2017-04-07 13:30:00

Vijana ninyi ni majembe mazito ya Kanisa!


Mtakatifu Yohane Paulo II miaka thelathini na mbili iliyopita alianzisha mchakato wa Kanisa kuandamana na vijana katika maisha yao kwa kuanzisha Siku ya Vijana Duniani, changamoto inayoendelezwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa kuitisha Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana itakayoadhimishwa mjini Vatican, mwezi Oktoba 2018. Hii ni nafasi kwa vijana wa kizazi kipya kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, wito uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika barua ya mwaliko kwa vijana ili kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana. Vijana wanapaswa kuwa kweli ni wamissionari kwa vijana wenzao kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Haya ni kati ya mambo mazito ambayo viongozi wa Kanisa wameyazungumza siku ya Alhamisi, 6 Aprili 2017 kwa wajumbe 300 kutoka katika nchi 103 na vyama 44 vya kitume miongoni mwa vijana wa kizazi kipya wanaoshiriki katika kongamano la kimataifa ili kufanya tathmini ya kina mintarafu maadhimisho ya Siku ya 31 ya Vijana Duniani, Jimbo kuu la Cracovia, Poland tayari kuweka sera, mipango na mikakati ya maadhimisho ya Siku ya 34 ya Vijana Duniani itakayoadhimishwa nchini Panama kunako mwaka 2019. Kongamano hili limeandaliwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kwa kushirikiana na Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu.

Vijana nao wameshirikisha changamoto na mang’amuzi yao kwa kuwataka viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, Hati ya Kutendea Kazi inaandaliwa kiasi kwamba, itaweza kuwafikia vijana wengi zaidi na kama inawezekana basi, iwekwe pia katika mitandao ya kijamii, mahali ambako kuna idadi kubwa ya vijana wa kizazi kipya. Makanisa mahalia, yahakikishe kwamba, kweli vijana wanashirikishwa kikamilifu katika maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, ili kweli mawazo yao yaweze kuwasilishwa kwa Mababa wa Sinodi.

Vijana wamegusia pia changamoto za maisha na imani katika ujumla wake; changamoto zinazohitaji sera na mikakati makini kwa ajili ya utume kwa vijana! Changamoto kubwa ni umaskini, ukosefu wa ajira, vurugu na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yanayowatumbukiza vijana wengi katika malimwengu, kiasi cha kuzipatia kisogo tunu msingi za maisha ya: kroho, kiutu, kimaadili na kitamaduni!

Professa Alessandro Rosina, Jaalimu kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore cha Milano” amepembua kuhusu takwimu za idadi ya vijana sehemu mbali mbali za dunia na changamoto zake. Changamoto za vijana zinatofautiana kutoka sehemu moja hadi nyingine; kumbe, Kanisa halina budi kujizatiti zaidi kwa kusoma alama za nyakati ili kuwasaidia vijana kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya ujana, kwani ujana mali, fainali uzeeni! Vijana wasibweteke, watambue kwamba, wao ni “majembe ya nguvu” ulimwenguni! Wajumbe kwa wakati huu wamegawanyika katika makundi kufuatana na lugha ili kurahisisha mawasiliano zaidi pamoja na kucheua changamoto zilizotolewa na viongozi wa Kanisa katika maisha na utume wa vijana, tayari kuanzisha safari ya kukutana na kuambatana na Yesu kama alivyofanya Mtume Yohane!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.