2017-05-06 14:37:00

Jumapili ya Kuombea Miito Duniani: Ushuhuda wa Masista wa Mt. Yosefu!


Maisha ya kitawa hudokeza mwaliko wa utakatifu katika maisha ya kiroho; udugu katika maisha ya pamoja katika jumuiya, sadaka na majitoleo katika huduma makini kwa familia ya Mungu. Yote haya hufumbatwa katika mashauri ya Kiinjili, yaani: Usafi wa moyo, utii na ufukara. Watawa katika maisha yao, wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa waaminifu katika nadhiri zao kama kielelezo cha upendo kwa Mungu, Kristo na Kanisa lake. Shirika la Masista wa Mtakatifu Yosefu, Jimbo kuu la Mombasa, Kenya lilianzishwa kunako mwaka 1938 na Askofu John Hefferman, CSSP, wa Shirika la Roho Mtakatifu, aliyekuwa msimamizi wa kitume wa Vikarieti ya Zanzibar kwa wakati ule. Alisaidiana kwa karibu sana na Mama Amadea, na Shirika hili likawekwa chini ya ulinzi na usimamizi wa Mtakatifu Yosefu, Baba Mlishi wa Yesu na mlinzi wa Vikarieti ya Zanzibar.

Askofu John Hefferman alianzisha Shirika la Masista wa Mtakatifu Yosefu, ili kusaidia mchakato wa uinjilishaji wa kina, uliokuwa unagusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Alitaka masista wawe kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu katika huduma kwa wagonjwa; katekesi kwa watoto, wazee na vijana; elimu makini kwa watoto kwa kutambua kwamba, elimu ni mkombozi wa mwanadamu bila kusahau maendeleo endelevu. Alipenda kukita shughuli na utume wa Masista wa Mtakatifu Yosefu kwanza kabisa Mombasa iliyokuwa na changamoto nyingi, lakini hatimaye, utume wao ukaenea nchini Kenya.

Shughuli ya malezi na majiundo ya kitawa ilifanywa chini ya usimamizi wa Masista wa Damu Azizi ya Yesu na kwa namna ya pekee chini ya uongozi wa Sr. Rosalina, tunayemkumbuka kama mwanzilishi mwenza wa Shirika. Akawapokea wasichana wa kwanza walionesha nia ya kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani kwa njia ya maisha ya kitawa. Bura, iliyoko mjini Taita, ikawa ni nyumba mama hadi leo. Masista wetu wa kwanza wakaweka nadhiri zao tarehe 8 Desemba 1941 na kujiweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili.

Roho yetu ya Shirika inajikita zaidi katika maisha ya Kibenediktini, tukiongozwa na kauli mbiu “Sala na kazi” yaani “Ora et Labora”. Hizi ndizo sifa kuu za Mtawa wa Shirika la Masista wa Mtakatifu Yosefu, Jimbo kuu la Mombasa. Tunapenda kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano na Kristo Yesu kwa njia ya Sala, Tafakari ya Neno la Mungu; kwa kuadhimisha Liturujia Takatifu, lakini zaidi kwa njia ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wetu. Kwa njia ya Sala na Kazi, tunamtukuza, tunamsifu na kumshangilia Mwenyezi Mungu, aliye asili ya miito yote. Kwetu sisi Mtakatifu Yosefu ni mfano bora wa kuigwa katika kazi: umakini, usikivu, uadilifu na utayari wa kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha.

Kwa njia ya sala na kazi na kwa mfano wa Mtakatifu Yosefu, Watawa wetu wanajisadaka kwa ajili ya kushiriki katika mchakato wa kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la umaskini, ujinga na magonjwa; mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu! Tunaishi katika jumuiya ili kudumu katika moyo mmoja na roho moja kama walivyokuwa Wakristo wa Kanisa la Mwanzo, ili kuimarisha na kudumisha upendo wa Mungu ndani mwetu, tayari kuwashirikisha wengine amana hii ya maisha ya kiroho. Maisha ya Kijumuiya ni sehemu ya utekelezaji wa Amri ya Upendo kwa Mungu na jirani, muhtasari wa Mafundisho makuu ya Yesu kwa wanafunzi wake. Sala, Tafakari na Ibada mbali mbali zinaonesha uwepo endelevu wa Kristo kati yetu, kielelezo makini cha umoja na udugu katika maisha ya kitawa. Huu ni msaada mkubwa katika kupyaisha maisha yetu ya kiroho na huduma kwa jirani zetu!

Utume wetu unatuongoza ili kweli tuweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu katika hali ya unyenyekevu na moyo mkuu, kwa kutolea yote kama sehemu ya sala na maisha yetu ya kila siku, tunapojitahidi kumfuasa, kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliye: Mwalimu, Mganga na Nabii. Tunatumwa kuwafundisha watu matendo makuu ya Mungu kwa njia ya Neno; kuwaganga wagonjwa, wazee na wale wote wanaoteseka: kiroho na kimwili: yaani watoto yatima, watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi; wafungwa na wale wote wanaoonewa na kupuuzwa. Wote hawa tunawapatia ujumbe wa matumaini katika mahangaiko yao! Sisi tunataka kuwa mashuhuda wa Injili ya huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake.

Kwa sasa, tunatekeleza utume wetu Jimbo kuu la Mombasa, Malindi, Machakos, Kitui, Nakuru na Jimbo kuu la Nairobi. Kwa upande wa Tanzania, tunafanya utume wetu Jimbo kuu la Dar es Salaam, Jimbo kuu la Arusha pamoja na Jimbo Katoliki la Bukoba. Baba Mtakatifu Francisko anatukumbusha kwamba, Jumuiya ya Kikristo ni mahali mahususi kabisa pa kuibua, kukuza na kushuhudia wito! Kwa msichana anayejisikia kuwa Mtawa, basi awasiliane na Paroko wake, kwa msaada zaidi. Kwa wale wanaotumia mitandao, wanaweza kuwasiliana nasi kwa anuani ifuatayo:

www.ssjmombasa.org.

Na SR. SYGOLINAH MGHOI WACHENJE, SSJMombasa.








All the contents on this site are copyrighted ©.