2017-04-28 07:30:00

Fumbo la Ufufuko ni tendo la huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu


Ndugu wapendwa, hali halisi inayozunguka maisha yetu ya imani kwa wakati huu ni habari ya ufufuko wa Bwana. Katika maandiko matakatifu, habari ya mateso, hukumu, kifo na maziko yake Bwana iko wazi na inaeleweka. Waandishi wetu wa maandiko matakatifu wameandika kwa mpangilio wazi. Habari inayotusumbua ni hii ya ufufuko wa Bwana – siyo kama Yesu hakufufuka – ila kafufuka namna gani na hata ushuhuda wa Petro katika somo la I na II – hautoshi kuwafanya wale wafuasi wawili kutoondoka na kushika njia kwenda zao. Aidha inaonekana wazi kuwa uelewa wetu na uwezo wa kuelezea ufufuko wahitaji bado uwepo wa Yesu, tunaona katika somo la III - mioyo yetu haikuwaka ndani yetu alipokuwa akizungumza nasi?

Ndugu zangu, ugumu unakuja hapa hasa pale ambapo tunataka kuelewa na kueleza ufufuko kwa nguvu zetu au juhudi binafsi. Na hapa ndipo tumekwama wengi wetu. Na ugumu unaongezeka na mioyo yetu inasita hasa pale ambapo tunashindwa kuishi ushuhuda wa ufufuko, pale tunaposhindwa kuishi  maisha mapya ya ufufuko – imani mpya, matumaini mapya na mapendo mapya. Pengine tunahangaika bado na jinsi ufufuko ulivyotokea na si katika kujua maana yake katika upya wa maisha – na wajibu wangu kwa tukio hilo la kimungu. Hatuna budi kujiuliza jinsi tunavyoufikisha ujumbe wa ufufuko wa Bwana katika ulimwengu huu wetu leo hii. Kwa kifupi – anayekutana na Mungu anaanza maisha mapya na ujumbe huo unapelekwa kwa wengine. Je sisi ambao tunaamini katika ufufuko wa Bwana tunaufikishaje ujumbe huo katika ulimwengu wetu wa leo?

Katika masomo yetu ya leo tunaona kuwa; Wote wanaelewa kilichotokea – zaidi sana katika somo la I – Petro anamshuhudia pamoja na wale 11 na katika somo la II – tunaalikwa kutambua thamani ya wokovu wetu. Mahangaiko yapo katika Injili – watu 2 wanakata tamaa – wanaondoka – ila inaonekana wazi kuwa walikuwa wanafunzi wake – ila kuna kitu hakiendi vizuri hapa – wanaweza kuongea juu ya Mungu lakini kama asemavyo mwandishi mmoja wengi wetu tuna uwezo wa kuongea juu ya Mungu lakini hatuongei na Mungu. Ndiyo hali waliyonayo. Hakika habari ya ufufuko inawachanganya zaidi. Tukio la hukumu, mateso na kufa kwake haliwatoki akilini mwao, ila wanaongea kwa huzuni kubwa juu ya tukio hilo la ufufuko.

Mwandishi mmoja – Annon – anasema kuwa tukio la ufufuko halikutokea katika kikao cha kamati fulani chini ya mwenyekiti na katibu aliyekuwa akiandika dondoo. Hiyo kwa aaminiye asipoteze muda kupata dondoo za kikao. Ushuhuda wa masomo ya leo watosha. Ni tokeo la huruma na upendo wa Mungu. Tukumbuke adhimisho la ibada jumapili ya pili ya pasaka – juu ya huruma takatifu ya Mungu. Kwamba ufufuko ni dhihirisho la upendo na huruma ya Mungu kwetu sisi wanadamu.

Mtakatifu Yohane Krisostomu (mwenye midomo ya dhahabu) anaelezea Pasaka hivi: wale waliokuwa wakiishi katika aibu ya dhambi sasa wanaishi kwa matumaini na katika haki: siyo tu kwamba wako huru, bali ni watakatifu, siyo tu watakatifu bali ni watu wa haki, siyo tu watu wa haki bali pia waana, siyo tu waana bali pia warithi, siyo tu warithi bali pia ndugu zake Kristo, siyo tu ndugu zake Kristo, bali warithi pamoja naye, siyo tu warithi pamoja naye bali pia wenyeji wa ufalme, siyo tu wenyeji wa ufalme wa Mungu bali pia hekalu na siyo tu warithi wa hekalu lakini vyombo vyake Roho Mtakatifu.

Ndugu zangu, ufahamu ni wokovu. Hatuna budi kutumia muda na kipindi hiki cha pasaka kuongea zaidi na Mungu. Kina Kleopa wasingeongea na Mungu hatujui hatima ya maisha yao ingekuwaje? Je nani anajua ni mara ngapi tumemwacha Yesu mfufuka apite katika au katikati ya maisha yetu bila kuongea naye? Je, ni mara ngapi tumekosa kutambua nguvu yake ya kuokoa kwa sababu ya woga, ugeni au ubaridi wa kiimani?

Kleopa na rafiki yake walikuwa wakiondoka – walielewa kile kilichotokea lakini hawakuelewa tena kilichokuwa kinaendelea. Lakini jambo hilo wanaendelea kulizungumza. Na mgeni anatokea – anaongea nini? Lk. 24:17. Unategemea nini? Wanamshangaa kwa jambo lipi? Hapa mazungumzo yakaanza – wakazungumzana – halafu wakakaa mezani, wakala na wakakaa pamoja. Baada ya kuelewa, wale wafuasi wanaondoka jioni ile na wanarudi Yerusalemu wakiwa na furaha. Kwa hawa wafuasi wawili – iko wazi – Yesu anawafunulia hayo yote – wanampata. Ni hapa macho yao yanafunguka – yule mgeni wa njiani – kumbe ndiye Bwana. Ufumbuzi huu – unawatoa katika mashaka ya zamani na kuanza upya – Yesu kumbe anaishi: sababu ya imani yao mpya, wito wao n.k. wakaondoka saa ile wakarudi tena Yerusalemu. Kinachofuata ni ushuhuda. Wanaeleza tukio hilo kwa mitume.

Wanatuachia majukumu ya kuendelea kushududia ufufuko na ndicho tunachotakiwa kufanya sisi leo kama tunatambua lazima ya kuutangaza ufufuko. Tunaambiwa kuwa mitume/wafuasi; Wanapotangaza ufufuko wa Yesu, ni Yesu anaongea kupitia kwao. Wale wanaosikia na kuelewa hiyo furaha wanaipeleka kwa wengine. Sote tunaalikwa tufungue akili, mioyo na masikio yetu ili tusikie vizuri. Hilo Fumbo la Pasaka likitangazwa katika sadaka ya Ekaristi: katika kuumega na kuupokea mwili wake  na kumtambua. Hivyo sisi tunaompokea Bwana – ni kitu gani kipya na cha pekee kinachoonekana katika maisha yetu?

Tumsifu Yesu Kristo.

Na Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.