2017-04-27 09:45:00

Jubilei ya miaka 750 ya Kanisa kuu la Jimbo kuu la Monreale: Umoja!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 750 tangu kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Jimbo kuu la Monreale, nchini Italia, hapo tarehe 26 Aprili 2017 amewatumia ujumbe wa matashi mema waamini wote wa Jimbo kuu la Monreale na kuwataka kuhakikisha kwamba, maadhimisho haya yanaibua ndani mwao, umuhimu wa kujishikamanisha na Kristo Yesu sanjari na ushiriki wao katika maisha na utume wa Kanisa. Ujumbe huu ambao umeandikwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa niaba ya Baba Mtakatifu, unaiweka familia ya Mungu Jimbo kuu la Monreale chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mkombozi. Baba Mtakatifu Francisko anawapatia wote baraka zake za kitume!

Katika mahubiri yake, Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anasema, maadhimisho haya ni kumbu kumbu ya shukrani, furaha; ni wakati wa kusali na kuomba rehema na hekima ya kuendelea kuwajibika barabara katika maisha na utume wa Kanisa. Uzuri na utakatifu wa Kanisa hili unazungumzia Fumbo la Mungu na ukuu wake, changamoto kwa waamini kutambua na kuthamini uwepo endelevu wa Mungu katika hija ya maisha yao, kwani kizazi cha sasa kinataka kumwondoa Mungu katika maisha na vipaumbele vyao na matokeo yake ni kutumbukia katika utupu wa maisha ya kiroho.

Kanisa anasema Kardinali Bagnasco limepambwa kwa tafakari ya kina ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, Ibada kwa Bikira Maria na Watakatifu wa Mungu. Kwa haraka haraka, huu ni muhtasari wa Maandiko Matakatifu kwa ajili ya waamini wa kawaida; mwaliko kwa waamini wote kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, vinginevyo, wanaweza kujikuta wakiwa wametumbukia katika imani potofu na ushirikina. Mwenyezi Mungu anapaswa kupewa sifa na utukufu na mwanadamu kutakatifuzwa anaposhiriki katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Mwenyezi Mungu licha ya ukuu na utakatifu wake, lakini amejinyenyekesha na kujisadaka katika upendo, ili aweze kuwa karibu zaidi na waja wake!

Kumbe, ni wajibu wa waamini kumpenda na kumkimbilia Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yao ya kila siku, ili kukuza na kudumisha imani, inayomwilishwa katika matendo! Waamini wanakumbushwa kwamba wao ni sehemu ya Hekalu Takatifu la Mungu; mahali ambapo Mungu anakutana nao, ili kusali katika ukweli na haki kwani Mwenyezi Mungu ni utimilifu wa ukweli wote, uhuru na upendo kamili. Waamini wanapoingia kusali, wajikabidhi kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kutenda kwa njia yao, daima wakitambua kwamba, wao hapa duniani ni wasafiri ambao wanaelekea nyumbani kwa Baba wa milele kwa sababu wameumbwa kwa lengo hili la kukaa na Mwenyezi Mungu milele yote!

Kardinali Bagnasco anasema, ikiwa kama waamini watakuwa na mwelekeo kama huu, wataweza kuishi kwa amani, upendo na mshikamano wa kidugu kama ilivyokuwa kwa Jumuiya ya Wakristo wa mwanzo waliokita maisha yao katika sala, wakadumu katika kusikiliza mafundisho ya mitume; wakatambulikana kwa jamii kwa kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiasi cha kuwasaidia kuwa ni Ekaristi inayomegwa kwa ajili ya huduma msingi kwa jirani. Huu ni mwaliko wa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu: kiroho na kimwili.

Waamini waendelee kujitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano na Kanisa, huku wakionesha upendo kwa Kristo Yesu anayewasha moto wa mapendo katika nyoyo zao. Ni Kristo anayewawezesha waamini kupendana na kusameheana pale wanapokoseana: ni chachu ya ukarimu na upendo kwa jirani. Kardinali Bagnasco amemkumbuka na kumwombea pia Askofu mkuu Michele Pennis wa Jimbo kuu la Monreale anayeadhimisha kumbu kumbu ya miaka minne tangu alipokabidhiwa kuliongoza Jimbo hilo!

Katika salam zake za shukrani katika maadhimisho haya Askofu mkuu Michele Pennis anasema, Kanisa kuu ni Mama ya Makanisa yote, ni makao makuu ya Askofu ambaye amepewa dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Ni mahali ambapo Mafumbo ya Kanisa yanaadhimishwa na umoja wa Kanisa kushuhudiwa. Jubilei ya miaka 750 tangu kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Jimbo kuu la Monreale ni nafasi kwa waamini kutafakari Fumbo la Kanisa ambamo Kristo yumo na anatenda kazi zake. Hili ni Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume. Waamini wataendelea kulitafakari Fumbo hili kwa njia ya maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, kwa katekesi makini, tafakari ya Neno la Mungu na matendo ya huruma: kiroho na kimwili! Kwa upande wake, Rais Sergio Mattarella wa Italia anawapongeza na kuwatakia waamini wa Jimbo kuu la Monreale heri na baraka wanapoadhimisha Jubilei ya miaka 750 tangu Kanisa kuu  la Jimbo kuu la Monreale lilipotabarukiwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.