2017-04-15 14:48:00

Ujumbe wa Pasaka 2017 kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania


Ndugu waamini wenzangu katika safari ya utakaso, kwa shangwe na furaha zote napenda kuwatakieni baraka na neema za Kristo mfufufuka. Kwetu sisi tunaomwamini Kristo, leo zaidi ya siku zote katika maisha yetu tutaimba “Alleluya Kuu” alama ya furaha kwamba giza la dhambi lililokuwa limetawala mioyo yetu limeondolewa kwa njia ya fumbo la ufufuko wa Kristo. Leo ndio kilele cha safari yetu ya siku 40 za tafakari juu ya furaha  ya Injili na Uumbaji. Katika tafakari ya zawadi ya Injili y.n habari njema tumefunuliwa namna Mungu  alivyoumba ulimwengu na mwishowe mwanadamu kama mwenza wake ktk kuendeleza, kuutunza na kutumia yvote kwa utukufu wake Mungu (Mwz. 1:28-30). Mwanadamu aliyepewa vyote vilivyoumbwa mwishowe kwa uhuru wake alitaka kuwa sawa na Mungu na hivyo akajikuta mkiwa na mpweke. Hakuweza tena kuona uso wa Mungu. Madhara ya dhambi yake yaligusa vyote alivyomkabidhi muumba na hivyo uhasilia wa furaha yao ukabadilika. Mungu ambaye kila wakati ni mwenye huruma hakupenda mwanadamu abakie kwenye giza la mauti. Alimtuma nafsi yake ya pili kuinua na kurudisha hali ya asili. Huyu ndiye Kristo mwahidiwa. Maadhimisho ya Pasaka ndiyo kilele cha ukombozi huo, ni katika ufufuko wa Kristo vyote vimeumbwa upya, na ni katika ufufuko vyote vimerudishiwa hadhi ya kuuona tena uso wa Mungu.

Nguvu za Ufufuko wa Kristo:

Kwa ufufuko wa Kristo dhambi zimedhoofishwa na kusamehewa,  makosa ya zamani yamefutwa, walioanguka wameinuliwa, na wenye uzuni wamejazwa furaha tena. Sote hatuna budi kuimba Alelluya Kuu, iliyo tangazo la furaha na uhuru wetu. Kristo Amefufuka kweli – Alelluya, Alelluya, Alelluya! Leo na siku zote, Kristo aliyehukumiwa kuwa mwalifu na mtu asiye na nidhamu kwa tamaduni za mababu ameshinda giza la mauti kwa njia ya ufufuko. Msalabani alikotundikwa ilidhaniwa na watesi wake kwamba ni mwisho wa mafundisho na nguvu zake, lakini, lo, pamoja na ulinzi mkubwa kaburini, Kristo amefufuka na yupo hai na wafuasi wake. Ufufuko wa Kristo ni ushindi dhidi ya uongo, uonevu na ukatili. Ufufuko wa Kristo leo na siku zote ni kielelezo ya kwamba kamwe maovu ya ulimwengu hayatashinda upendo na wema wa Mungu. Kristo kwa ufufuko wake ameunganyisha yale ya duniani na Mbinguni, kwa ufufuko ametujengea matumaini mapya ya kwamba sisi si watu wa giza ila watu wa mwanga. Kielelezo chake kikiwa Mshumaa wa Pasaka ulio alama na mwanga wa Kristu kwetu. Ufufuko wa Kristo unarudisha uhasilia wa furaha ya mwanadamu, unatuasa tulinde viumbe na tuheshimu vyote alivyotukabidhi Muumba. Kama dhambi ilivyoathiri vyote alivyoumba Mungu, ufufuko wa Kristo unarudisha hadhi ya viumbe vyote kupitia kwa mwanadamu.

Ufufuko wa Kristo Nguvu ya Wanyonge na Maskini:

Kwa njia ya kifo Msalabani Kristo aliondoa giza la dhambi, na kwa njia ya ufufuko wake ameleta mwanga wa kuona ukweli na hivyo mwaliko wa kutenda kuendana na ukweli huo. Ndugu zangu, furaha za Pasaka ambazo kilele chake ni Ufufuko hazitakuwa za kweli kama sisi sote hatutashughulika kuondoa giza la maovu katika jamii. Taifa letu sasa linaishi kipindi kigumu kilichokubikwa na woga mwingi unaosababisha kutowajibika kwa viongozi wengi kwa sababu za ubinafsi, na uchoyo wa kulinda nafasi zao. Mimi ninaamini kabisa kwamba kazi kubwa ya viongozi ni kulinda haki na amani ya raia na hasa katika kutatua shida na kero zao. Viongozi wengi walipewa nafasi hizi kwa sababu walionekana wana elimu uwezo, hekima na ueleji wa kufanya hivyo. Tunachoshuhudia sasa ni woga wa kutenda na hivyo kubaki kuimba wimbo wa kiongozi wa juu hata kama una kasoro. Mfano mzuri ni ukame uliosababisha kutokuwa na chakula cha kutosha sehemu nyingi za nchi yetu. Pamoja ya kwamba njaa ilikuwa kubwa sehemu mbalimbali za nchi, ni wachache sana waliothubutu kusema sasa ni janga la taifa hivyo serekali iwajibike. Hili halikufanyika kwa sababu ati mkuu wa nchi hajatamka kwamba ni janga, wakati huo huo wanyama wanakufa na raia wengi wanateseka. Kiongozi yeyote anaposhindwa kutimiza wajibu wake husababisha mateso kwa raia na hili ni  kunyima raia haki zao. Ujumbe wa Ufufuko wa Kristo kwetu sote na hasa viongozi ni kuwajibika zaidi na kutenda yale Kristo aliyofunua katika ufufuko wake, yaani ukweli, haki na uadilifu wa kutunza vizuri viumbe tulivyokabidhiwa.    

Ufufuko ni Ujumbe wa matumaini na furaha kwa wote:

Ufufuko wa Kristo ulio kielelezo cha ushindi dhidi ya giza la dhambi ni kwa wanadamu na viume vyote. Wakati watanzania wakitarajia mengi mazuri kutoka kwa serekali zao ushirikiano wa kufichua wezi wa mali za umma umekuwa mdogo na lawama kwa mkuu wa nchi zimekuwa nyingi kiasi cha kukatisha tamaa. Kilio cha watanzania wengi kwa miaka mingi ni kuona serekali ina nia thabiti ya kupigana na janga la rushwa, uwajibikaji wa viongozi, madaya ya kulevya, wizi, na uuzaji wa rasilimali za nchi usiokuwa na tija kwa taifa. Wakati haya yakishughulikiwa viongozi na raia wengi wamebaki kuwa watazamaji na wasioridhika na yanayofanyika. Ni lazima tuelewe kwamba hakuna mabadiliko ya kweli yasiyodai Msalaba, kwa kujinyima na utayari wakuwa mashahidi kwa ajili ya wengi. Bila mateso ya Kristo Msalabani hakuna Ufufuko. Tukubali kwamba yanayofanyika ktk kupunguza kero za watanzania nia ni njema ila kuwe na mfumo yakinifu na uzingatiaji wa sheria zilizopo. Kusipokuwa na mfumo yakinifu na endelevu mazuri yote yanayofanyika na serekali ya awamu ya tano yatafutwa haraka sana baada ya uongozi wao.

Ufufuko wa Kristo Kero kwa Viongozi wasiowajibika:

Ndugu zangu Kristo aliyetundikwa Msalabani na kufa, hakuwa na kosa lolote, ila ni kwa sababu alikuwa kero kwa viongozi na aliyesumbua dhamiri za wengi waliotaka kubaki madarkani wakati wote. Kristo alielimisha watu juu ya haki zao, aliwaasa viongozi, alishungulikia waliogandamizwa na sheria zilizolinda wachache na kuwaacha wengi katika lindi la mateso. Ufufuko wa Kristo umekuwa aibu kubwa kwa viongozi wanaochelea kufanya maamuzi muhimu, kama mfalme Pilato alivyoshindwa kumwachia huru asiyekuwa na hatia kwa sababu ya kutafuta umaarufu bila kuwajibika. Ufufuko wa Kristo ni fundisho kwetu sisi viongozi wa ngazi zote kuwajibika zaidi. Ufufuko ni kiilelezo kwamba mwisho wa mateso na mahangaiko ni furaha. Waisraeli waliteseka  utumwani miaka 400, mwishowe walikuwa huru na kuona nchi ya ahadi kwa sababu walikubali mabadiliko ktk maisha yao. Nasi hatuna budi kukubali mabadiliko kwa kupokea yale mazuri yanayofanika kwa kujua kwamba mazuri yanadai kujinyima na kujikatalia kwingi.

Kamwe hatutaweza kuona Tanzania tunayotamani ya Haki na Amani inayuoleta maendeleo bila sisi wote kushiriki.  Ndugu zangu, ni takribani muda wa mwaka moja na nusu hivi, tangu serekali ya awamu ya tano kuwa madarakani. Serekali hii ilitarajiwa sana kuwa serekali ya mabadiliko na matumaini kwa watanzania.  Ndiyo ni mapema mno kutoa tathimini, lakini kwa kusoma alama na matukio machache, tunaweza kusema, kuna mengi ya kurekebesha ili maendeleo tuliyosubiria  yafikiwe. Kamwe nchi haiendeshwi na mtu mmoja, ni kwa ushirikiano na viongozi wote na raia. Dhana ya kusubiria Raisi wa nchi aseme ndiyo lifanyike, hakika halitatufikisha tunakotamani. Kutenda kwa woga ni dhana mbovu na isiyo na tija kwa wananchi-muundo huu wakutenda kwa woga huishia kuonea wengine wasio na hatia kwa sababu za kutaka kumfurahisha aliye juu! Kristo alitenda kwa haki ndiyo maana leo ni mshindi. Tunawaasa viongozi na mahakama zetu watumie sheria zilizopo, uwezo na weledi wao na kutenda kwa haki. Ukitumbuliwa kwa sababu umetenda kwa haki umma utakutetea.

Sababu kuu za Kristo kufa Msalabani ni kumaliza kero za watu; swali la mikopo kwa wanafunzi limekuwa ni anasa na lenye ubaguzi usiokuwa na msingi. Kuweka kigezo kwamba mwanafunzi aliyesoma shule za binafsi asipewe mkopo, huu ni ubaguzi kwa sababu mkopo ni deni na kila anayekopa lazima alipe. Tunaomba sera hii irekebishwe la sivyo tutaumiza wengi wenye sababu msingi za kujiendeleza. Mkopo mahali popote si msaada ila ni haki ya mlipa kodi na masharti yake lazima ulipwe.

Swali la ajira nalo limekuwa kero katika nyanja nyingi, vijana wengi wasomi hawana ajira, huku kukiwa na mapengo makubwa ya wahudumu katika taasisi nyeti kama vile elimu na afya. Shule na hospitali nyingi hazina wahudumu wa kutosha, lakini bado kuna maelfu ya waalimu na madaktari wanaosubiria ajira. Tunaomba bunge la bajeti ya serekali mwaka huu litenge bajeti ya kutosha.  Serikali pia ibuni mbinu ya kutafuta ajira kwa wahitimu wetu na hata ikiwezekana nje ya nchi kwa muda. Ndugu zangu, tutakuwa tumejidanganya kama, Alelluya kuu tunayoimba leo na siku zote, haitaleta furaha na  mwanga kwa kero hizi. Kristo tunayemwadhimisha angerudi kimwili katika mazingira yetu, vitu ambavyo angeshughulikia sana ni kero za jamii kama ukosaji wa ajira, umaskini wa kukosa mahitaji muhimu, madaya ya kulevya yanayopunguza nguvu kazi na  kutowajibika kwa wengi. Kristo aliyefufuka hawezi kukemea haya kwa mdomo wake, ila anaagiza sisi tuyashughulikie kwa nguvu na ueleji wetu  kuwafikia wenye shida. Naomba sote tuwe alama ya matumaini na furaha kwa wote wanaoteseka na kamwe tusikubali kusherehekea siku ya leo wenyewe-Tujaribu sana kuwapelekea furaha za Kristu Mfufuka  majirani zetu.   

Nawatakieni nyote neema na baraka za Kristo Mfufuka - Alleluya Alleluya Alluluya –Amina!

Askofu, Augustine Shao, C.S.Sp.

Jimbo Katoliki la Zanzibar.








All the contents on this site are copyrighted ©.