2017-05-08 15:34:00

Kardinali Crescenzio Sepe anaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Upadre


Upadre ni zawadi ambayo Mwenyezi Mungu amewakirimia baadhi ya waja wake ili kushiriki katika huduma ya Neno, Sakramenti na Huduma kama vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake. Mapadre wanashiriki dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Dhamana hii wanaitekeleza kwa namna ya pekee katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa pamoja na huduma kwa familia ya Mungu. Hivi karibuni, Kardinali Crescnezio Sepe, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Napoli, Italia, ameadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Upadre kwa kumwimbia Mungu utenzi wa sifa, shukrani na kuomba tena rehema na baraka ya kuendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani zake.

Tukio hili limehudhuriwa na umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Napoli. Anaadhimisha pia kumbu kumbu ya Miaka 25 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu. Kumbe, imekuwa ni nafasi ya pekee kumshukuru Mungu, aliyemkirimia zawadi ya wito wa Upadre na kulikamilisha Daraja Takatifu kwa kuwekewa mikono kama Askofu na sasa kama Kardinali. Anasema, yeye ni mchungaji mwema anayeyasadaka maisha yake kwa ajili ya kondoo wake, utambulisho unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na una maana kubwa sana katika Maandiko Matakatifu. Hii inatokana na ukweli kwamba, Mungu mwenyewe ndiye mchungaji mkuu wa kondoo wake, anawalinda, anawatunza na kuwaongoza kwenye malisho ya majani mabichi. Yesu, Neno wa Mungu aliyetwaa mwili na kukaa kati ya watu wake ndiye Mchungaji mwema wa Agano Jipya, aliyejisadaka pale Msalabani ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kristo katika maisha na utume wake, alijitaabisha kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu, akawaondolea dhambi zao na kuwapatia mahitaji yao msingi: kiroho na kimwili.

Kardinali Sepe anasema, hata yeye pia aliitwa, akaisikia sauti na kuitikia wito kwa furaha na bashasha kubwa akamtumikia Mungu na jirani kama Jaalimu mjini Roma; akajikuta anatumwa nchini Brazil kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu waliokuwa wanaogelea katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato na huko kwa kweli ameacha sehemu ya moyo wake, kwa kuguswa na hali ya watu wa Mungu eneo hili.

Anasema, Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya matumaini na maisha mapya, akabahatika kuwekwa wakfu kuwa Askofu na Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Kardinali na kwa sasa imepita miaka kumi na mmoja tangu alipoteuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Napoli, Italia. Hapa ni mahali ambapo kumesheheni historia ya maisha, tamaduni, imani na ibada hasa kwa Bikira Maria na watakatifu kama Januari, waliotajirisha na kuboresha historia ya Jimbo kuu la Napoli na watu wake! Jimbo kuu la Napoli, linaendelea kujizatiti kwa ajili ya huduma kwa familia ya Mungu, ili kusikiliza na kujibu kilio cha watu wake; bila kusahau matumaini yao. Katika maadhimisho ya Jubilei maalum ya mwaka 2011, familia ya Mungu Jimbo kuu la Napoli, ikaonesha umoja, upendo na mshikamano wa dhati, ili kujikita katika kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii! Waamini wakataka kuhakikisha kwamba, wanakita maisha yao katika tunu msingi za Kiinjili, kiutu na maadili mema ili kuondokana na matendo ya giza yaliyokuwa yanachafua utu na utambulisho wao.

Yesu mchungaji mwema na Mlango wa upendo na huruma ya Mungu, akawajalia waamini wa Jimbo kuu la Napoli kuwa ni vyombo na mashuhuda upendo, mshikamano na udugu; akawawezesha waamini kusimama kidete katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na utawala wa sheria, ili kuzima kiu na njaa ya haki na amani. Huu ndio wito wa binadamu unaobubujika na kujikita katika wito wa Mungu, ni wito wa Padre na Askofu. Kila mwamini anaalikwa kuwa ni mchungaji mwema wa maisha, ndani ya Jumuiya, na eneo la kazi kwa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya uhai, upendo, uhuru na urafiki wa dhati! Kardinali Crescenzio Sepe, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika hija ya imani, matumaini na mapendo, ili kweli kila mmoja aweze kuwa tayari kujisadaka bila ya kujibakiza katika huduma kwa Mungu na jirani, kwa kutambua kwamba, wote wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa ni wachungaji wema na malango ya huruma na upendo wa Mungu duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.