2017-04-26 14:34:00

Askofu Mkuu Antonio Filipazzi ateuliwa kuwa Balozi wa Vatican Nigeria


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Antonio Guido Filipazzi kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Nigeria. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Filipazzi alikuwa ni Balozi wa Vatican nchini Indonesia. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Antonio Guido Filipazzi alizaliwa kunako tarehe 8 Oktoba 1963 huko Melzo, Jimbo kuu la Milano, nchini Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi tarehe 10 Oktoba 1987 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre.

Baada ya masomo yake kwenye Chuo kikuu cha “Santa Croce” mjini Roma ambako alijipatia shahada ya uzamivu katika sheria za Kanisa, kunako mwaka 1992 alianza utume wake katika masuala ya kidiplomasia mjini Vatican na kutumwa kwenda Austria. Kati ya Mwaka 1995 - 1998 alikuwa kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Ujerumani. Kunako mwaka 1998 - 2003 alikuwa mjini Vatican katika Idara ya Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa.

Baadaye mwaka 2003 – 2011 alihamishiwa kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Tarehe 8 Januari 2011, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuliwa kuwa Askofu mkuu na kumweka wakfu tarehe 5 Februari 2011 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Tarehe 23 Machi 2011 akateuliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuwa Balozi wa Vatican nchini Indonesia. Tarehe 26 Aprili 2017 ameteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Nigeria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.