2017-05-08 08:01:00

Rais Magufuli ni jembe la nguvu, nchi iko mikononi mwa mtu makini!


Napenda kuchukua nafasi hii  kumshukuru sana Mhe. George Kahema Madafa, Balozi mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Italia pamoja, watumishi Ubalozini na Jumuiya ya Watanzania kwa   ukarimu wenu na mapokezi mazuri mliyonipatia mimi binafsi na wajumbe niliombatana nao kutoka Wizara mbalimbali na sekta binafsi. Na kabla sijaendelea, napenda kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Balozi Madafa kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kulitumikia Taifa letu hapa Italia. Ni heshima kubwa sana; na napenda kuwahakikishia Diaspora wote mliopo hapa Italia na maeneo ya Uwakilishi kuwa mmepata Balozi mchapakazi, mwadilifu ambaye pia atakuwa mlezi mzuri wa Jumuiya zenu za Diaspora popote zilipo ndani na nje ya Italia.

LENGO LA ZIARA

Mhe. Balozi, Watanzania wenzangu,

Lengo la ziara hii ya kikazi ni kukuza mahusiano mazuri ya kisiasa na kiuchumi kati ya Tanzania na Italia; ambapo imeniwezesha kukutana na viongozi wa Serikali ya Italia kuzungumzia masuala ya ushirikiano katika sekta mbalimbali.. Aidha, ziara hii pia inatoa nafasi kwangu kuiwakilisha Tanzania katika Kongamano la Kibiashara lililolenga kukuza fursa za uwekezaji baina ya nchi hizi mbili na kupanua soko la kibiashara. Kutokana na fursa hiyo ya kipekee ya ushiriki huo, nimeona ni muda muafaka pia niweze kukutana nanyi; nawashukuru sana kwa kuweza kujiandaa na kujumuika pamoja. Ni mategemeo yangu kuwa mtazidi kuungana na kujijenga vizuri katika jamii zenu; ili kupanga mikakati thabiti ya kutatua matatizo na changamoto zozote za maisha mnazokabiliana nazo. Niwahakikishie kuwa Serikali itaendelea kuwahamasisha na kuwashirikisha kikamilifu ili muweze kuchangia kile mlichokichuma katika kuleta maendeleo chanya nchini Tanzania.  Ni vizuri mtambue kuwa elimu, uzoefu, au maarifa yoyote mliyobobea ni chachu ya maendeleo nyumbani. Kwani Mcheza Kwao Hutunzwa”.

3. Hali ya kisiasa na kiuchumi nchini Tanzania

Kisiasa: Hali ya nchi yetu kisiasa ni nzuri.  Uhusiano na nchi zinazotuzunguka/majirani zetu ni mzuri. Mipaka iko salama. Labda mtakuwa mmesikia matukio siku za karibuni ya mauaji ya askari na kupotea kwa silaha; matukio haya yasiwatie shaka, ni vitendo vya kijambazi na serikali yetu iko makini kufuatilia na kuchukua hatua stahiki kwa watakaopatikana na hatia.

Hali kiuchumi: Uchumi wa Tanzania umeendelea kukua kwa aslilimia 7.2. Hii inatokana na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi madhubuti wa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Kuongeza mapato na kupiga vita Rushwa: Jitihada kubwa za serikali ni pamoja na juhudi mbalimbali za makusudi za kukusanya mapato ya kodi ya ndani kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA); kuziba mianya ya rushwa, ubadhirifu, wizi na upotevu wa fedha za umma. Aidha, jitihada hizo zinajumuisha pia udhibiti wa matumizi mabaya ya rasilimali za umma; uboreshwaji wa miundombinu na usafiri wa anga ili kupanua wigo wa vivutio vipya vya utalii; kukuza uzalishaji wa mazao ya chakula; kuimarisha ukaguzi wa shughuli za uzalishaji na biashara ya madini; uzalishwaji wa umeme katika maeneo muhimu ya maendeleo. Juhudi nyingine za serikali ni kufichua watumishi hewa maofisini; wanafunzi hewa mashuleni; wanaotumia vyeti vya kugushi; kupiga vita biashara na utumiaji wa madawa ya kulevya na uzembe sehemu za kazi. Aidha zoezi la kuwafichua watumishi na wanafunzi hewa limeiwezesha  serikali kuokoa maelfu ya pesa za walipa kodi.

Kuboresha Elimu:

Mojawapo ya malengo ya serikali ya awamu ya Tano ni kuboresha Elimu na kutoa elimu bure kwa Watoto kuanzia shule za Msingi hadi Sekondari. Hili linaenda sambamba pamoja na kuhakikisha mazingira mazuri ya watoto mashuleni, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kila mwanafunzi anakaa kwenye dawati.

Mafanikio mbalimbali:

Ununuzi wa ndege: Ukiacha maeneo ya ujumla niliyotaja, ningependa kuzungumzia pia maeneo ya kujivunia ambayo yamefanyika tangu Rais Magufuli kuingia madarakani. Serikali tayari imenunua ndege 2 aina ya Bombardier na zimeanza kazi ndani ya nchi. Aidha, serikali imenunua ndege nyingine 03 ikiwemo ndege kubwa yenye uwezo wa kufanya safari za masafa marefu nje ya nchi. Ujenzi wa barabara ya juu (Fly-overs) Ujenzi wa miundombinu nchini unaendelea kuimarika. Serikali iko mbioni kujenga barabara za juu kwenye makutano ya barabara eneo la Ubungo na Tazara. Kazi ya ujenzi wa fly-overs imeanza. Tunaamini kukamilika kwa barabara hizi kutapunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam na kuboresha shughuli za kiuchumi.

Ujenzi wa Reli ya Kati (Standard gauge): Awamu ya Kwanza ya Ujenzi - Dar es Salam hadi Morogoro

Mwezi Aprili 2017 Rais Magufuli aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa kipande cha Reli kuanzia Dar Es Salaam hadi Morogoro Pesa za ujenzi wa reli ambayo ni ya mwendo kasi (160Km kwa saa) kiasi cha Tshs 3.2 Trillioni zimetolewa na serikali, bila msaada wowote kutoka nje. Aidha, Kampuni kutoka Uturuki ikishirikiana na wataalam wetu itajenga kipande hicho cha reli ambayo inategemewa kukamilika ndani ya miezi 30.  Awamu zitakazofuata za ujenzi ni kutoka Morogoro hadi Makutoporo (Dodoma) (Km 336), Makutopora hadi Tabora (Km 294), Tabora hadi Isaka (Km 180) na Isaka hadi Mwanza (km 249). Kukamilika kwa ujenzi wa reli kutaboresha usafiri wa ndani, kuunganisha nchi yetu na nchi jirani, ajira kwa Watanzania na kuchochea ukuaji wa uchumi. Serikali itahitaji msaada katika kukamilisha ujenzi wa reli hiyo.

Mheshimiwa Balozi, Mabibi na Mabwana,

Katika kipindi hiki cha mwaka 2016/2017 Serikali inaendelea kukusanya mapato ya kodi kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambapo hadi sasa yameongezeka kwa shilingi trilioni 1.2 kwa mwezi; kutoka wastani wa shilingi bilioni 850 kwa mwezi kwa mwaka 2015/2016. Ni azma ya Serikali ya Awamu ya Tano kuwa na uchumi wa viwanda kwa kuchochea ukuaji wa Sekta za kipaumbele kama vile Kilimo, miundombinu, nishati na madini; ambapo utaifikisha Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025; ili kuondokana na umaskini. Tujumuike pamoja kuisaidia serikali yetu katika juhudi zake za kukuza uchumi na kuinua hali za maisha ya Watanzania.

4. KUHAMIA DODOMA

Kama mtakumbuka mwaka jana Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitangaza uamuzi wa Serikali kutekeleza azma yetu ya kuhamia Dodoma. Napenda kuchukua nafasi hii kuwafahamisha kuwa zoezi hilo kwa upande wa Serikali limeanza na linaendelea vizuri. Asilimia kubwa ya watumishi wa serikali kutoka Wizara mbalimbali walishahamia Makao Makuu Dodoma. Tunategemea ifikapo mwaka 2019 watumishi wote wa serikali watakuwa wamehamia Dodoma. Kwa upande wetu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki zoezi hili limetekelezwa kikamilifu; na tayari Uongozi wote wa juu wa Wizara umehamia Dodoma tangu Februari 2017, ikiwa ni pamoja na baadhi ya Maafisa kutoka idara mbalimbali Wizarani.

Fursa za kuwekeza Dodoma

Dodoma ni mji unaokuwa kwa kasi sana na fursa za kuwekeza ni nyingi. Serikali inakaribisha wadau kuwekeza katika ujenzi wa mji na miundombinu ya kisasa (barabara, uwanja wa ndege, reli, mawasiliano); ujenzi wa mashule, mahospitali, mahoteli ya kitalii, nyumba za kuishi watumishi, 'supermarkets' na ofisi kwa huduma mbalimbali.  Serikali itashirikiana na wadau kutoka sekta binafsi ili kuhakikisha huduma zote muhimu zinapatikana. Napenda kuwahimiza Diaspora kuzitambua fursa hizi na kuchukua hatua za haraka kujipatia ardhi Dodoma kwa ajili ya kuwekeza.  Kwa sasa gharama za ardhi ziko chini, nina hakika gharama hizi zitazidi kupanda.

Mauzo ya Shares za Vodacom

Bila shaka mmepata taarifa kuhusu fursa za kununua "shares" za Vodacom ambazo zilitangazwa mwezi Aprili 2017. Mauzo ya shares hizo bado yanaendelea. Tumieni Dawati la Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje kupata maelezo zaidi ya fursa zinazopatikana kwa uwekezaji.

5. USHIRIKISHWAJI WA DIASPORA KULETA MAENDELEO

Mheshimiwa Balozi, Mabibi na Mabwana,

Serikali inatambua shauku yenu kubwa ya kutaka kufahamu nafasi yenu katika kuleta maendeleo Tanzania. Umuhimu huo ni moja ya hatua ya makusudi iliyochukuliwa na Serikali ya kuwatambua Diaspora kama moja ya wadau muhimu kuleta maendeleo Tanzania.  Aidha, serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa michango yenu inaleta maendeleo chanya yenye kukuza pato la Taifa; kufungua soko la bidhaa za Kitanzania nje ya nchi; kukuza sekta ya utalii na uwekezaji, n.k.   Hivyo, ni muhimu mjipange kutumia nafasi zenu mkiwa ughaibuni kuhakikisha kuwa mnasaidia kulea maendeleo Tanzania kupitia elimu, rasilimali fedha, ujuzi au maarifa.

6. MAKONGAMANO YA DIASPORA

Serikali imekuwa ikiratibu makongamano ya Diaspora ndani na nje ya nchi; ambayo yamekuwa yakileta mafanikio makubwa nchini kupitia michango mbalimbali ya maendeleo inayotolewa na Diaspora. Kwa mwaka huu, Wizara inatarajia kuandaa tena Kongamano la Diaspora, ambalo litakuwa la nne (4) kufanyika Tanzania. Kama mtakumbuka Kongamano la Tatu lilifanyika mwaka jana mwezi Agosti huko Zanzibar; ambapo Diaspora kutoka maeneo mbalimbali walishiriki na kukutana na Taasisi Binafsi na za Serikali, ili kupata huduma na taarifa za fursa za utalii, uwekezaji na biashara katika sekta hizo.  Tutawajulisha tarehe kamili za Kongamano kwa ushiriki wenu.

7. MATARAJIO YA SERIKALI

Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikikuza sekta za kipaumbele ili kuchochea na kupanua wigo wa uwekezaji katika viwanda vidogo, vya kati na vikubwa, ili kufikia uchumi wa kati hapo mwaka 2025. Ni rai ya Serikali kuwa Diaspora wa Kitanzania waendelee kuwa wazalendo wenye machungu na nchi yao; ili washiriki kikamilifu katika kuijenga Tanzania ya viwanda, yenye uchumi wa kati wenye kuleta mabadiliko ya maendeleo bora kwa kila mwananchi. Hivyo, ni mategemeo ya Serikali kuwa mtaendelea kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania popote mlipo katika kuitangaza nchi yetu kutokana na vivutio vya utalii na maliasili, fursa za uwekezaji na biashara zilizopo nchini Tanzania.

8. HITIMISHO

Mhe. Balozi, Mabibi na Mabwana,

Naomba nimalize na hayo machache na kutumia nafasi hii tena kuwashukuru sana kwa ukarimu wenu. Nawaomba msichoke kutuma nyumbani chochote mlichokichuma iwe elimu, ujuzi, maarifa, au rasilimali fedha; ili kuleta maendeleo ya Taifa letu. Vile vile, niwaombe mtoe ushirikiano mzuri kwa Mhe. Balozi Madafa na kuitumia ipasavyo Ofisi ya Ubalozi kama kiunganisho cha kushirikiana nanyi katika kuitangaza nchi yenu na kuleta maendeleo chanya kwa vizazi vya sasa na baadae.

Wosia wangu ni kuwaomba wote kuwa waadilifu, muishi kwa kufuata taratibu na sheria za nchi hii; msijiingize katika vitendo viovu. Jaribuni kusaidiana; unapoona mwenzio anapotea jaribu kumsaidia kwa kumrudisha kwenye mstari. Tudumishe upendo na ushirikiano. Imarisheni umoja wa Watanzania kwa kulinda heshima ya Taifa la Tanzania.  Nyie ni Mabalozi wa Tanzania huku nje. Taifa linawategemea.  Chochote kizuri mnachokipata au kukisikia ambacho ni cha manufaa kwa nchi yetu, peleka taarifa ofisi ya ubalozi kwa hatua zaidi. Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu. Basi tujenge kwa pamoja Umoja wa Taifa letu. 

Asanteni sana kwa kunisikiliza!








All the contents on this site are copyrighted ©.