2017-04-04 07:51:00

Maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana, Oktoba, 2018


Askofu Fabio Bene, Katibu mkuu msaidizi wa Sinodi za Maaskofu katika uzinduzi wa Hati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Mkutano wa XV wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana unaoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito” itakayoadhimishwa kunako mwaka 2018 anasema, Kanisa linataka kuwashirikisha kikamilifu vijana katika maandali na hatimaye maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana.

Dhamana hii inatekelezwa kwa njia ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, Makanisa mahalia pamoja na wadau mbali mbali, ili kweli vijana kutoka katika medani mbali mbali za maisha, waweze kusikilizwa, ili hatimaye, Kanisa liweze kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya vijana: kiroho na kimwili, mintarafu mwanga wa Injili. Kanisa linataka kujenga na kudumisha utamaduni wa kuwasikiliza vijana kwa makini, ili kusikia hamu inayobubujika kutoka katika sakafu ya maisha yao, mipango na miradi yao ya maisha; ndoto, changamoto na kinzani wanazokutana nazo katika uhalisia wa maisha ya kila siku! Ushiriki wao katika maisha na huduma za kijamii na Kikanisa.

Askofu Fabio Bene anakaza kusema, Kanisa linataka kujenga na kudumisha utamaduni wa kuwasikiliza vijana, kama alivyowahi kukazia Mtakatifu Benedikto, Abate kwa kusema kwamba, hata vijana wanapaswa kusikilizwa maoni yao kabla ya kufanya maamuzi msingi katika maisha, jambo ambalo pia linapewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake kwa Vijana kwa Mwaka 2017 kama sehemu ya maandalizi ya mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana hapo mwaka 2018.

Mwelekeo huu mpya unafumbatwa katika taalimungu, kwani mara nyingi Mwenyezi Mungu ameamua kujifunua kwa njia ya vijana! Kwa mawazo, maneno, lakini zaidi kwa njia ya uwepo wao katika maisha na utume wa Kanisa kama anavyokaza kusema, Mtakatifu Yohane Paulo II. Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu itaanzisha mtandao wa kijamii ili kuweza kupata maoni kutoka kwa vijana sehemu mbali mbali za dunia. Majibu ya maswali haya msingi, yatakuwa ni sehemu ya maandalizi ya Hati ya Kutendea Kazi, yaani “Instrumentum Laboris” pamoja na mawazo mbali mbali yatakayokuwa yamekusanywa kutoka kwenye Mabaraza ya Maaskofu Katoliki na Makanisa mahalia. Baba Mtakatifu Francisko ataendelea kutoa Katekesi kuhusu maisha na utume wa Vijana ndani na nje ya Kanisa ili kuwasaidia vijana kupata mang’amuzi mapana zaidi katika maisha na utume wao.

Kabla ya maadhimisho ya Jumapili ya Matawi kwa mwaka 2017 ambayo kimsingi ni Siku ya Vijana Kijimbo, Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu itafanya mkutano wa kimataifa kuanzia tarehe 5- 8 Aprili 2017 ili kuangalia mchakato wa kipindi cha mpito kutoka maadhimisho ya Siku ya Vijana huko Cracovia, Poland hadi kuelekea Siku ya Vijana Duniani huko Panama kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha. Hapa, wawakilishi wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia watapewa hati ya maandalizi mintarafu Makanisa mahalia. Ijumaa jioni tarehe 7 Aprili 2017 kutakuwa na tamasha la Muziki kwa vijana wa kizazi kipya! Hii itakuwa pia ni fursa kwa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia kutoa ushuhuda wa maisha, imani na matumaini yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Tamasha hili linapania kuwa ni daraja la majadiliano ya kina na vijana wa kizazi kipya. Tarehe 8 Aprili 2017 kutakuwa ni Mkesha wa Sala kwa ajili ya kuombea Siku ya Vijana Kijimbo kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Roma. Kanisa hili limechaguliwa kama sehemu ya mchakato wa maandalizi ya Siku ya Vijana Duniani itakayoadhimishwa nchini Panama kunako mwaka 2019.

Mama Kanisa anapenda kutumia maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana ili kufanya upembuzi yakinifu katika maisha ya vijana wa kizazi kipya. Mwezi Septemba, 2017 kutafanyika semina kuhusu vijana kwa kuwashirikisha wataalam na mabingwa wa utume wa vijana kutoka sehumu mbali mbali za dunia katika maandalizi haya. Kanisa linataka kutekeleza wajibu wake wa kulipa deni kubwa mbele ya vijana, kwa kuwajibika barabara na kuwaandalia sera na mikakati makini ya elimu na maeneo mbali mbali ili kweli vijana ambao ni jeuri ya Kanisa na Jamii, waweze kutekeleza ndoto yao ya kujenga leo na kesho iliyo bora zaidi inayojikita katika haki na udugu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.