangu Sanamu ya Bikira Maria wa Aparecida ilipopatikana huko Brazil. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa wajumbe wa CELAM anapenda kukuza mambo makuu matatu katika maadhimisho haya yaani: kukua na kukomaa kwa imani, kuendelea kujizatiti katika utume kwa familia ya Mungu huko Amerika ya Kusini pamoja na kuendelea kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini!

Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu kuangalia hali ya wavuvi na wananchi wa kawaida ambao walibahatika kuokota Sanamu ya Bikira Maria wa Aparecida. Ni watu ambao hawana uhakika wa usalama na maisha yao; wanataabika kujipatia mahitaji yao msingi kwa kujishughulisha na uvuvi. Hii ndiyo changamoto na ugumu wa maisha unaowakabili wananchi wengi huko Amerika ya Kusini. Lakini, jambo la kusikitika ni kuona rushwa na ufisadi wa mali ya umma vikiendelea kushamiri kiasi hata cha kuwatumbukiza wananchi wengi katika lindi la umaskini wa hali na kipato. Rushwa imekuwa ni saratani inayopukutisha maisha ya watu wengi Amerika ya Kusini, changamoto kwa wananchi ni kusimama kidete kupambana na rushwa na ufisadi wa mali ya umma!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Bikira Maria ni Mama mpole na mnyenyekevu anayesikiliza kwa makini kilio cha watoto wake na kuwasindikiza hatua kwa hatua katika maisha. Daima yuko karibu pamoja nao katika mchakato wa kukabiliana na changamoto za maisha. Bikira Maria alipokutana na wale wavuvi hawakupata samaki wengi, bali walishuhudia uwepo mwanana wa Bikira Maria katika mapambano ya maboresho ya hali yao ya maisha! Huu ni uwepo wa matumaini wa Bikira Maria, unaowatia shime kusonga mbele kwa imani na matumaini pasi na kukata wala kujikatia tamaa.

Huu ni mwaliko anasema Baba Mtakatifu Francisko kwa Kanisa kujikita katika mambo msingi; kwa kujizatiti katika imani ya Kanisa la mwanzo, iliyoifanya Amerika ya Kusini ikawa ni chemchemi ya matumaini. Bikira Maria wa Aparecida anawahamasisha waamini kupyaisha matumaini ya maisha yao, ili kupambana na mambo yanayowakatisha watu tamaa. Umefika wakati wa kujifunza imani inayomwilishwa katika maisha ya watu wa kawaida, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, wanasaidiwa kukuza na kuidumisha imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, ili liweze kuzaa matunda yanayokusudiwa yaani kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini, upendo na mshikamano wa dhati na watu wa kawaida!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.