2017-05-01 13:30:00

Juma la Kijamii nchini Italia: Uhuru, Ubunifu, Umoja na Mshikamano


Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani kwa Mwaka 2017 linasema, kuna watu wamejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia  Habari Njema ya Wokovu na kwamba kazi ni sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji wa kina, jambo ambalo limepewa kipaumbele cha kwanza na Mama Kanisa tangu mwanzo kabisa wa uhai wake. Kuanzia tarehe 26 hadi 29 Oktoba 2017, huko Cagliari, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia litakuwa linaadhimisha Juma la Kijamii nchini Italia ambalo kwa mwaka 2017 linaongozwa na kauli mbiu “Kazi tunayohitaji: ni ile inayofanywa kwa uhuru, kwa ubunifu kwa kushirikiana na kushikamana na wengine” ili kudhihirisha na kudumisha utu, heshima na maisha ya binadamu wote! Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linakazia umuhimu wa haki katika kazi!

Ukosefu wa fursa za ajira nchini Italia ni kati ya changamoto petu sana hasa miongoni mwa vijana, lakini waathirika wakuu ni vijana wanaotoka Kusini mwa Italia. Kuna zaidi ya watu milioni 8 wanaotishiwa na baa la umaskini kutokana na ukosefu wa fursa za ajira au kudhulimiwa haki yao kwa kulipwa mshahara kiduchu! Zaidi ya watu milioni 4 nchini Italia wanaogelea katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato na kwamba, ukosefu wa fursa za ajira licha ya juhudu zote zinazofanywa na Serikali, bado ni janga la kitaifa, kumbe, kazi inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza nchini Italia.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linasema, kwa namna ya pekee kabisa linaguswa na changamoto ya ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, kiasi hata cha kushindwa kufanya maamuzi mazito katika maisha ya kuanzisha familia! Kuna wanawake wanaotengwa na kunyanyaswa kazini; watu wazima wasiokuwa na matumaini ya kupata kazi tena baada ya kuwachishwa bila kusahau wahamiaji wanaodhulumiwa kwa kufanyishwa kazi ngumu kwa msahara kiduchu! Ili kuweza kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa fursa za ajira na maendeleo ya kiuchumi kuna haja ya kuwa na wongofu wa maisha ya kiroho, kwa kuthamini ushirikishwaji na uzoefu wa wafanyakazi kazini, daima haki ikipewa msukumo wa pekee, utu na heshima ya binadamu vizikingatiwa, badala ya kutafuta faida kubwa. Kazi inapaswa kuwa ni kipimo cha uzalishaji na huduma kwa jamii; kazi inapaswa kuhusishwa na maisha, ustawi na maendeleo ya wengi!

Kumbe, kuna haja ya kujenga uchumi unaozingatia umuhimu wa kazi katika maisha ya watu! Muda wa kazi unapaswa kutoa nafasi kwa wafanyakazi, kuweza kutekeleza dhamana, majukumu na wito wao wa kifamilia. Wafanyabiashara wasaidie kuwajengea vijana uwezo wa kiuchumi kwa kuwekeza katika fursa za kazi, ili kuwapatia matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Wongofu wa maisha ya kiroho unaomwilishwa katika sera na mikakati ya kiuchumi nchini Italia ni muhimu sana katika mchakato mzima wa maboresho ya uchumi endelevu na kwamba, Italia inahitaji kuwa na kazi inayofanywa kwa uhuru, kwa ubunifu kwa kushirikiana na kushikamana na wengine”. Lengo ni kuhakikisha kwamba, kazi inapewa kipaumbele cha kwanza, kwa kuzingatia na kuheshimu tunu msingi za maisha ya binadamu; maendeleo ya sayansi na teknolojia. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuibua mbinu mkakati wa utekelezaji wa sera na mikakati hii katika masuala ya kazi, sanjari na kujibu changamoto za ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.