2017-05-01 12:55:00

Siku ya Wafanyakazi Duniani: Ajira, Utu, haki na wajibu!


Mei Mosi, kila mwaka, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani. Hii ni siku muafaka ya kutafakari na kutathmini kazi iliyofanyika kwa kipindi cha mwaka mzima, ili kujiwekea tena sera na mikakati ya kuboresha mafanikio yaliyofikiwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Jambo linalopewa uzito wa pekee hapa ni ushirikishwaji wa wadau mbali mbali katika kuzalisha na kutoa huduma sanjari na kujenga mshikamano wa dhati kati ya vyama vya wafanyakazi na wanachama wao kwa kuzingatia kanuni, sheria na nidhamu; weledi, uadilifu na uwajibikaji; utawala bora, ulinzi na usalama kazini!

Mama Kanisa, Mei Mosi anaadhimisha kumbu kumbu ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, aliyetoka jasho ili kuhakikisha kwamba, Familia Takatifu inapata mahitaji yake msingi, ulinzi na usalama. Hii ni siku kuu iliyoanzishwa na Baba Mtakatifu Pio XII kunako mwaka 1955. Lengo la Mama Kanisa ni kutambua na kuenzi heshima ya kufanya kazi kama utimilifu wa utu wa mwanadamu. Hii ni sehemu ya mchakato wa amri ya kuendeleza kazi ya uumbaji yaani kuutisha ulimwengu, uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, hii ndiyo huduma makini inayopaswa kutolewa na utekelezaji wa kazi.

Kanisa linafundisha kwamba, kazi ni haki msingi ya binadamu na ni jambo jema na kwamba, ukosefu wa fursa za ajira ni janga la kijamii, changamoto kubwa katika nyakati hizi, baada ya mtikisiko wa uchumi kitaifa na kimataifa. Kanisa linakazia ajira kamili, ili kuondokana na mifumo ya ajira inayopelekea wafanyakazi kunyanyasika na kudhulumiwa utu, heshima na haki zao msingi, kiasi hata wafanyakazi kushindwa kutekeleza ndoto katika maisha yao! Ili kazi iweze kuwa na tija, kuna haja kwa wafanyakazi kuhakikisha kwamba wanatumia vyema: akili, uwezo na taaluma yao, kumbe, mfumo wa elimu unaotolewa na nnchi yoyote ile unapaswa kumjengea uwezo mfanyakazi ili aweze kutekeleza vyema wajibu wake. Ikumbukwe kwamba, kazi ni msingi wa malezi na tunu msingi za maisha ya familia, ni haki na wito wa kila familia.

Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi  Duniani, mara nyingine imekuwa ni siku ya wafanyakazi kudai ongezeko la mishahara, hali nzuri na mazingira bora zaidi ya kazi. Yote haya yanaweza kufikiwa ikiwa kama kutakuwepo na tija na uzalishaji wa kutosha na kwamba, ufanisi kazini unatokana na mchango makini unaotolewa na wafanyakazi wenyewe. Wizi, ufisadi, udanganyifu wa kiwango cha elimu, hujuma na tamaa kazini ni kati ya mambo yanayochangia kukwamisha mchango wa mafanikio bora kazini.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume “Evangelii gaudium” yaani furaha ya Injili, changamoto mbali mbali zinazoendelea kuwakabili watu katika ulimwengu mamboleo zinawanyima ile furaha ya maisha. Hizi ni changamoto zinazopaswa kuvaliwa njuga kwa njia ya ushirikiano na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa unaoongozwa na kanuni auni. Kumekuwepo na maendeleo makubwa katika maboresho ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya wengi. Kwa bahati mbaya, Jamii imejikuta ikiishi katika ushindani mkubwa sayansi na teknolojia; silaha na nguvu za kiuchumi na matokeo yake ni kuibuka kwa uchumi huria ambao umejenga matakaba makubwa na watu wengi kujikuta wakiwa wamesukumizwa pembezoni mwa jamii.

Huu ndio mfumo wa uchumi usioshirikishi, mfumo unaotafuta faida kubwa kwa mateso ya wengi. Matokeo ni ukosefu wa fursa za ajira, ukosefu wa haki msingi za binadamu, utu na heshima yake. Huu ni uchumi unaojikita katika ubinafsi kwa kuambata utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko yaw engine. Kinachozingatiwa hapa ni fedha inayoonekana kuwa kama “sabuni ya roho”. Baba Mtakatifu Francisko anakumbusha kwamba, mfumo wa fedha unapaswa kujielekeza katika kutoa huduma badala ya kutawala, matokeo yake ni hali ngumu ya maisha kwa watu wengi, vurugu na kinzani. Ili kweli kazi iweze kuwa ni sehemu ya mchakato wa utimilifu wa utu na maisha ya binadamu, sera za uchumi na maendeleo zinapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi; kwa kuzingatia uchumi shirikishi unaowaamba watu wote pasi na kuwatenga! Hapa kila mdau anapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara. Ikumbukwe kwamba, haki daima inaambatana na wajibu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.