2017-04-07 14:18:00

Jubilei ya Miaka 150 ya Chama cha Vijana Katoliki Italia!


Chama cha Kitume cha Vijana Wakatoliki Italia, kinaadhimisha Jubilei ya miaka 150 tangu kuanzishwa kwake na kilele cha maadhimisho haya ni hapo tarehe 27 Aprili 2017 kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko. Maadhimisho haya yatawashirikisha pia wajumbe wa Kimataifa kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwa muda wa siku tatu na hatimaye, Jumapili tarehe 30 Aprili 2017 watakusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ili kuunganika na Baba Mtakatifu kwa Sala ya Malkia wa mbingu. 

Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 150 ya Chama cha Kitume cha Vijana Wakatoliki Italia yanaongozwa na kauli mbiu “Utume wa Vijana Wakatoliki kwa ajili pamoja na wote”. Shirikisho la Vyama vya Utume wa Vijana Kimataifa, (FIAC) ndilo lililopewa dhamana ya kuandaa na kuratubu maadhimisho. Wajumbe watapata pia nafasi ya kuchagua viongozi watakaowaonesha dira na mwongozo baada ya maadhimisho ya miaka 150. Wajumbe 50 kutoka katika nchi wanachama na watazamaji 40 watakuwa na dhamana ya kuwachagua viongozi wapya.

Huu utakuwa ni mkutano wa kumi na sita kitaifa kufanyika tangu kuanzishwa kwa Chama cha Kitume cha Vijana Wakatoliki Italia miaka 150 iliyopita. Taarifa inaonesha kwamba, jumla ya wajumbe 1200 wanatarajiwa kushiriki katika mkutano huu ili kuwachagua wajumbe watakaounda uongozi wa kitaifa. Hili ni tukio muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa kwa vijana hasa wakati huu wa maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana sanjari na maandalizi ya Siku ya 34 ya Vijana Duniani itakayoadhimishwa nchini Panama kunako mwaka 2019. Kanisa linataka kuweza zaidi miongoni mwa vijana wa kizazi kipya ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda kwa Kristo Yesu na Kanisa lake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.