2017-04-19 11:00:00

Jubilei ya miaka 300 tangu Bikira Maria alipotokea Aparecida!


Msemaji mkuu wa Vatican Dr. Greg Burke amethibitisha kwamba, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia barua binafsi Rais Michel Miguel Elias Temer wa Brazil ambaye ameingia madarakani tangu tarehe 31 Agosti 2016. Barua hii haikuweza kuchapishwa na kuwekwa hadharani kwani ni barua yenye masuala binafsi zaidi. Vatican inafafanua kwamba barua hii ni sehemu ya majibu ambayo Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia Rais Temer katika barua yake iliyokuwa inamwomba Baba Mtakatifu Francisko kutembelea Brazil kwa mwaka 2017 kama sehemu ya maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 300 tangu Bikira Maria alipotokea huko Aparecida nchini Brazil.

Katika barua hii, Baba Mtakatifu anasema, angependa kutembelea tena Brazil ili kuungana na familia ya Mungu nchini humo ili kumwimbia utenzi wa sifa na shukrani kwa Bikira Maria kutokea huko Aparecida na kusaidia kwa kiasi kikubwa kujenga na kuimarisha Ibada kwa Bikira Maria, lakini kutokana na majukumu kadhaa yaliyoyoko mbele yake, itashindikana kuweza kuunganika na familia ya Mungu nchini Brazil kwa ajili ya tukio hili la kihistoria. Katika barua hii, Rais Temer amemwelezea Baba Mtakatifu Francisko kuhusu changamoto anazokabiliana nazo katika masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi nchini mwake na jinsi anavyojitahidi kuzivalia njuga changamoto hizi. Kwa upande wake, Baba Mtakatifu Francisko anamtia shime Rais Temer kujizatiti zaidi katika mchakato wa kuwawezesha maskini, ili waweze kupambana vyema na mazingira na hatimaye, kuboresha hali ya maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.