2017-04-24 08:26:00

Kardinali Attilio Nicora, "Jembe mahiri la kazi" amefariki dunia!


Baba Mtakatifu Francisko katika salam za rambi rambi alizomwandikia Dr. Carlo Nicora ameonesha kusikitishwa kwake na taarifa ya kifo cha Kardinali Attilio Nicora aliyekuwa na umri wa miaka 80 kilichotokea Jumamosi jioni tarehe 22 Aprili 2017 mjini Roma. Enzi ya uhai wake, aliwahi kuwa ni Rais wa Amana ya Kanisa, Mwakilishi wa Papa kwenye Makanisa Makuu ya Mtakatifu Francisko na Bikira Maria Malkia wa Malaika Jimboni Assisi na Rais wa Mamlaka ya Habari za Kifedha mjini Vatican, Aif.

Baba Mtakatifu anapenda kutuma salam za rambi rambi kwa wote walioguswa na msiba huu mzito wa kuondokewa na Mtumishi mwaminifu na mchapa kazi, ambaye nyuma yake anaacha kumbu kumbu ya daima ya mtu aliyejisadaka bila ya kujibakiza, akaonesha ujuzi na weledi mkubwa katika huduma kwa Kanisa na Jamii ya Italia katika ujumla wake. Alikuwa ni gwiji wa masuala ya sheria aliyeshiriki kikamilifu katika mapitio ya Mkataba wa Laterano kati ya Serikali ya Italia na Vatican. Akaonesha umahiri mkubwa katika masuala ya kiuchumi katika Kanisa Katoliki kiasi cha kuanzisha mchakato wa wananchi wa Italia kulichangia Kanisa Katoliki kwa njia ya kodi pamoja na kuwaenzi Wakleri katika maisha na utume wao!

Alikuwa ni kiongozi mahiri anasema Baba Mtakatifu Francisko na kwamba, amecha pengo kubwa kwa Kanisa. Kwa maombezi ya Mtakatifu Yohane Paulo II aliyemtuma kuwaongoza watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Verona na kumteuwa kuwa Kardinali na kwa maombezi ya Bikira Maria yamwezeshe kupata maisha ya uzima wa milele. Baba Mtakatifu anawapatia baraka zake za kitume wale wote wanaoomboleza msiba wa kardinali Attilio Nicora.

Itakumbukwa kwamba, Marehemu Kardinali Attilio Nicora alizaliwa tarehe 16 Machi 1937 huko Varese, Jimbo kuu la Milano, Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 27 Juni 1964 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Baada ya masomo na utume Jimbo kuu la Milano, kunako tarehe 16 Aprili 1977, Mwenyeheri Paulo VI akamteuwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Milano na kuwekwa wakfu tarehe 28 Mei 1977.

Tarehe 30 Juni 1992 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Verona na kung’atuka madarakani tarehe 18 Septemba 1997 ili kujisadaka zaidi kwa ajili ya shughuli za kitume mjini Vatican, kazi ambayo ameitekeleza kwa nafasi mbali mbali kuanzia mwaka 2002 hadi tarehe 30 Januari 2014 alipong’atuka na kuachia ngazi nyadhifa zote alizokuwa nazo mjini Vatican. Mtakatifu Yohane Paulo II alimteuwa kuwa Kardinali kunako mwaka 2003. Kwa hakika ni kiongozi aliyetumia vyema karama na vipaji vyake kwa ajili ya kuliendeleza Kanisa la Kristo! Atakumbukwa na wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.