2017-04-04 07:09:00

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya Vijana: Jumapili ya Matawi 2017


Maadhimisho ya Siku ya 31 ya Vijana Duniani sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ulikuwa ni muda muafaka wa kutafakari kwa kina na mapana Jubilei ya Vijana, kwa kuongozwa na watakatifu Yohane Paulo II na Mtakatifu Faustina Kowalska; mitume na mashuhuda wa huruma ya Mungu, ili kujibu kikalimifu changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo. Jubilei ya vijana duniani Jimbo kuu la Cracovia, ilikuwa ni nafasi ya kukuza na kudumisha udugu na furaha kwa kutoa ushuhuda wa matumaini sanjari na kufungua mioyo ya watu ili kujikita katika ujenzi wa madaraja ya watu kukutana.

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani inayoadhimishwa mwaka huu hapo tarehe 9 Aprili 2017 katika ngazi ya kijimbo. Jumapili ya Matawi, ni Siku ya Vijana Duniani, inayowapatia vijana nafasi ya kumzunguka Askofu wao Mahalia. Itakumbukwa kwamba, baada ya maadimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 huko Cracovia, Poland, kunako mwaka 2019 maadhimisho haya yatafanyika nchini Panama, kwa kusindikizwa nan a Bikira Maria ambaye vizazi vyote vinamwita mbarikiwa. Baba Mtakatifu anasema, maadhimisho ya Siku ya 32 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2017 yanaongozwa na kauli mbiu “mwenye nguvu amenitendea makuu”. Baada ya tafakari kuhusu Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu, katika kipindi cha miaka mitatu Bikira Maria atakuwa ni dira na mwongozo wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa kujikita katika: kumbu kumbu, ujasiri na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi; mambo msingi yanayofumbatwa katika maisha ya Bikira Maria.

Kwa ufupi, Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2017 inaongozwa na kauli mbiu “mwenye nguvu amenitendea makuu”. Lk. 1: 49. Kwa mwaka 2018 kauli mbiu itakuwa “Usiogope Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Ni nafasi ya kutafakari fadhila ya upendo inayofumbatwa katika ujasiri uliomwezesha Bikira Maria kupokea Habari Njema ya Wokovu. Kwa mwaka 2019 huko nchini Panama, Vijana watatafakari kwa kina tema ifuatayo “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyo nena”. Haya ni majibu muafaka yaliyotolewa na Bikira Maria kwa Malaika yakiwa yamesheheni sana matumaini.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2017 anakaza kusema, Mwezi Oktoba 2018, Mama Kanisa ataadhimisha Sinodi ya Maaskofu itakayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya miito”. Mababa wa Sinodi watapembua kwa kina na mapana jinsi ambavyo vijana wanavyomwilisha imani katika maisha na changamoto wanazokabiliana nazo. Wataangalia jinsi ya kukua na kukomaa katika maisha, mang’amuzi ya wito wao katika ndoa, kama waamini walei na wataalam katika medani mbali mbali za maisha sanjari na wito wa kipadre na kitawa. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu yatakwenda sanjari na maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2019 nchini Panama.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Bikira Maria aliposikia na kukubali mpango wa Mungu katika maisha aliondoka kwa haraka kwenda kumsaidia binadamu yake Elizabeth aliyekuwa ni mjamzito. Bikira Maria, akiwa bado ni msichana mbichi kabisa alikuwa amepewa zawadi kubwa sana maishani mwake, zawadi iliyokuwa inaandamana na changamoto zake; Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja naye, lakini hata hivyo bado alibaki na maswali mengi akilini na moyoni mwake, lakini hakumezwa na woga wala kiburi wala kuponda maisha ya ujana wake, bali aliondoka kwa haraka kwenda kumsaidia binadmu yake Elizabeth, huku akiwa anaongozwa na Roho Mtakatifu hakuona vikwazo, bali fursa ya kuweza kutafakari kwa kina na mapana matendo makuu ya Mungu katika maisha yake. Hivi ndivyo inavyotendeka hata katika maisha ya vijana wengi wanapokuwa katika hija, wanakumbuka matukio mbali mbali ya maisha na kuyapatia nafasi ya kukua sanjari na kuwa na mang’amuzi mapana zaidi ya wito uliofunuliwa kwa kukutana na Mwenyezi Mungu pamoja na huduma kwa jirani.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Bikira Maria alikutana na Elizabeth, huku wakiwa wamejazwa nguvu ya Roho Mtakatifu, furaha na mshangao mkuu, wakiwa wamebeba zawadi ya uhai, watoto wanacheza kufurahia maisha. Lakini, Elizabeth anashangazwa na imani ya Bikira Maria kiasi cha kupaaza sauti na kusema “Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana”. Imani ni kati ya zawadi kubwa ambazo Mwenyezi Mungu alimkirimia Bikira Maria; ni zawadi ambayo inapaswa kupokelewa kwa mikono miwili, ndiyo maana Elizabeth anambariki kwa zawadi hii na Bikira Maria anamjibu Elizabeth kwa utenzi wa “Magnificat” ambamo anasema “mwenye nguvu amenitendea makuu”.

Bikira Maria anasali sala ya kimapinduzi, inayomwonesha akiwa amesheheni imani sanjari na kutambua udhaifu na mapungufu yake ya kibinadamu, lakini daima alijiaminisha kwa huruma ya Mungu, ushuhuda wa ujasiri unaomwezesha kumshukuru Mungu kwa kwa kuwa ameuangalia unyenyekevu wa mjakazi wake na kutenda matendo makuu kwa maskini na wanyofu wa moyo. Imani ni kiini cha historia nzima ya maisha ya Bikira Maria. Utenzi wake unawasaidia waamini kutambua huruma ya Mungu ni injini ya historia ya mtu binafsi na ya binadamu katika ujumla wao.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwenyezi Mungu anapomgusa kijana, anakuwa na uwezo wa kutenda mambo makuu katika maisha, kama yale ambayo Bikira Maria anazungumzia katika utenzi wake, mambo yanayogusa pia safari ya maisha ya vijana wengi katika wasi wasi na mashaka, wanaweza pia kupata utimilifu wake. Baba Mtakatifu anatambua kwamba, vijana wanayo mapungufu yao, ni wadhambi, lakini Mwenyezi Mungu anapowaita anaangalia yale mambo msingi ambayo wataweza kutenda kwa siku za usoni kwa kujikita katika upendo. Kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, vijana wanaweza kutumia maisha yao katika kuboresha ulimwengu ili uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, kwa kuacha alama katika historia yao wenyewe pamoja na jirani zao.

Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana wamba, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria aliyeweza kuunganisha historia ya maisha yake na ya wahenga wake, hata wao wanahistoria ya Jumuiya ya watu waliowatangulia katika maisha, ni sehemu ya historia ya Kanisa inayofumbatwa katika Mapokeo yanayorithishwa kizazi baada ya kizazi kwa kurutubishwa na uzoefu wa kila mtu binafsi, kumbe hata wao ni sehemu ya historia ya Kanisa, mwaliko kwa vijana ni kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili waweze kuwa ni vyombo na wadau katika kazi ya ukombozi; kwa kuwajibika sanjari na kutambua matendo ya huruma ya Mungu katika maisha yao.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2017 anapenda kuwauliza ni kwa jinsi gani wanavyotunza kumbu kumbu za matukio mbali mbali ya maisha yao; madonda katika maisha; hakuna mtakatifu wala mdhambi asiyekuwa na historia ya mambo yaliyopita na yale yajayo! Yesu, kwa njia ya huruma na upendo wake, anaweza kuganga na kuponya majeraha yaliyojichimbia ndani kabisa ya mioyo ya watu na hivyo Mwenyezi Mungu kuonesha nguvu yake katika udhaifu wao. Vijana wajifunze kupokea historia ya maisha iliyopita, ili kuandika historia ya maisha yao kwa leo na kesho ijayo! Ni kazi ngumu lakini muhimu sana ili kutambua upendo wa Mungu unaounganisha matukio yote ya maisha.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kujenga utamaduni wa kutafakari kuhusu maisha yao, tayari kujiwekea malengo kwa siku za usoni, ili kutengeneza historia ya maisha ya kweli kwa kutambua kwamba, wao wenyewe wanapaswa kuwa ni wahusika wakuu wa historia na watu wanaoamua mustakabali wa maisha yao kwa siku za usoni. Baba Mtakatifu anawaalika vijana kufuata mfano bora wa Mama Bikira Maria kwa kuwa wameungana na historia yao ya zamani. Jambo hili linawezekana kwa kuchunguza dhamiri kila siku ili kuangilia yale mema na mazuri waliyotenda kwa siku hiyo na mabaya yaliyowaangusha; kwa kushuruku, kutubu na kujikabidhi mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Ni changamoto ya kusali kwa ajili, pamoja na juu ya maisha, ili kutambua matendo makuu ya Mungu katika medani mbali mbali za maisha.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Utenzi wa “Magnificat” unaonesha kwamba, Bikira Maria alikuwa anaufahamu mkubwa wa Maandiko Matakatifu; alifahamu sala ya watu wake urithi mkubwa kutoka kwa wazazi wake. Alikuwa ni msichana mwenye Ibada na amana kubwa ya imani iliyomwezesha kutunga utenzi wa “Magnificat” ambao umekuwa pia ni utenzi wa Kanisa. Changamoto kwa vijana ni kuifahamu Biblia, kulitafakari Neno la Mungu sanjari na kujenga utamaduni wa masomo ya kiroho yatakayopasha joto mioyo yao na kuangaza mapito wakati wa nyakati za giza. Bikira Maria anawafundisha vijana kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Ekaristi kama alama ya shukrani kwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu; Sakramenti ya Upatanisho kama mwanzo na hatima ya maisha yao, kwa kupyaisha maisha yao ya kila siku yanayogeuka kuwa ni utenzi wa kudumu kwa Mwenyezi Mungu. Vijana wafanye kumbu kumbu ya uwepo wa Mungu katika maisha yao kwa kujikita katika huruma na furaha ili kufuta madoa ya ubaya katika maisha.

Bikira Maria katika utenzi wa “Magnificat” anasaidiwa kwa namna ya pekee na imani, mtazamo na maneno ya binamu yake Elizabeth kutambua ukuu wa matendo na utume wa Mungu ambao amemkabidhi Bikira Maria. Vijana wanapokutana na wazee, wawe ni chemchemi ya utajiri kwa kujifunza hekima na dira kutoka kwa wazee pamoja na kupokea ushuhuda wa watu waliowatangulia, ili kujenga kesho imara na thabiti zaidi. Vijana wakumbuke kwamba, wao wana nguvu, lakini wazee kumbu kumbu na hekima kama alivyoshuhudia Elizabeth.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kuthamini Mapokeo na kuwa ni waaminifu kwa matendo makuu ambayo Mwenyezi Mungu anaendelea kutekeleza katika maisha yao ya sasa, changamoto ni kutambua asili yao ili kuweza kurejea tena katika mambo msingi, daima wakiwa na uaminifu unaojikita katika ugunduzi ili kuunda nyakati mpya ili kuendelea kuupyaisha ulimwengu. Vijana wawe na ujasiri wa kuthamini yaliyopita, yaliyopo na yale yajayo, kwa kuambata urithi wa tunu msingi za maisha ya ndoa, wito wa upadre na maisha ya kitawa; tunu ambazo kamwe haziwezi kupitwa na wakati bali yataendelea kuwa ni chemchemi ya furaha, ikiwa kama vijana watapata uzoefu na mang’amuzi ya upendo unaaomwilishwa katika uhalisia wa maisha yao kwa kutambua na kuitikia wito kutoka kwa Mungu, jambo linalowawezesha kuwa na furaha ya kweli.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa Siku ya Vijana Duniani inayoadhimishwa kwenye ngazi ya kitaifa na kijimbo kwa kuwakumbusha kwamba, maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya 32 ya Vijana Duniani huko Panama sanjari na maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018; lakini pia mwaka 2017 umesheneni matukio muhimu sana, kwani imegota miaka 300 tangu Bikira Maria wa Aparecida alipotokea nchini Brazil; Jubilei ya miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima, nchini Ureno na kwamba, anatarajia kwenda huko kama hujaji wa imani, kuanzia tarehe 12 – 13 Mei 2017.

Mtakatifu Martin, mmoja watakatifu wasimamizi wa Amerika ya Kusini na Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama, katika shughuli zake za kawaida alikuwa na mazoea ya kumpatia Bikira Maria maua mazuri, kama alama ya upendo wake kwake. Baba Mtakatifu anawataka vijana kujenga urafiki na mazoea ya kujiaminisha kwa Bikira Maria, kwa kumtolea furaha, matatizo na wasi wasi wao, kwani kamwe hawatajutia kuzaliwa!. Bikira Maria sehemu mbali mbali za dunia anasema Baba Mtakatifu Francisko amejifunua kwa sura na majina mbali mbali ili kuwa karibu zaidi na watoto wake, awaombee kila mmoja wao na awasaidie kuimba matendo makuu ya Mungu anayotenda kwa njia yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.