2017-04-08 15:05:00

Maadhimisho ya Juma kuu kwa Vijana wa Mexico


Maadhimisho ya Juma Takatifu au Juma kuu kama ambavyo wengi wamezoea kusikia ambamo Kanisa linafanya kumbu kumbu ya Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni juma muhimu sana kwa utume wa vijana nchini Mexico! Huu ni wakati ambapo Mama Kanisa anawaalika vijana kutoka katika ubinafsi wao, tayari kuanza safari ya kuelekea kwenye mambo msingi ya kiimani, kiutu na kitamaduni. Ni wakati muafaka wa kufanya mang’amuzi na maamuzi magumu katika maisha kwani ni nyakati kama hizi, baadhi ya vijana wamekata shauri ya kuwa ni: mapadre, watawa au watu wa familia.

Vijana wanatoka katika maeneo salama ya maisha, hifadhi na tunza makini ya familia zao kwa kujiaminisha kwa tunza na usalama wa Mama Kanisa kwa watoto wake, wanaosafiri huku bondeni kwenye machozi! Ni wakati mahususi kwa vijana kuweza kukabiliana na ugumupamoja na changamoto za maisha, ili hatimaye kujenga utashi na dhamiri nyofu, ili kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Hivi ndivyo anavyosimulia Padre Josè Suàrez, Mkuu wa Jumuiya ya Wayesuit huko Parras, Kijiji kinachowapokea na kuwakirimia vijana wa Mexico wakati wa maadhimisho ya Juma kuu kila mwaka! Anasema, kijijini hapo, vijana wanapata nafasi ya kushirikisha mawazo, maono na mang’amuzi yao katika maisha; ni wakati wa kuonesha wema, upendo na ukarimu kwa kutambua kwamba, kila mmoja wao ni zawadi muhimu sana kwa jirani yake kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa mwaka 2017.

Juma kuu kwa vijana wa Mexico ni muda wa sala na tafakari ya kina; muda wa kubadilishana mawazo kwa kuwatembelea wanakijiji, ili kuonja ile furaha ya Injili inayofumbatwa katika mchakato wa ujenzi wa madaraja ya watu kukutana na kusaidiana katika maisha, kwani mwandamu ni kiumbe jamii! Vijana wakati huu wanaonja na kuwaonjesha wengine huruma na upendo wa Mungu katika hija ya maisha yao ya kila siku! Maadhimisho ya Matukio makuu ya Juma kuu yaani: Jumapili ya Matawi, Alhamisi Kuu, Ijumaa na Mkesha wa Pasaka yanawazamisha vijana katika Fumbo la Pasaka wanalolimwilisha katika uhalisia wa maisha na mazingira wanamoishi, ili kujenga na kudumisha urafiki, upendo na mshikamano na maskini ambao kimsingi ni amana na utajiri wa Kanisa na walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.