2017-05-05 14:50:00

Papa Francisko kujibu kero na changamoto za vijana kuhusu amani!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 6 Mei 2017 atakutana na kuzungumza na wanafunzi kutoka sehemu mbali mbali za Italia. Atatumia fursa hii kuweza kujibu maswali na kero za vijana wa kizazi kipya kuhusu umuhimu na dhamana ya kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha Injili ya amani duniani, dhidi ya vita, chuki, uhasama na mipasuko ya kijamii. Lengo ni kuwasaidia vijana kuanza kujenga ndani mwao utamaduni wa haki, amani; upendo, udugu; huku kwa pamoja wakisimama kidete kulinda na kuendeleza nyumba ya wote! Tukio hili limeandaliwa na Baraza la Kipapa la huduma ya maendeleo endelevu ya binadamu na kama sehemu ya mchakato wa Mama Kanisa kutaka kuwasikiliza vijana; Kanisa linapojiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana inayoongozwa na kauli mbiu: “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito” itakayotimua vumbi mjini Vatican mwezi Oktoba, 2018.

Rais Sergio Mattarella wa Italia katika ujumbe wake kwa vijana takribani 7, 000 anapenda kuwatakia heri na baraka wanafunzi, walimu, walezi na wadau wote walioandaa tukio hili maalum linaliwakutanisha vijana ili kwa pamoja waweze kwenda kwenye shule ya amani, kwa kutambua kwamba, wanaishi na kutenda katika nyumba ya wote inayopaswa kulindwa, kutunzwa na kudumishwa na wengi. Vijana wanapaswa kuzingatia na kuheshimu haki zao msingi sanjari na wajibu kwani haya ni mambo mawili yanayotegemeana na kukamilishana kwa ajili ya ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu. 

Vijana wanapaswa kukumbuka kwamba, kuna uhusiano wa dhati kati ya: maendeleo endelevu, mazingira; mchakato wa kuondokana na ukosefu wa usawa katika jamii unaounda matabaka ya watu, ili kukuza na kudumisha chachu ya maendeleo hasa miongoni mwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni ma jamii! Hii ni dhamana na wajibu unaopaswa kutekelezwa na wote pasi na ubaguzi wala kudhani kwamba, ni dhamana inayotekelezwa na Serikali pamoja na taasisi mbali mbali. Vijana washikamane katika ujenzi wa jamii inayomsikwa katika usawa, haki, amani, utu na heshima kwa wote!

Watambue na kuthamini tofauti zao kama sehemu ya utajiri unaopaswa kukuzwa na kudumishwa na wengi! Vijana waheshimu na kuthamini uhuru wao na mipaka yake pamoja na kutambua pia uhuru wa jirani zao. Vijana wa kizazi kipya anasema Rais Sergio Mattarella wa Italia wanapaswa kweli kufundwa katika misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Wakazie tunu msingi za kiutu, kijamii na kiroho ili kujenga na kuimarisha mtandao wa mshikamano  na ujenzi wa jumuiya.

Ni matumaini ya Rais Mattarella kwamba, vijana wataitumia fursa hii kukuza kipaji cha ubunifu na ugunduzi; sanaa ya majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kwa pamoja waweze kukua na kukomaa kiutu kama binadamu! Kati ya mada zinazojaliwa ni pamoja na umuhimu wa kufundisha na kujifunza amani; Umuhimu wa kujikita katika ujenzi wa dunia iliyo bora zaidi; raia wa ulimwengu wa utandawazi; jinsi ya kuzuia na kupambana na dhuluma, nyanyaso na kinzani miongoni mwa watoto wa dogo, changamoto za elimu katika huduma ya hadhara; umuhimu wa amani; vijana kama wajenzi na mashuhuda wa amani na hatimaye, haki zote msingi ni kwa ajili ya binadamu wote na kwamba, wote wanaweza kujizatiti kupiga vita na utandawazi usiojali wengine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.