2017-04-06 14:04:00

Yesu Bwana, Masiha na Mfalme ni kielelezo cha unyenyekevu hadi kifo!


Dominika ya Matawi hutuingiza katika Juma kuu, juma ambalo linabeba kiini cha imani yetu ya kikristo. Ni juma ambalo huitimishwa kwa maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Dhamira kuu ya Dominika hii ni adhimisho la Bwana kuingia kwa shangwe Yerusalemu, mji ambao ni kiini cha imani ya Kiyahudi na kitovu cha shughuli zote za kidini. Kristo anaingia katika mji huu akinuia kuikamilisha ile kazi ambayo kwayo amekuja duniani, kazi ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi.

Adhimisho la Dominika hii huanza kwa mapokezi ya shangwe: “Hosana Mwana wa Daudi; ndiye mbarikiwa, yeye ajaye kwa jina la Bwana, Mfalme wa Israeli; Hosana juu mbinguni”. Wayahudi wa Yerusalemu wanajitokeza kumpokea huyu mfalme anayekuja akiwa amepanda punda. Huu ni ufunuo wa namna ufalme wake ulipaswa kueleweka. Mfalme anayeingia huku amepamda ya Punda anaonekana kuwa ni dhaifu na ameshindwa. Ni vigumu kueleweka maana yake katika hali ya kawaida. Mfalme alipaswa kuonesha nguvu na fahari zake. Alitarajiwa kuingia akiwa amepanda farasi maridadi kabisa na wenye kuonesha ufahari wake.

Hapa tunauona muunganiko wa namna alivyoingia duniani na namna hii anapoingia Yesuralemu. Wakati wa kuzaliwa alizaliwa katika mahali duni, katika zizi la kulishia ng’ombe na leo hii anapoingia Yerusalemu kwa ajili ya kutushirikisha utukufu wake na kutufanya kuzaliwa katika Yeye anaingia katika hali hii inayopokeleka kama hali ya unyonge sana. Haya yote yamekwisha aguliwa kama anavyodokeza mwinjili Matayo anaponukuu maandiko ya Nabii Zekaria akisema: “Mwambieni binti Sayuni, Tazama mfalme wako anakuja kwako, mpole naye amepanda punda, na mwana punda, mtoto wa punda” (Rej Zek 9:9).

Haiba ya unyenyekevu ndiyo inayotawala katika ufalme wake. Haiba hii ndiyo inayomwezesha kujivika uvumilivu na kujitwika mabaya yetu yote na kuyagongomelea juu ya msalaba. Nabii Isaya anaelezea vizuri haiba hiyo na anadokeza kwamba chanzo chake ni Mungu mwenyewe. “Bwana Mungu amenipa ulimi wa hao wafundishwao... amenizibua sikio langu wala sikuwa mkaidi… naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang’oao ndevu mashavu yangu; sikuuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate”. Katika hali hii ya unyenyekevu tunafundishwa kujitegemeza kwa Mungu na kutokusikiliza sauti nyingine.

Huu ni mwaliko mahsusi kwa juma hili kuu ambalo linatufikisha katika kilele cha maisha ya kipasaka ambayo yamefumbatwa katika hali ya mwanadamu kumpatia Mungu utukufu wote. Chanzo cha anguko la mwanadamu ni kiburi. Katika kiburi chake mwanadamu alijitenga na sauti ya Mungu na kujivunia uwezo wake. Dhambi imemtenga mwanadamu na Mungu kwa sababu amepoteza paji la unyenyekevu. Hivyo namna hii ya unyenyekevu anayoingia nayo Kristo katika mji wa Yerusalemu ni kielelezo mahsusi kwetu cha namna tunavyopaswa kujiweka mbele ya Mungu ili kuyapokea maisha ya kipasaka, yaani ukombozi kutoka katika dhambi.

Kilele cha unyenyekevu huo ni mauti ya msalaba. “Kristo alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina”. Msalaba ambao ni ishara ya juu kabisa ya dharau na aibu kwa jamii ya Kiyahudi wakati wa Kristo inakuwa ishara ya wokovu wetu, mahali ambapo Kristo anatufundisha kunyenyekea na kuwa mtii kwa mapenzi ya Baba yake wa mbinguni katika hali zote hata kama utadaiwa uhai wako. Utii wa Kristo unatufunulia namna njema ambayo tunapaswa kuuonesha uhuru wetu wa kibinadamu, yaani kutenda katika kweli, kadiri ya mipango na miongozo ya muumba wetu.

Tunapoianza safari hii ya juma kuu kwa shangwe tunaalikwa kuzielekeza shangwe hizo katika muktadha huo, yaani kuwa tayari kumsindikiza Kristo katika safari yake hii ambayo anaonesha unyenyekevu wake na kulikaribisha neno la Mungu lime ndani mwake na mwisho kuyaonesha matunda yake katika kifo cha msalabani. Historia ya Mateso ya Kristo kadiri ya Mwinjili Matayo inayosomwa katika liturujia ya mwaka huu inaonesha jinsi anavyorandana na mtumishi anayeaguliwa na Nabii Isaya katika njia yake ya mateso hadi kifo chake juu ya msalaba. Alidhiakiwa, alitukanwa na hata wale waliokuwa karibu yake walimkana ila yeye alibaki mkimya na mnyenyekevu kwa ajili ya kuyatimiza mapenzi ya Mungu.

Mvutano wa ndani wa dhambi ya binadamu na utukufu wa Mungu unaonekana wazi katika sala yake anapokuwa Gethsemane: “Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe”. Mwili wake unaonesha udhaifu na shahuku ya kuyakwepa mateso. Katika hali hiyo ndipo anapotupatia fundisho kuu ambalo kwalo linatufikisha katika wokovu. Pamoja na kujisikia kutokuweza, kujiona yu dhaifu lakini ndani kabisa katika dhamiri yake anautanguliza mpango wa Mungu. Huu ni uthibitisho wa hali ya juu kabisa wa unyenyekevu. Ni dhahiri kwamba Kristo alikuwa na uwezo binafsi wa kuepuka hali ile ya mateso iliyokuwa inamkabili, lakini akiwa ameunganika na Mungu katika sala anaisikiliza na kuipatia kipao mbele sauti ya Baba.

Safari nzima ya Kwaresima ambayo tunaelekea katika kilele chake imekufunulia kilema cha maisha, imekutaadharisha na hatari fulani kutokana na mwenendo wako. Mara nyingi tunavutika na hatutamani kutoka huko. Tunaisikia sauti ya Mungu lakini hatuipatii kaipao mbele. Hamu zetu na kimwili, vipaji na uwezo wetu hutuadaa kupenda kubaki katika vilema hivyo na ambavyo mara nyingi hutupatia faraja za kimwili na zinazoshikika. Mwaliko wa Mungu wa kuifuta njia yake hutuletea hali ya kuhisi kupokonywa utamu huo na hivyo tunauwekea ukinzani.

Mtakatifu Agustino aliahirisha sana safari yake ya wokovu lakini ikafika wakati akamwambia Mungu sasa inatosha naanza sasa kukufuata. Ni vema nasi tukasema kwa Mungu kwamba sasa inatosha. Ingawa naona utamu katika hali hii au ile, ingawa naweza kupangilia maneno mazuri kukitetea kilema changu lakini sasa basi, najiweka chini ya Mungu, nasafiri pamoja na Kristo kuelekea kilele cha wokovu wangu na wetu. Paji la unyenyekevu ndiyo nyenzo sahihi ya kutufikisha katika kilele cha maisha ya kipasaka kwani ni katika unyenyekevu ndipo tunapoweza kujisadaka nafsi zetu na kumsikiliza mwenyezi Mungu. Unyenyekevu hutufanya tuweze kutoka nje ya nafsi zetu na kumpatia Mungu nafasi atawale.

Shangwe zetu katika Dominika hii zitualike katika safari hiyo ya unyenyekevu. Tumsindikize Kristo katika safari yake wakati wa juma hili kuu huku tukiwa tayari tujiachanisha na matamanio yetu ya kibinadamu na hivyo kumpatia Mungu nafasi atende kadiri anavyotaka. Tutambue kwamba katika utii ndipo utukufu wa Mungu unatamalaki na utawala wake unakuwa juu yetu.

Kutoka studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.