2017-04-25 14:24:00

WHO:Chanjo ya kuzuia Malaria itatolewa Ghana,Kenya na Malawi 2018


Tarehe 25 Aprili ya kila mwaka ni siku ya Maadhimisho ya Malaria duniani,ambapo kila taifa duniani linaalikwa kukabiliana na janga hili linalo endelea kuathiri kwa kiwango kikubwa duniani na hasa katika nchi zinazoendela. Shirika la Afya Ulimwenguni  katika  ofisi zilizopo   Afrika WHO/AFRO limetangaza Jumatatu 24 Aprili 2017, hatua muhimu za utekelezaji wa mpango wa chanjo ya Malaria (MVIP) unaoratibiwa na WHO. Ni mradi ambao utakuwa ni wa kwanza wa chanjo ya malaria duniani kupatikana katika maeneo ya nchi za Ghana , Kenya na Malawi  kuanzia mwaka 2018 ambao utagharimu dola karibu milioni 50 katika awamu ya kwanza.

Katika kilele cha maadhimisho ya ugojwa wa malaria duniani hata  nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, changamoto bado ni kubwa katika kuutokomeza ugonjwa huo kama ilivyo malengo ya Shirika la Afya duniani WHO ilivyo ifikapo mwaka 2030. Ripoti ya WHO kwa miaka miwili mfululizo 2015-2016 imebaini kwamba zaidi ya asilimia arobaini ya raia wa DRC wamefariki dunia kutokana na ugonjwa wa malaria. Na kwa mujibu wa ripoti hiyo, Congo na Nigeria zimekuwa nchi za kwanza duniani kuathiriwa na ugonjwa wa Malaria.Kwa njia hiyo ni Chanjo ya kwanza ya malaria duniani inayotarajiwa kufanyika kwa mara ya kwanza katika kiwango kikubwa kwa nchi za Afrika ambazo ni  Ghana, Kenya na Malawi kuanzia mwaka 2018.

Shirika la Afya Duniani WHO limesema chanjo hizo zinaweza kuokoa maisha ya wengi , huku malaria ikiendelea kupoteza maisha ya watu. Mpango huo ambao uko katika majaribio utahusisha zaidi ya watoto laki saba, lakini haijathibitika kwamba chanjo hiyo inaweza kufanya kazi kwa asilimia mia moja, japokuwa  wataalamu wa masuala ya afya wanasema chanjo hiyo ni hatua muhimu katika mapambano ya dunia dhidi ya ugonjwa wa malaria. 
Hii inafuata miongo kadhaa ya tafiti ya kutafuta ugonjwa ambao una ongoza kwa vifo vingi duniani. Chanjo hiyo mpya itakwenda sambamba na hatua nyengine za kujikinga kama vile neti, dawa za kufukuza mbu, na dawa za kukinga malaria. Chanjo ijulikanayo kama RTS,S inasemekana itaokoa maisha ya mamilioni ya watoto hususani Afrika ambako kunabeba mzigo mkubwa wa ugonjwa huo duniani. Mradi wa  majaribio ya chanjo utahusisha watoto wa umri kati ya miezi mitano na mwaka mmoja na nusu. 

Mwakilishi wa Shirika la Afya WHO Mary Hamel katika  hotuba yake  Jumatatu 24 Aprili 2017 amesema, "Tunatarajia chanjo hiyo kuanza katikati ya mwaka 2018 na tutatumia majaribio haya kuelewa vyema jinsi ya kuwafikia watoto na dozi hizi nne za chanjo katika maisha ya kawaida na kuona jinsi chanjo hiyo itakavyofanya kazi dhidi ya malaria na idadi ya vifo." Halikadhalika taarifa zinasema kuwa Chanjo hiyo ya RTS,S inaipa mafunzo kinga ya mwili ili iweze kusbulia viini vya Malaria ambavyo husambazwa na mbu. Mtu anastahili kupewa chanjo hiyo mara nne , mara moja kwa mwezi kwa muda wa miezi mitatu kabla ya kupata chanjo ya nne miezi 18 baadaye. Mafanikio haya yamepatikana kufuatia majaribio yaliyopata ufadhili mkubwa lakini haujulikani ikiwa majaribio hayo yanaweza kufanyika katika nchi ambapo huduma za afya ni duni. Hii ndiyo sababu WHO inaendesha majaribio hayo kati nchi tatu kubaini ikiwa mpango mzima wa utoaji chanjo hiyo unaweza kuanza.

Halikadhalika nchini Tanzania, Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu amewataka watanzania kwa pamoja kuungana kupambana na ugonjwa wa Malaria ili kusaidiana na serikali kutokomeza ugonjwa huo ambao husababisha vifo vya watu wengi nchini. Waziri Ummy ameyesema   hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kilele cha siku ya Maralia Duniani ambapo  ameawataka wananchi kushiriki kikamilifu ili kutokomeza ugonjwa huo.Waziri Ammy amesema “Msisitizo mkubwa wa Wizara yangu ni kwa wananchi na wadau wote kuona umuhimu na kutoa kipaumbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria kwa kuhakikisha matumizi sahihi ya mikakati iliyopo katika kuuthibiti ugonjwa huu, .“Iwapo mikakati hiyo itatekelezwa ipasavyo ni dhahiri kuwa maambukizi yataendelea kupungua kwa kiasi kikubwa na hatimaye kumaliza kabisa tatizo hili,” 

Na Sr Angela Rwezaula

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.