2017-04-11 10:22:00

Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani Panama, 2019! Vijana wamewasha moto!


Maadhimisho ya Siku ya 32 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2017 Jimbo kuu la Roma yamepambwa kwa uwepo na ushiriki wa ujumbe wa vijana 300 kutoka katika nchi 103 na vyama 44 vya kitume vinavyotekeleza dhamana yake miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Wajumbe hawa wamefanya tathmini ya kina mintarafu maadhimisho ya Siku ya 31 ya Vijana Duniani, Jimbo kuu la Cracovia, Poland ili kuweka sera, mipango na mikakati ya maadhimisho ya Siku ya 34 ya Vijana Duniani itakayoadhimishwa nchini Panama kunako mwaka 2019.

Kongamano hili liliandaliwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kwa kushirikiana na Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu. Vijana hawa wameshiriki pia katika kesha la Siku ya Vijana Kijimbo kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko Jimbo kuu la Roma na hatimaye, Jumapili ya Matawi kuandamana na Baba Mtakatifu Francisko katika viunga vya Vatican na kuhitimishwa kwa Ibada ya Misa Takatifu. Vijana wanakumbushwa kwamba wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Hii ni changamoto inayotolewa mkazo na Askofu mkuu Josè Domingo Ulloa Mendieta wa Jimbo kuu la Panama, Jumatatu, tarehe 10 Aprili 2017 alipokuwa anawasilisha mpango mkakati w Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani itakayoadhimishwa kuanzia tarehe 22 - 27 Januari 2019 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Anasema, idadi kubwa ya familia ya Mungu Amerika ya Kusini inaundwa na vijana wa kizazi kipya, lakini kwa bahati mbaya sana, wengi wao wanakabiliwa na ukosefu wa fursa za ajira, hawa ndio ambao Kanisa linataka kuwaonjesha huruma ya Mungu kwa njia ya sera na mikakati makini ya utume wa vijana.

Panama hata katika umaskini wake ni nchi ambayo imebahatika kuwa na msingi thabiti wa utume wa vijana kitaifa. Itakumbukwa kwamba, hili ni Jimbo la kwanza kabisa la Kanisa Katoliki kuundwa Barani Amerika, kunako tarehe 9 Septemba 1513, chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria wa Antiqua. Panama inataka kuwaonesha walimwengu uzuri, uhai wa imani na furaha ya maisha na utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wanaotoka katika makabila na tamaduni mbali mbali. Wanataka kuwashirikisha vijana umuhimu wa mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene ili kujenga mshikamano na mafungamano ya kijamii yanayojikita katika misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, tofauti zao za kiimani, kiitikadi, na kidini ni utajiri mkubwa unaopaswa kuwaunganisha kama ndugu wamoja!

Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa anachukua nafasi ya pekee kabisa katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji miongoni mwa vijana. Hii ni kutokana na sababu kwamba, familia ya Mungu Amerika ya Kusini ina Ibada kubwa sana kwa Bikira Maria. Hapa vijana wanakumbushwa kwamba, wanapaswa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu za: kijiografia na mambo msingi katika maisha ya watu, ili wote hawa waweze kuoneshwa njia inayowasindikiza kwa Kristo Yesu, rafiki wa vijana. Bikira Maria ni nyota ya uinjilishaji, mwaliko kwa familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia ni kutubu na kumwongokea Mungu; kwa kuliwezesha Kanisa kuwa ni chemchemi ya ukarimu, huruma na upendo wa Mungu kwa watu wote. Kanisa nchini Panama liko tayari kumpokea na kumkirimia Khalifa wa Mtakatifu Petro ili aweze kuwaimarisha ndugu zake katika imani!

Kwa upande wake, Kardinali Josè Luis Lacunza ambaye uwepo na ushiriki wake umekuwa na mchango mkubwa katika kuibua na kupanga mbinu mkakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 nchini Panama anasema, Kanisa linataka kujielekeza zaidi kwa ajili ya huduma kwa maskini na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi!Familia ya Mungu nchini Panama wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani inatarajia kutoa hifadhi, chakula na malazi kwa vijana laki mbili kutoka sehemu mbali mbali za dunia ili kuonja wema, upendo na ukarimu wa familia huko Panama. Hii ni changamoto kubwa kwa nchi kama Panama. Nchi za Honduras na Sal Salvador zitasaidia kuwakarimu vijana siku chache kabla ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Masuala yote kuhusu nyaraka za kwenda Panama, usafiri na mambo msingi yataendeelea kuratibiwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kama ilivyokuwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, Jimbo kuu la Cracovia, nchini Poland. Serikali ya Panama inasema, inaendelea kujipanga vyema ili kufanikisha tukio hili la kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.