2017-05-01 12:29:00

Papa Francisko achonga na waandishi wa habari wakati akirejea Vatican


Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha hija yake ya kumi na nane kimataifa nchini Misri iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu “Papa wa amani nchini Misri” Jumamosi mchana, tarehe 29 Aprili 2017 ambako amekazia umuhimu wa majadiliano ya kidini kama njia ya kujenga na kudumisha haki, amani, maridhiano. Amesisitiza juu ya uekumene wa damu unaofumbatwa katika : ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake sanjari na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Amewataka Wakristo kuwa ni mashuhuda wa Injili ya upendo; vyombo vya amani na wajenzi wa madaraja ya ushirikiano kati ya watu! Anasema, angependa kwenda kutembelea Piramidi, lakini nafasi imekuwa finyu, ingawa baadhi ya wasaidizi wake, wametumia nafasi hii kujionea fahari ya utamaduni wa Wamisri!

Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kurejea mjini Vatican alipata nafasi ya “kuchonga” pamoja na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake nchini Misri. Katika mahojiano hayo amekazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika majadiliano na diplomasia ili kuepusha majanga ya vita yanayoweza kutokea kutokana na malumbano na majaribio ya kijeshi yanayoendelea kujionesha kati ya Marekani na Korea ya Kaskazini, changamoto ya wakimbizi na wahamiaji duniani; hali tete ya kisiasa nchini Venezuela; dhamana na mchango wa Umoja wa Mataifa pamoja na mchakato wa majadiliano ya kiekumene!

Baba Mtakatifu amechukua fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake kwa kazi nzuri waliyoifanya wakati wa hija yake nchini Misri. Anasema, pamoja na mambo mengine, alibahatika kufanya mazungumzo ya faragha na Rais Abdel Fattah Al Sisi wa Misri, Papa Tawadros II wa Kanisa la Kikoptik pamoja na Patriaki Ibrahim Isaac Sedrack wa Kanisa Katoliki la Kikoptik pamoja na  Sheikh Muhammad Al Tayyib, Imam mkuu  wa Msikiti wa Al-Azhar, Cairo. Yale mambo ya faragha yataendelea kuwa ya faragha.

Baba Mtakatifu anasema, kuma Vita Kuu ya Tatu ya Dunia inayoendelea kupamba moto sehemu mbali mbali za dunia, vita ambayo inapiganwa vipande vipande. Vitisho vya mashambulizi ya kivita vinazidi kupamba moto kutokana na malumbano yanayoendelea kati ya Korea ya Kaskazini na Marekani. Kwa muda wa mwaka mzima, Korea ya Kaskazini inafanya majaribio ya kurusha makombora ya silaha kali kinyume cha taratibu na kanuni za Umoja wa Mataifa. Kumbe, majadiliano na diplomasia ya kimataifa ni muhimu sana  katika mchakato wa kutafuta suluhu ya kudumu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu kwa sasa na kwa siku za usoni.

Leo hii vita ya nyuklia ikifumuka duniani, itasababisha madhara makubwa kwa watu, mali, tamaduni pamoja na urithi wao. Dunia haitakuwa na nguvu ya kuweza kuhimili kishindo cha madhara ya vita, ndiyo maana Umoja wa Mataifa unapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake katika kutatua migogoro na kinzani zinazoendelea kujitokeza katika uso wa nchi! Hata wakati huu kuna moshi wa vita na madhara yake unaendelea kufuka sehemu mbali mbali za dunia: huko Mashariki ya kati na baadhi ya nchi Barani Afrika. Kuna nchi wapatanishi kama Norway zinaendelea kusaidia upatanishi katika kinzani na migogoro hii, lakini, Umoja wa Mataifa unapaswa kushika hatamu ya uongozi, kwani kidogo unasinzia katika masuala haya. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hana ubaguzi kwa Rais au kiongozi wa nchi anayeomba kuonana na kuzungumza naye! Hadi wakati huu hajapata ombi maalum kutoka kwa Rais Donald Trump wa Marekani kutaka kuzungumza naye, wakati atakapotembelea Italia, ili kushiriki katika Mkutano wa G7.

Baba Mtakatifu anasema, Venezuela inakabiliwa na hali tete sana ya kisiasa baada ya makundi makubwa makubwa ya wananchi nchini Venezuela kuendelea kuandama kila siku yakitaka Rais Nicolás Maduro Moros kung’atuka kutoka madarakani. Baba Mtakatifu anasema, anaipenda sana Venezuela na watu wake na kwamba, Vatican imejitahidi kufanya majadiliano ya kidiplomasia na takribani Marais wanne, lakini mazungumzo haya bado hayajafua dafu! Yale mambo msingi yanayopaswa kutekelezwa kwa ajili ya kujenga na kudumisha haki, amani na maridhiano nchini Venezuela yanapaswa kutekelezwa bila kuchelewa!

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, kampeni za uchaguzi wa Marais sehemu mbali mbali za Ulaya zimejichimbia zaidi kwenye tema ya wakimbizi na wahamiaji ili kujipatia umaarufu na kujijenga kisiasa. Jumuiya ya Ulaya isipokuwa makini kujibu changamoto msingi za maisha ya watu wake, itaporomoka. Huu ndio ukweli wa mambo. Uhamiaji ni sehemu ya maisha ya mwanadamu na wala changamoto hii haikuanza leo! Lakini, Jumuiya ya Ulaya inaonekana kukereka sana na changamoto ya wakimbizi na wahamiaji. Lakini, ikumbukwe kwamba, historia ya Bara la Ulaya inasimikwa katika msingi wa wahamiaji.

Changamoto ya wahamiaji na wakimbizi inapaswa kufanyiwa upembuzi wa kina na mapana, ili kuibua mbinu mkakati wa kukabiliana nayo kwa kujikita katika: utu na heshima ya binadamu; haki msingi za binadamu pamoja na kuheshimu maoni ya wengine! Haya ni maoni ambayo yanapaswa kuwa kweli na kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi na wala si kwa ajili ya kuwaenzi wanasiasa wanaotafuta umaarufu kwa kutumia migongo ya wakimbizi na wahamiaji. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kuna baadhi ya kambi za wakimbizi na wahamiaji ambazo zimegeuzwa kuwa ni kambi za mateso na mahangaiko! Watu hawana uhuru wa kutembea, wamefungiwa ndani na hawawezi kutoka.

Akizungumzia kuhusu kesi ya Giulio Regen kijana mtafiti kutoka Italia aliyeuwawa kikatiliki nchini Misri kunako mwaka 2016 anasema, yale mambo ya faragha yanabaki kuwa ni faragha. Amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wazazi wake, Vatican ikaamua kuivalia njuga kesi hii, lakini bado kesi hii inaendelea kuwa ni faragha. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika tunu msingi za maisha kama vile: haki na amani; usawa, uhuru wa kuabudu na kidini; mambo msingi yanayopaswa kuvaliwa njuga na Serikali mbali mbali kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Kuhusu majadiliano ya kiekumene, Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema, kumekuwepo na mauaji, nyanyaso na madhulumu kwa Wakristo kwa nyakati hizi pengine hata kuliko ilivyokuwa kwa kwenye karne za mwanzo. Huko Mashariki ya Kati kuna Wakristo wanaoendelea kuuwawa kila kukicha! Huu ndio uekumene wa damu unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa, changamoto kwa Wakristo kuendelea kutembea kwa pamoja katika uekumene wa huduma na damu; Uekumene wa sala na maisha ya kiroho! Kimsingi huu ni uekumene unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya Wakristo kwa kutoa nafasi pia kwa wanataalimungu kuendelea kujadiliana ili hatimaye, kufikia muafaka kwa mambo msingi! Uekumene unajengwa kwa kutembea pamoja! Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza waandishi wa habari kwa kazi nyeti wanaoitenda kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi! Amewataka waendelee kujizatiti katika huduma hii nyeti kwa kuwasaidia wananchi na kuboresha mawasiliano ili kweli mawasiliano yaweze kuwasaidia watu kuwa na dira na mwelekeo sahihi wa maisha, vinginevyo, watu watachanganyikiwa na kusambaratika!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.