2017-04-30 12:45:00

Wakleri, watawa na majandokasisi wamshukuru Papa Francisko!


Ilikuwa ni furaha isiyokuwa na kifani kwa wakleri, watawa na majandokasisi kutoka Misri kuweza kukutana na Baba Mtakatifu Francisko, Khalifa wa Mtakatifu Petro aliyekwenda nchini Misri kwa ajili ya kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo. Uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko miongoni mwa viongozi wa Kanisa ni kama ushuhuda wa Kristo Mfufuka kati ya mitume wake, waliokuwa wamejifungia ndani kwa woga na hofu baada ya kushuhudia mateso na hatimaye, kifo cha Kristo Yesu Msalabani.

Mitume walibaki mjini Yerusalemu wakitarajia faraja ya Israeli na hatimaye kumfurahia Kristo Mfufuka! Kristo ambaye aliweza kuwafafanulia Wafuasi wa Emau utimilifu wa Maandiko Matakatifu yaani: Unabii na Sheria kuhusu Mtumishi wa Mungu na wao wakamtambua katika kuumega mkate! Macho yao yakafunguka, wakarejea tena hima mjini Yerusalemu kutangaza na kushuhudia kwamba, kweli Yesu amefufuka kwa wafu! Mitume waliokuwa na hofu na mashaka, wakapata tena ile furaha ya upendo wao wa kwanza kwa Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu!

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Padre Toma Adly Zaky, Gombera wa Seminari kuu ya Mtakatifu Leo Mkuu ya Upatriaki wa Kanisa Katoliki la Kikoptik, Misri wakati wakleri, watawa na majandokasisi walipokutana na kusali pamoja na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Misri, Jumamosi alasiri, tarehe 29 Aprili 2017. Viongozi hawa wa Kanisa wamemwomba Baba Mtakatifu Francisko kuwakumbuka na kuwaombea katika sala zake ili waweze kukabiliana kikamilifu na changamoto katika maisha na utume wao kwa Kristo na Kanisa lake. Wanasema, maisha ya kijumuiya ni changamoto kubwa inayofumbata uzuri na ugumu wake, lakini wanapaswa kujifunza kuishi kwa pamoja kwa njia ya unyenyekevu! Wamemwomba Baba Mtakatifu sala na sadaka yake kwa ajili ya walezi wa watawa na mapadre, ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa uaminifu, majitoleo na sadaka. Kimsingi wamemwomba Baba Mtakatifu Francisko kusali kwa ajili ya familia ya Mungu nchini Misri, ili wale wote waliokabidhiwa kwao na Kanisa waweze kukua na kukomaa katika imani, ili wafurahie wito na maisha ya viongozi wao, licha ya changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha yao ya kila siku!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.