2017-04-29 15:33:00

Uekumene wa damu udumishe umoja na mshikamano wa Wakristo duniani!


Fumbo la Pasaka ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa na kwa namna ya pekee, Makanisa ya Kikristo kwa mwaka 2017 yameadhimisha pamoja Siku kuu ya Pasaka, kwa kukumbuka ile siku Yesu alipowatokea wafuasi wake nafasi pia kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Papa Tawadros II wa Kanisa katoliki la Kikoptik nchini Misri kukutana, kusali na kukumbatiana ili kubadilishana matashi mema ya amani. Baba Mtakatifu ni hujaji na mjumbe wa amani anayekwenda kupokea pia baraka na kukumbushana matukio muhimu katika maisha na utume wa Kanisa, kama ilivyokuwa hapo tarehe 10 Mei 2013 Papa Tawadros II alipomtembelea Baba Mtakatifu Francisko, muda mfupi baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki na hiyo ikawa ni siku ya kuadhimisha Siku ya Uhusiano kati ya Wakoptik na Wakatoliki.

Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake kitume nchini Misri, Ijumaa jioni tarehe 28 Aprili 2017 alipata nafasi ya kumtembelea na kusali pamoja na Papa Tawadros II na baadaye, kuweka mkwaju kwenye tamko la pamoja kati ya viongozi hawa wawili. Baba Mtakatifu anasema, wanayo dhamana ya kuendeleza majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika maisha na utume wa Mtakatifu Petro na Mwinjili Marko kwa kuzingatia pia yale yaliyokubaliwa katika Tamko la pamoja la viongozi wa Makanisa haya mawili takribani miaka 40 iliyopita. Mwenyeheri Paulo VI na Papa Amba Shenouda III kunako mwaka 1973 walitia sahihi makubaliano yaliyomaliza kinzani na hali ya kutoaminiana iliyotokana na sababu ambazo zilikuwa nje kabisa na taalimungu. Kwa pamoja wakatambua Ubinadamu na Umungu wa Kristo; Mungu ambaye ni Mkombozi na Mfalme wa wote!

Kwa pamoja wakuu hawa Makanisa wakatangaza ukuu wa Kristo Yesu ambaye ni wao wote na hivyo kuanza kujizatiti katika mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kanisa kama sehemu ya utekelezaji wa mapenzi ya Kristo Yesu, ili wawe wamoja na ulimwengu upate kusadiki na wakamilifu katika umoja. Hakuna tena muda wa kupoteza kwani imani katika Ubatizo mmoja na Bwana mmoja ni msingi wa imani ya Kanisa inayowaunganisha wote na kuwafanya kuwa ni viumbe wapya, mwaliko ni kumaliza kasoro zilizobakia ili hatimaye, siku moja waweze kuadhimisha kwa pamoja Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Dhamana hii ni nyeti anasema Baba Mtakatifu Francisko lakini wanapaswa kutambua kwamba, daima Kristo Yesu yuko pamoja nao na wanasindikizwa na umati mkubwa wa mashuhuda wa imani na watakatifu unaowasukuma kuwa ni kielelezo hai cha Yerusalemu ya mbinguni. Kuna uhusiano wa karibu sana kati ya Mwinjili Marko aliyekazia katika Injili yake ungamo la imani la Mtakatifu Petro pale alipojibu swali la Yesu na kusema “Wewe ndiwe Kristo”! Hii ndiyo furaha wanayopaswa kuitangaza na kuishuhudia katika maisha yao kama Wakristo. Wanahamasishwa kuiungama imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, kielelezo cha imani tendaji inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini wanaozungumza lugha ya upendo katika Kristo Yesu. Umoja wa Kanisa hauna budi kujengwa, kuimarishwa na kushuhudiwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku na kwamba, iko siku wataweza kuwa wamoja kadiri ya mapenzi ya Mungu. Baba Mtakatifu anamshukuru na kumpongeza Papa Tawadros II kwa upendo na mshikamano wake wa kibaba na kichungaji kwa waamini wa Kanisa Katoliki la Kikoptik wanaoishi nchini Misri.

Kwa pamoja, wameendelea kujenga na kudumisha umoja kwa ajili ya huduma makini kwa familia ya Mungu nchini Misri. Amekuwa pia mstari wa mbele katika kufadhili mikutano ya majadiliano ya kiekumene inayotekelezwa na Kamati ya pamoja kati ya Kanisa la Kikoptik na Kanisa Katoliki, ili kuonesha kwamba, Makanisa haya yanategemeana na kukamilishana kama ilivyokuwa kwa Mwinjili Marko na Mtume Petro. Hapa mkazo ni upendo wa kidugu na umoja katika utume, kwani kwa njia ya Sakramenti Wakristo wamezaliwa kwa Maji na Roho Mtakatifu. Haya ni maisha yanayofumbatwa katika upendo uliofunuliwa na Kristo Yesu kwa gharama kubwa, kiasi hata cha kumwaga Damu yake Azizi.

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza Wakristo wote ambao wamejisadaka bila ya kujibakiza kiasi hata cha kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kama inavyoshuhudiwa kwenye Kitabu cha Orodha ya Majina ya Wafiadini wa Kanisa la Kikoptik. Hata hivi karibuni, damu ya mashuhuda wa imani imeendelea kumwagika nchini Misri kielelezo makini cha uekumene wa damu katika mateso na kifo. Damu ya mashuhuda wa imani inawaunganisha Wakristo wote na kuwaimarisha katika mchakato wa ushuhuda, ili kutangaza na kupandikiza wema, maridhiano, umoja na mshikamano; kwa kusali ili sadaka ya mashuhuda hawa wa imani isaidie kuimarisha mchakato wa umoja wa Kanisa na amani kwa wote.

Misri ni nchi ambayo imebahatika kuwa ni chemchemi ya utakatifu wa maisha ya Wakristo licha ya madhulumu na nyanyaso za kidini, lakini pia hapa ni mahali ambapo maisha ya kimonaki yalipata chimbuko lake, kielelezo makini cha matendo makuu ya Mungu katika maisha ya waja wake. Uekumene wa damu ndiyo changamoto iliyomfanya Baba Mtakatifu kufunga safari ili kufanya hija kama ilivyokuwa kwa Mwenyezi Mungu kwa kujifunua pale Mlimani Sinai na Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu kupta hifadhi. Wakristo wanahamasishwa kutoka kifua mbele ili kuanza safari ya umoja na kutangaza amani, huku wakiongozwa na Bikira Maria, Mama wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.