2017-05-04 13:19:00

Kristo Yesu ndiye mchungaji mwema, igeni mfano wake!


Kanisa linaadhimisha Dominika ya Kristo Mchungaji Mwema, siku mahususi ambayo Jumuiya nzima ya waamini hualikwa kuombea miito mitakatifu yaani: maisha ya ndoa na familia, Kipadre na Kitawa! Kristo Mchungaji Mwema anajitambulisha kwetu kama kielelezo kwa Wachungaji wetu ambao kwa jina lake hupokea jukumu la kwaongoza. Kuwafundisha na kuwatakatifuza kondoo wa Mungu katika malisho bora ya Neno na Sakramenti za Kanisa Ninawaalika kwa namna ya pekee mwaka huu kuungana na Kanisa la Tanzania ambalo linaadhimisha Jubilei ya miaka 100 tangu kupata Mapadre wake wa kwanza wazalendo. Hili ni tendo la shukrani kwa Familia ya Mungu nchini Tanzania na shukrani kwa Mungu ambaye amewashirikisha watoto wake wa kitanzania jukumu hili adhimu la kuongoza, kulisha na kulitakatifuza kundi lake!

Somo la Injili ya Dominika hii linaiweka wazi njia sahihi ya mchungaji mwema. Neno la Mungu linatuambia kwamba: “Aingiaye mlangoni ni mchungaji wa kondoo. Bawabu humfungulia huyo, na kondoo huisikia sauti yake; naye huwaita kondoo wake kwa kwa majina yao na kuwapeleka nje”. Katika Injili hiyo Kristo anajitambulisha kuwa ndiye huo mlango: “Mimi ndimi mlango wa kondoo”. Sehemu hii inafafanua mahali pengine alipojitambulisha kuwa ni Njia, Ukweli na Uzima (Rej Yoh 14:6). Hili linatuelezea haiba ya kundi ambalo tunaalikwa kulichunga; ni kundi la Mungu ambalo limeshirikishwa maisha hayo ya kimbingu kwa njia ya Kristo. Utumishi wetu wa kuitangaza habari njema na kuwavuta watu wote kwa Mungu unawekewa njia yake ya kipekee ambayo bila hiyo husambaratisha kundi. Mchungaji mwema anaelekezwa kuuchota utume wake kutoka katika Fumbo la Kristo. Nje ya hapo ni kujitafutia maslahi yake binafsi na matokeo yake ni uharibifu wa utume anaokabidhiwa.

Kristo ameifafanua vyema nafasi yake hiyo na kutuonesha huo mlango tunaopaswa kuupitia. Wakati wa utume wake alitenda yote kwa ajili ya manufaa ya kondoo wake huku akiwa amepambwa na wema, huruma, upendo na kuwapatanisha au kuwarudisha kundini waliopotea. Huu ndiyo mlango ambao kila mtume wa Mungu anapaswa kuupitia kwa ajili ya kuicheza vema nafasi hii anayopangiwa na Mwenyezi Mungu. Tunu hizo chache za kiutu zilizotajwa pamoja na nyingine nyingi zililenga katika kumfanya huyu mchungaji kuwa sababu ya furaha, nguvu na matumaini kwa ndugu zake anaokutana nao. Ni mlango ambao unamuingiza mchungaji katika uwanja wa binadamu mwenzake na kumpokea katika hadhi yake anayostahili. Ni njia inayomfikisha katika ufanisi wa utume wake ambao ni kuukarabati ubinadamu uliochakazwa na dhambi.

Hivyo kila mchungaji anapaswa kurandanisha utumishi wake na Fumbo la Kristo. Mtume Petro katika somo la kwanza anausimika ukweli huo. Yeye aliwaambia Wayahudi: “Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu”. Himizo hili la kitume linathibitisha ukweli kwamba ni kwa njia Kristo Mfufuka pekee ndipo tunaingia katika wokovu wa Mungu. Ukaidi wa mwanadamu katika ukweli huu hautamsaidia kitu. Wayahudi wanaelekezwa katika njia hii na kuaswa kuacha ukaidi wao. Ukaidi wao ulimsulubisha Kristo lakini kutokana na nguvu ya utume wake na pia ili kuipatia nguvu hoja yake, kwamba ndiye njia pekee au mlango kwa zizi la kondoo Mungu alimfufua kutoka wafu na “amemfanya kuwa Bwana na Kristo”.

Baba Mtakatifu Francisko amesakafia wazo hili katika ujumbe wake maalum wa siku hii ya 54 ya kuombea miito mitakatifu wenye kichwa cha habari «kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu katika utume». Anasema kwamba: “Kuwa mfuasi katika umisionari humaanisha ushiriki hai katika utume wa Kristo. Kristo mwenyewe aliuelezea huo ndani ya Sinagogi la Nazareti kwa maneno haya: «Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema, Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa, na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa»(Lk 4:18 – 19)”. Askofu Mkuu wa Roma na kiongozi wa Kanisa Katoliki ulimwenguni anasisitiza ukweli huo wa kumfuata Kristo Mchungaji mwema kama kondoo wanavyomfuata Yeye ambaye ananuia katika ukombozi wa mwanadamu. Utume wetu uliotukuka kwa Mungu unapotoka nje ya njia hiyo unakuwa sawa na utume wa yeye asiyepitia katika mlango wa zizi na kukwea penginepo. Mchungaji mwema, anaendelea kuhimiza Halifa wa Petro, anapaswa kuwa “amepakwa mafuta na Roho Mtakatifu na kutoka kwenda kwa ndugu zake kwa ajili ya kuwatangaza kwao Neno la Mungu na kuwa kwao njia ya wokovu”.

Mtume Petro anaendelea kuhimiza kudumu katika Kristo akisema: “Kustahimili, mtendapo mema na kupata mateso, huu ndiyo wema hasa mbele za Mungu. Maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zako”. Mlango huo ambao mchungaji anapaswa kuupitia ambao ni Kristo Mfufuka ni njia inayoambatana na hadha nyingi na mateso. Upole na unyenyekevu wake ni kielelezo kwetu katika utume wetu kama wachungaji wa kondoo. Mazingira ya jamii ya leo si rafiki sana katika kuitangaza habari njema. Wakati mwingine inakatisha tamaa; wakati mwingine tunazidiwa na ubinadamu wetu na kushawishika kutuliza mateso hayo hata kwa kupitia njia za uovu. Muhimu kwetu ni kutambua kwamba tunaifanya kazi ya Mungu naye yupo daima na sisi akitushika mkono kuelekea ufanisi wa kweli na wa kudumu.

Katika hili Baba Mtakatifu Fransisko anaendelea kutukumbusha kitu katika Ujumbe wake mahsusi wa siku hii akisema: “Mbegu ya ufalme wa Mungu, ingawa ni ndogo sana, isiyoonekana na wakati mwingine kuonekana haina tija, kwa sababu ya kazi ya Mungu isiyokoma huendelea kumea katika ukimya. Hii ni sababu ya kwanza kwetu kujiamini: Mungu huyashinda matarajio yetu yote na hudumu katika kutushangaza kwa ukarimu wake. Huzifanya juhudi zetu zizae matunda nje ya matarajio ya kibinadamu”. Yote haya yarudi katika wazo la kwanza la Kristo kama mlango wa zizi la kundi. Mchungaji wa kondoo anapaswa kutimiza wajibu wake na kushirikisha vipaji vyake kwa uaminifu. Vikwazo, mateso na upinzani visiwe sababu ya kukata tamaa. Hii ni kazi ya Mungu na Yeye mwenyewe aliyeianzisha kazi hiyo njema ndani mwako, basi wenyewe ataikamilisha.

Tunapoiombea miito mitakatifu pia tunapaswa kuombea chimbuko lake ambalo nalo si kitu kingine tofauti na wito mtakatifu pia. Hapa nataka kuzungumzia familia za kikristo. Tunaposema kuwa Kristo ni mlango ambao mchungaji anapasa kuupitia tunamaanisha pia kitalu hiki cha msingi cha malezi ya kibinadamu kipaswa kuakisi uhalisia wa mlango huo yaani Kristo. Uwepo wake unapaswa kuwa hai daima ili kutokana na familia hizi wazaliwe na kukuzwa wachungaji wema. Jukumu la kimisionari ingawa kwa sehemu kubwa linajidhihirisha katika miito mitakatifu ya ukasisi na utawa lakini bado linasalia kuwa ni la jumuiya nzima ya wakristo. Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wake analitazama hilo kama tabia maalum kabisa ambayo inashikamana na kuutambulisha ukristo wetu. Yeye anasema kwamba: “Wakristo wote wameitwa kuwa Wamisionari wa injili. Hatuipokei tunu ya upendo wa Mungu kama wafuasi wa Kristo kwa ajili ya faraja zetu binafsi, au kwa kujikweza sisi binafsi au kwa ajili ya shughuli zetu. Sisi tunasalia kuwa tu ni wanaume na wanawake tulioguswa na kugeuzwa na furaha ya upendo wa Mungu na ambao hatuwezi kuuhifadhi kwa ajili yetu tu. «Furaha ya Injili ambayo huichachusha jumuiya ya wafuasi ni furaha ya kimisionari» (Furaha ya Injili, 21)”.

Katika familia za kikristo ambamo  kwamo miito mitakatifu huchipukia «Furaha ya Injili» ambayo ni Kristo Mchungaji Mwema inapaswa kuonekana na kuzifanya familia hizo kuwa mahali mahsusi kwa ajili kuonesha njia, mwanga na mlango wa kupitia kuelekea katika miito mitakatifu. Tuziombee familia zetu na jumuiya nzima ya kikristo ili kusudi kwa sala na mifano yao ya maisha miito mitakatifu izaliwe kwa wingi na Kanisa liendelee kupata wachungaji wengi wanaotenda mithili ya Kristo Mchungaji mwema.

Kutoka studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.