2017-04-10 08:54:00

Papa Francisko asikitishwa na mashambulizi ya kigaidi nchini Misri


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuadhimisha Jumapili ya Matawi tarehe 9 Aprili 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kuhudhuriwa na bahari ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana alionesha masikitiko yake makuu kutoka na mashambulizi mawili ya kigaidi yaliyotokea nchini Misri na kusababisha watu zaidi ya 45 kupoteza maisha na wengine wengi kupata majeraha makubwa.

Mashambulizi haya yamefanyika kwenye Kanisa la Kikopkik huko Cairo na Alexandria, nchini Misri ambako idadi ya waamini wa Kanisa la Kikoptik inakadiriwa kuwa walau ni asilimia 10% ya idadi ya wananchi wote wa Misri ambao kwa sasa wanakadiriwa kuwa ni milioni 85. Taarifa zinaonesha kwamba, bomu limelipuka muda mfupi tu baada ya Papa Tawadros II, Mkuu wa Kanisa la Kikopitik nchini Misri kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la Mtakatifu Marko, huko Alexandria.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana ametumia fursa hii kuonesha uwepo na mshikamano wake wa dhati na Papa Tawadros II, Kanisa la Kikoptik pamoja na familia nzima ya watu wa Mungu nchini Misri. Baba Mtakatifu ametuma salam zake zar ambi rambi kwa wale wote walioguswa na msiba huu mzito. Amemwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuongoa nyoyo za watu wanaojenga hofu na utamaduni wa kifo pamoja na wale wote wanaotengeneza na kufanya biashara ya silaha duniani. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kufanya hija ya kitume nchini Misri kuanzia tarehe 28- 29 Aprili 2017. Baba Mtakatifu wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana aliwakimbuka na kuwaombea watu waliofariki dunia kutokana na shambulizi la kigaidi lililofanyika Siku ya Ijumaa, tarehe 7 Aprili 2017 huko Stockholm, Sweden na kusababisha watu wanne kupoteza maisha na wengine 15 kupata majeraha makubwa. Mtu anayeshutumiwa kwa shambulio hili tayari amekwisha kukamatwa na vyombo vya ulinzi na usalama.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.