2017-05-08 10:53:00

Papa Francisko hujaji wa matumaini na amani nchini Ureno!


Rozari takatifu ni muhtasari wa historia nzima ya ukombozi wa mwanadamu na ni sehemu ya maisha ya Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wakati huu wa Mwezi Rozari Takatifu kusali kwa ajili ya: toba na wongofu wa ndani pamoja na kuombea amani duniani kama Bikira Maria alivyowataka Watoto wa Fatima, yaani Francis, Yacinta Marto na Lucia dos Santos, hasa wakati huu, Kanisa linapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea watoto hawa!

Baba Mtakatifu anasema, kuanzia tarehe 12- 13 Mei 2017 atafanya hija ya kitume mjini Fatima, nchini Ureno kushiriki Jubilei ya miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima, sanjari na kuwatangaza Wenyeheri Francis na Yacinta Marto kuwa ni watakatifu.  Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican anakaza kusema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Ureno inaongozwa na kauli mbiu “Papa Francisko mjini Fatima pamoja na Bikira Maria kama mahujaji wa matumaini na amani”. Kumbe, hapa mkazo si hija ya kitume, bali, Baba Mtakatifu anakwenda kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima kama hujaji wa matumaini na amani.

Baba Mtakatifu anatarajiwa kuondoka mjini Vatican kuelekea Fatima, Ureno na kutua kwenye Uwanja wa Kijeshi wa Monte Real. Hapa atapokelewa na Rais wa Ureno pamoja na kufanya naye mazungumzo ya faragha. Anatarajiwa kuonana na kuzungumza na Waziri mkuu wa Ureno, Jumamosi tarehe 13 Mei 2017. Kumbe, hija nzima ya Baba Mtakatifu Francisko inajikita katika Ibada kwa Bikira Maria wa Fatima: Sala na shukrani ni mambo makuu yanayoongoza hija ya 19 ya Baba Mtakatifu Francisko kimataifa. Ureno inakuwa ni nchi ya 28 kutembelewa na Papa Francisko nje ya Italia. Akiwa mjini Fatima, Baba Mtakatifu atatoa hotuba tatu muhimu na kusali mbele ya Sanamu ya Bikira Maria wa Fatima. Hotuba zake zote zitakuwa kwa lugha ya Kireno!

Ratiba elekezi katika undani wake inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu anatarajiwa kuwasili mjini Fatima Ijumaa, tarehe 12 Mei 2017 majira ya jioni saa 10: 20 kwa saa za Ulaya na kupokelewa na Rais Marcelo Rebelo de Sousa wa Ureno. Atapata nafasi ya kutembelea na kusali kidogo kwenye Kikanisa cha Uwanja wa Ndege wa Kijeshi na kutoa heshima zake kwa Bikira Maria wa Fatima kama wafavyo mahujaji wengine wanapowasili mjini Fatima. Jioni hiyo, Baba Mtakatifu atabariki mishumaa na kusali Rozari Takatifu pamoja na kutoa hotuba. Baada ya Baba Mtakatifu kuondoka katika eneo hili, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa mahujaji watakaokuwepo hapo!

Jumamosi, tarehe 13 Mei 2017, majira ya asubuhi, Baba Mtakatifu atatembelea na kusali kwenye makaburi ya Watoto wa Fatima na baadaye, kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu ambamo atawatangaza Mwenyeheri Francis na Yacinta Marto kuwa watakatifu. Tukio hili litahitimishwa kwa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, baraka kwa wagonjwa pamoja na kuwapatia salam zake za pekee. Baba Mtakatifu Francisko atapata chakula cha mchana na Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno na hatimaye, majira ya jioni kuagwa rasmi, tayari kuondoka na kurejea tena mjini Vatican kuendelea na maisha na utume wake. Anatarajiwa kuwasili mjini Roma majira ya saa 1:00 za Jioni kwa saa za Ulaya.

Takwimu zinaonesha kwamba, tayari kuna umati mkubwa waamini na mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia ambao tayari wanajipanga kwenda kuhudhuria kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima. Ni tukio la aina yake, linalowajumuisha Makardinali 8, Maaskofu 71, Mapadre 2000 pamoja na wakuu kadhaa wa serikali mbali mbali duniani wenye Ibada kwa Bikira Maria wa Fatima.

Baba Mtakatifu katika hija yake kwenye Madhabahu ya Fatima ataongozana na Kardinali Josè Saraiva Martins, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu pamoja na Kardinali Monteiro de Castro. Baba Mtakatifu Francisko anakuwa ni Papa wa nne kutembelea Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima. Mwenyeheri Paulo VI alitembelea Madhabahu haya wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima. Mtakatifu Yohane Paulo II akatembelea madhabahu haya mara tatu katika Mwaka 1982, 1991 na Mwaka 2000. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alitembelea Madhabahu haya kunako mwaka 2010.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican itakuwa nawe bega kwa bega ili kukujulisha yale mambo msingi yanayojiri katika hija ya Baba Mtakatifu Francisko huko Fatima nchini Ureno, kuanzia tarehe 12 – 13 Mei 2017.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.