2017-05-10 14:56:00

Papa Francisko anataka kumkabidhi B. Maria mahangaiko ya watu wake!


Baba Mtakatifu Francisko ana ibada ya pekee kabisa kwa Bikira Maria kwani kila mara kabla na baada ya hija zake za kitume, humwendea Mama wa Mungu kumshukuru kwa ulinzi na tunza yake! Kunako tarehe 13 Oktoba 2013 katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Baba Mtakatifu Francisko alijikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Fatima, baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Alitumia nafasi hii kumshukuru Bikira Maria kwa uwepo na tunza yake ya kimama na kwamba, alipenda kuunganisha sauti yake na sauti ya vizazi vyote wanaomwita Mwenyeheri.

Baba Mtakatifu anasema, katika maisha ya Bikira Maria, Kanisa linaadhimisha Mafumbo makuu ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Mwenyezi Mungu kamwe hachoki kumwinamia mwanadamu aliyejeruhiwa kwa dhambi, ili aweze kumganga na kumwokoa kwa njia ya huruma na upendo wake. Baba Mtakatifu alipenda kujikabidhi kwa Bikira Maria wa Fatima, kwa kuonesha imani yake kwake kwani anatambua kwamba, kila mwamini ana upendeleo wa pekee machoni pake na kwamba, hakuna jambo lolote linaloweza kufichika moyoni mwao pasi ya kueleweka mbele ya Bikira Maria.

Baba Mtakatifu alimwomba Bikira Maria wa Fatima kuwaangalia waja wake kwa jicho la upole na kuwaonesha tabasamu la kukata na shoka! Alimwomba, ili aendelee kuhifadhi maisha ya watoto wake, asaidie kuombea nia njema, aimarishe imani, matumaini na mapendo na hatimaye, aweze kuwaongoza katika njia ya utakatifu wa maisha. Bikira Maria wa Fatima awafunde waamini kutoa upendeleo wa pekee kwa maskini, wagonjwa, wanaotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii; awakumbuke na kuwaombea wadhambi na wale waliopondeka na kuvunjika moyo; awakusanye watu wote chini ya Mwanaye mpendwa Yesu Kristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.