2017-04-03 07:29:00

Makovu ya tetemeko la ardhi yawatie matumaini, ari na moyo mkuu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 2 Aprili 2017 ametembelea eneo la Mirandola, Jimbo Katoliki Carpi na kuzungumza na familia ya Mungu iliyoathiriwa sana na tetemeko la ardhi kunako mwaka 2012 na kuonja mshikamano wa dhati na Kanisa kwa njia ya Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI na kwamba, uwepo wake miongoni mwao ni kutaka kuwaimarisha na kuonesha uwepo wa Kanisa kati yao, hasa wakati huu wanapoendelea na ujenzi pamoja na ukarabati wa miundo mbinu. Baba Mtakatifu amewapongeza na kuwashukuru wadau mbali mbali waliojisadaka bila ya kujibakiza ili kurejesha tena hali ya maisha ya kawaida miongoni mwa watu wa Mungu hapo Mirandola.

Baba Mtakatifu anasema, kwa hakika tetemeko la ardhi lilisababisha madhara makubwa kwa amana, rasilimali na utajiri wa eneo hili kiutu na kitamaduni bila kusahau uharibifu mkubwa uliojitokeza kwa makazi ya watu, shughuli za uzalishaji mali na hutoaji wa huduma; Makanisa, sanaa na ustaaarabu wa watu. Kuna watu walipoteza maisha, wakapata vilema na wengine kupata majeraha makubwa katika maisha.

Lakini pamoja na yote haya, bado watu wameshuhudia utu na heshima ya binadamu; mshikamano na upendo wa Kiinjili; kwa kutambua na kupokea uwepo wa Mungu mwingi wa huruma na mapendo hata katika matukio kama haya yanayowagusa na kuwatikisa wengi! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, familia ya Mungu eneo la Mirandola itaendelea kuwa na matumaini, nguvu na ujasiri wa kusonga mbele bila kukata wala kukatishwa tamaa na shida pamoja na changamoto za maisha. Mengi yamefanyika katika ujenzi na ukarabati wa miundo mbinu na maeneo muhimu katika historia na maisha ya watu. Haya ni maeneo ambayo yanawasaidia watu kujenga mafungamano ya kijamii na kikanisa. Ni matumaini ya wengi kwamba, shughuli za ujenzi na ukarabati wa maeneo yaliyobakia utaendelezwa kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya wengi. Baba Mtakatifu amewakumbuka wahanga wa tetemeko la ardhi eneo hili, ndugu na jamaa ya wale wote walioathirika na ambao bado wanaendelea kuishi katika hali ya wasi wasi, ili wote hawa waweze kupata msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu amewakumbusha wananchi wa Mirandola kwamba, baada ya siku chache, Kanisa litaadhimisha Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko kwa Kristo Yesu! Kristo Mfufuka awasaidie katika dhamana na kazi ya kukamilisha kazi ya ujenzi na ukarabati kwa kuwapatia matumaini, Bikira Maria na watakatifu wasimamizi wao wawatie shime na nguvu wale wote ambao bado wanateseka sana kutokana na tetemeko hilo, ili waweze kupata mwanga na nguvu ya kutekeleza mambo ambao ni matumaini ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.