2017-04-28 14:05:00

Salam na matashi mema kutoka kwa Papa Francisko kwa Italia na Ugiriki


Hija ya kitume ya 18 ya Baba Mtakatifu Francisko kimataifa nchini Misri kuanzia tarehe 28 - 29 Aprili 2017 imepambwa kwa mkesha wa sala na Ibada ya Misa takatifu ili kuomba ulinzi, usalama na mafanikio ya hija hii ya kitume, ambayo pamoja na mambo mengine, inapania kujenga na kudumisha misingi ya amani na majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kweli Misri iweze kuwa kisima cha amani kwa watu wake. Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, jioni tarehe 27 Aprili 2017 alikwenda kusali na kujiaminisha kwa ulinzi na tunza ya Bikira Maria Afya ya Warumi, kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, mjini Roma. Baba Mtakatifu ameanza safari yake kuelekea Cairo, Misri, siku ya Ijumaa, asubuhi, tarehe 28 Aprili 2017. Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Fumicino, Baba Mtakatifu amesindikizwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa na Serikali ya Italia.

Akiwa njiani kuelekea Cairo, Misri, Baba Mtakatifu Francisko kama kawaida ametuma salam za matashi mema kwa Rais Sergio Mattarella wa Italia, akimwelezea kwamba, alikuwa njiani kuelekea Misri kama mjumbe wa amani, ili kukutana na Jumuiya ya waamini wa Kanisa Katoliki pamoja na waamini wa dini mbali mbali nchini Misri. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anapenda kumpatia baraka na neema yeye binafsi na kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya: kiroho, kimwili na kijamii kwa familia nzima ya Mungu nchini Italia.

Baba Mtakatifu alipokuwa anapita kwenye anga za Nchi ya Ugiriki, amemtumia salam na matashi mema Rais Prokopis Pavlopoulos wa Ugiriki, akimwelezea kuhusu hija yake ya kitume nchini Misri. Amemtumia salam na matashi mema kwake binafsi na raia wote wa Ugiriki. Amewaombea amani na nguvu kwa familia yote ya Mungu nchini humo! Hii ni mara ya pili, Misri inatembelewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro katika historia yake. Kwa mara ya kwanza, Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea Misri kunako mwaka 2000 wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 2000 ya Ukristo. Mitaa mbali mbali ya Cairo imepambwa kwa picha za Baba Mtakatifu Francisko mjumbe wa amani nchini Misri!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.